Na Joseph Mihangwa
Yote haya yanaturejesha kwenye swali letu la awali: je, kuuawa kwa Karume kulikuwa na lengo la kulipiza kisasi kwa chuki binafsi, kama baadhi ya watu wanavyodai, au lilikuwa jaribio la Mapinduzi lililoshindwa kwa Serikali ya Mapinduzi? Ni nani huyu Luteni Hamoud Hamoud aliyeongoza mauaji na kwa nini?
Je, lengo lilikuwa ni mauaji hayo pekee au kulikuwa na mpango mkubwa zaidi nyuma? Ukiongozwa na nani?
Kupata majibu ya maswali haya, hatuna budi kuiangalia hali ya kisiasa Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na baada ya Muungano na Tanganyika, Aprili 26, 1964.
Kama nilivyoeleza katika mfululizo wa makala nne hivi karibuni katika gazeti hili kuhusu jinsi “Field Marshal” John Okello alivyoongoza Mapinduzi ya 1964, na kuundwa kwa Serikali ya Mseto kati ya vyama vya ASP na Umma, lengo kuu la Karume lilikuwa ni kuzivunja nguvu za wanaharakati wa Umma Party na za wakomunisti wa ASP walioshabihiana kimawazo na kimtazamo wa kitaifa na wana-Umma Party na kumnyima Karume usingizi.
Lakini tofauti na matarajio ya Karume, hatua hiyo iliwaleta karibu zaidi wanamapinduzi hao na kumnyima zaidi usingizi kwa hofu ya kupinduliwa, wakimtuhumu kushindwa kuongoza na kusimamia madhumuni ya Mapinduzi Visiwani.
Mungu bariki kwa Karume, ukatokea Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika mwaka huo, akaona vyema awasambaratishe kwa kuwatafutia nafasi Tanzania Bara ambako wasingeweza kufurukuta.
Waliokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na Abdulrahman Babu (Umma) na aliyepewa Uwaziri wa Mipango na Uchumi kwenye Serikali ya Muungano; Kassim Hanga (ASP) aliyeteuliwa Waziri katika Ofisi ya Rais wa Jamhuri, Mambo ya Muungano; Salim Ahmed Salim (Umma) aliyeteuliwa Balozi nchini Misri.
Wengine ni Othman Sharrif (ASP) aliyeteuliwa Balozi nchini Marekani, lakini Karume akampinga Nyerere akidai hastahili, uteuzi ukafutwa; badala yake akateuliwa kuwa afisa mifugo katika moja ya mikoa ya Kusini Tanzania, Mbeya au Mtwara, na Kanali Ali Mahfoudh (Umma) aliyeteuliwa Mkurugenzi wa Operesheni katika Jeshi la Wananchi (JWT), na wengineo.
Kwa wale wenye maoni tofauti na ya kukosoa Serikali waliobaki Visiwani, hasira ya Karume aliyetawala kwa mkono wa damu iliwashukia, wengi walikamatwa na kutiwa kizuizini na pengine kupoteza au kuuwawa kikatili na katika mazingira ya kutatanisha. Mmoja ya waliouawa kikatili kizuizini ni Mzee (mwanaharakati) Mohamed Hamoud, baba yake Luteni Hamoud Mohamed muuaji wa Karume.
Tangu Mapinduzi ya Januari 12, 1964, Zanzibar haikuwa na Katiba wala Sheria; iliongozwa kwa Amri za Rais (Presidential Decrees) kadri alivyoona inafaa. Na kwa mujibu wa Gazeti la “The Tanganyika Standard” la March 9, 1968, Karume aliapa kutofanya uchaguzi wala kuwa na Katiba Kisiwani kwa miaka 50 tangu 1964 - 2014 Kwa madai kwamba “chaguzi zote ni vyombo vya mabeberu kuwakandamiza wananchi”.
Na kadiri kalamu ya Karume ya wino wa damu ilipozidi kuandika historia ya ukatili, udikteta na umwagaji damu kwenye kurasa ngumu za kukwaruza ndivyo alivyojichongea na kujiongezea upinzani na uadui kwa jamii ya Kizanzibari.
Kufikia mwaka 1967 hofu ya Karume dhidi ya wenzake na kwa nafasi yake ilitia fora kiasi cha kuogopa kivuli chake mwenyewe. Na ili kuendelea kuwamaliza wenzake, mwaka huo zilitungwa tuhuma za uongo dhidi ya watu 14 makada wa ASP katika kumpindua, zikiwalenga hasa wenye fikra za kikomunisti.
Walioingizwa kwenye tuhuma hizo ni pamoja na mawaziri wa Serikali yake mabwana Abdallah Kassim Hanga, Salehe Saadallah Akida, Abdul Aziz Twala na makatibu wakuu wa wizara, Aboud Nadhif na Mdungi Ussi na baadaye Othman Sharrif.
Wote waliokuwa Visiwani walikamatwa, kisha Karume akamwomba Nyerere kuwarejesha Zanzibar kutoka Bara, Othman Sharrif na Hanga ili “wakahojiwe” lakini wote wakaishia kuuawa kikatili bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mmoja wa mashahidi wa uongo walioandaliwa dhidi ya “watuhumiwa” kwa vyombo vya Karume, alikuwa Ahmada ambaye kwa uongo wake, watu wanne akiwamo Hanga, Twala, Saadallah na Othman, walinyongwa mwaka 1969. Kwa uongo huo, Ahmada alizawadiwa cheo cha kapteni jeshini. Ni Kapteni Ahmada huyu, aliyeshiriki kwenye mauaji ya Karume miaka mitatu baadaye.
Kwa hofu ya jamii ya Kizanzibari kufikiwa na fikra na mawazo mapya ya kimaendeleo, Karume alipiga marufuku vijana wa Kizanzibari kwenda nje kwa masomo ya juu ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam; alipiga marufuku pia ujenzi wa Chuo Kikuu Visiwani.
Mbali na kutokuwapo kwa utawala wa sheria enzi za Karume, unyanyasaji wa kijinsia na ubaguzi kwa misingi ya historia na kisiasa ulitia fora. Kwa mfano, mwaka 1966, alitoa amri (decree) kuwanyima wazazi haki ya kuwakataa wanaume walioposa binti zao kama njia ya kuondoa ubaguzi wa rangi.
Kwa sababu hii, wasichana, hasa wale wa Kiarabu walilazimishwa kwa nguvu ya Serikali kuolewa kwa nguvu. Karume mwenyewe, wakati huo akiwa na umri wa miaka 65, aliwania kuoa kwa nguvu, wasichana wanne wa Kiajemi, na alipokataliwa, aliamrisha wazazi wao watiwe kizuizini na kuchapwa viboko kwa kosa la kuzuia mpango wa ndoa mchanganyiko, na baadaye kutimuliwa Zanzibar.
Chini ya mpango huo, raia wa kigeni waliotaka kuchumbia wasichana wa Kizanzibari walitakiwa kuilipa Serikali Sh. 64,000,000, bila hivyo hawakuruhusiwa kuwaoa.
Karume alikuwa ameanza kuwa mwiba kwa Mwalimu Nyerere pia juu ya Muungano. Kwa mfano, alimkatalia Nyerere kwa lugha ya dharau na kejeli juu ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha kutumika Zanzibar.
Na kuhusu akiba ya fedha za kigeni ya Zanzibar iliyofikia dola milioni 80 mwaka 1972, alimuonya asithubutu kuitolea macho, akamwambia: “Fedha ya kichwa cha Malkia si yako na usiniulize, labda niulize juu ya hii (sh.) yenye picha ya kichwa chako”.
Na kuhusu Muungano, Karume alikuwa ameanza kuchoka nao. Siku moja alisema, “Muungano ni kama koti tu; likikubana unalivua”