Social Icons

Tuesday, 1 September 2015

Kwa nini mkulima Mwamwindi alimpiga risasi RC, Dk. Kreruu? VII

Na Maggid Mjengwa

KWENYE mazungumzo yangu na Mzee David Butinini mtakumbuka nilimuuliza; Mmoja wa wazee nilioongea nao kwa simu na natarajia nitakutana naye kwa mazungumzo ya ana kwa ana ni mkulima Mzee Pesambili na ambaye alikuwa rafiki wa Said Mwamwindi. Huyu bwana ni mmoja kati ya wale waliokamatwa na kuwekwa kizuizini. Je, unafikiri ataniambia nini kuhusu kilichotokea?

Mzee Butinini alinijibu; Mzee Pesambili is still bitter! Unasikia, huyu bwana ana machungu sana. Na nadhani huenda atafurahi kuongea nawe ili aseme machungu yake. Na wakati nakuja kukutana na wewe, nimemwona  anatembea kwa miguu pale Stendi ya Daladala ya Miyomboni. 


Amevalia pama lake. Hatukusalimiana. Ukiongea nae ujue kuwa utakutana na mtu mwenye machungu ya yaliyomkuta.


Maana, usiku ule wa tukio aliposikia polisi tunamfuatilia alikimbia makazi yake.  Akaenda kukamatiwa Mufindi huko. Na baadaye akapelekwa kusikojulikana. Aliporudi akakikuta kiwanja chake pale Kihesa kimechukuliwa. Kimsingi maisha yake yakaharibika. Ari na moyo wa  kuendelea na kilimo ikamwishia. Kuna mifano mingine ya watu kama mkulima Pesambili,” anasema Mzee Butinini.


Taarifa hizi za kamata kamata  kwa  baadhi ya wakulima wakubwa bado ziko kwenye kumbukumbu za baadhi ya wenyeji wa Iringa. Kuna taarifa pia za wenyeji wa Iringa kuonyesha wazi  hisia zao za kuchukukizwa na uongozi wa  Dk. Kleruu na hivyo kuwa tayari kusimama upande wa mkulima Mwamwindi.


Kuna taarifa za  kuwapo kwa wakulima waliochangishana fedha kwa madhumuni ya kukodi wakili kutoka Uingereza aje kumtetea Mwamwindi kwenye kesi hiyo. Inasemekana vyombo vya usalama viliinasa orodha ya majina ya waliochangisha fedha na iliitumia orodha hiyo katika zoezi la kumkamata mmoja baada ya mwingine miongoni mwa wachangiaji.


Hali ilikuwa ni ya shaka sana wakati huo. Kuna wakati, wanafunzi wa Chuo cha Ualimu waliambiwa waandamane kupinga kitendo cha mauaji kilichofanywa na mkulima Mwamwindi. Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo ya mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho waliokuwepo wakati huo, mandamano hayo ilibidi wayatawanye wenyewe mara walipoingia mitaa ya mji wa Iringa, maana, walikutana na sura nyingi za wenyeji wa Iringa walioonyeshwa kukerwa na kitendo kile cha wanafunzi kuandamana.


” Tulihofia tusije tukapigwa mishale, tukatawanyika wenyewe kurudi chuoni,” anasema mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho ambacho baadaye kikaja kujulikana kama Chuo Cha Ualimu Cha Kleruu”.


Hakika, tukio lile la  Mkuu wa Mkoa kupigwa risasi na Mkulima Mwamwindi halikutikisa Iringa tu, bali nchi nzima. Na kwenye maeneo mengine ya nchi hii watu wa kabila la Wahehe walihofiwa kwa kudhaniwa ni wenye hulka ya kuua kama  Mwamwindi. Ikafika wakati, nje ya Iringa, mwanamume wa Kihehe akiingia kwenye baa, kuna  wenyeji wa sehemu hizo waliotania kwa kusema;  ameingia Mwamwindi.


Na taarifa juu ya siku ile ya tukio la mauji zimekuwa zikiwachanganya wengi hadi hii leo. Kupitia mfululizo wa simulizi hizi, zimeanza kujitokeza taarifa mpya zinazotoa mwanga wa kilichotokea. 

Mathalan, kuna polisi  mstaafu aitwaye Mushi na ambaye kwa sasa anaishi Moshi akiendesha kampuni ya ulinzi ana haya ya kusema; Bwana Maggid, mimi nilikuwa kaunta siku ile ya tukio; Jumapili ya Krismasi, Desema 25, 1971. Bwana Butunini uliyeongea naye tulikuwa naye pale polisi Iringa. 


Siku ile ya tukio, asubuhi kabisa Dk. Kleruu alifika pale polisi baada ya kutoka kwa RPC Aboubakar.

Kleruu na mimi tulikuwa marafiki baada ya kumsaidia kwenye upepelezi wa wizi uliotokea nyumbani kwake na nikafanikiwa kupata vitu vyake karibu vyote vilivyoibwa nyumbani kwake. 


Ulikuwa wizi wa ajabu maana nyumba ya Mkuu wa Mkoa ilikuwa inalindwa,” anasema Mushi. Kisha anaendelea kusimulia; Tangu hapo tukawa na  uhusiano wa kirafiki na Mkuu wa Mkoa Kleruu. 


Nakumbuka siku ile ya tukio alipofika pale kituoni aliniaga kwa kuniambia anaenda Nyang’olo kwenye mambo ya kilimo. Kisha akanikaribisha jioni hiyo niende nyumbani kwake nikale Krismasi. Basi, baadaye tukajua kuwa afande RPC Aboubakar alimwambia ampe walinzi wa kwenda nao, lakini Kleruu alikataa.”


Basi, jioni ile ndio tukaona gari lake likingiia kituoni. Aliyeliendesha hakuwa Dk. Kleruu. Mimi ndiye niliyepokea bunduki aliyoikabidhi Mwamwindi. Ilikuwa ya midomo miwili. Hata gari la Mkuu wa Mkoa ndiye mimi niliyeliendesha kulizungusha kule uani polisi baada  ya mwili wa marehemu kutolewa,” anasema polisi mstaafu Mushi.


Hakika, maelezo hayo yanathibitisha  kitendawili kigumu juu ya kilichotokea siku hiyo. Kama ilivyoelezwa huko nyuma na Amani Mwamwindi. Huyu ni  mtoto wa mkulima Mwamwindi. Alisema haya; ” Siku hiyo Kleruu, pamoja na kuwa ni Mkristo, aliamua kutokula Krismasi.


 Alivaa kofia yake ya pama. Kleruu akaendesha mwenyewe gari lake la mkuu wa mkoa aina ya Peugeot Injection, rangi ya bluu. Katika orodha yake, Kleruu alikuwa na watu watatu wa kuwashughulikia miongoni mwa wakulima wale wakubwa wa Isimani. Target nambari moja alikuwa Rashid Juma wa Nyang’olo. Nambari mbili ni marehemu baba. Namba tatu simjui.


Kleruu alipofika Nyang’olo hakumkuta mkulima Rashid Juma. Siku hiyo ya Krismasi Rashidi Juma alipata habari, kuwa kuna ng’ombe wake walipotelea milimani. Alikwenda huko milimani kusaka ng’ombe wake. Hivyo, Kleruu akafunga safari kurudi kwa target namba mbili, baba yangu Mzee Mwamwindi. Ni njia hiyo hiyo, Nyang´olo iko mbele ya ilipokuwa ngome ya mzee.”


”Basi, Kleruu akafika kwa Mzee. Baba akiwa shambani akaliona gari la Kleruu limesimama nje ya mji wake. Kisha akamwona Kleruu akitembea kumfuata shambani. Baba alihisi tu, kuwa Kleruu amekuja na shari.


Kleruu akamuuliza Mzee kwa ukali, ”Mbona mnafanya kazi leo siku ya Krismasi?” Baba akamwomba Kleruu waende wakuzungumze nyumbani. Akamwambia mdogo wangu Mohammed aendelee kulima. Mzee akatangulia mbele, nyuma anamfuatia Kleruu. 


Kabla ya kufika kwenye nyumba yake wakayapita makaburi. Kleruu akamtamkia baba mzee Mwamwindi; Hapa ndipo unapozika mirija yako?” Alitamka hivyo huku akimtomasa tomasa mzee na kifimbo alichoshika mkononi.


Jambo hilo lilizidi kumkasirisha marehemu mzee. Akafika nyumbani kwake. Mlangoni alisimama mke wake mdogo. Inaonekana mzee alishafanya uamuzi. Jana yake alikwenda kuwinda. Hakupata mnyama. Bunduki yake moja aina ya riffle kati ya bunduki zake mbili ilikuwa bado ina risasi. Akamwambia mke wake mdogo huku Kleruu akiwa anasikia; kanichulie bunduki yangu,” anasema Amani Mwamwindi, mtoto wa Mkulima Mwamwindi.


Mwanga zaidi juu ya  tukio hili unazidi kupatikana. Lakini, kuna mengine yanayotakiwa kufanyiwa utafiti ili kubaini ukweli wa kilichotokea. Bila shaka, mahojiano yangu na mkulima Pesambili na  ambaye alikuwa ni rafiki wa mkulima Mwamwindi  yatatupa mwanga mwingine. Na kuna wengine wanaozidi kuchangia katika kutupa mwanga. Na je, ni nini tafsiri ya hukumu ya kesi ya Mwamwindi.


Siwezi kuyasimulia yote haya kupitia makala za gazetini. Wasomaji wengi wameniomba niandike kitabu. Nakubaliana nao, hivyo, nakiandaa sasa kijitabu kidogo kinatakachoweza kutupa undani wa kilichotokea siku ya Krismasi, Desemba 25, 1971. Na tuvute subira kukisubiri kijitabu hicho.


Chanzo.Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates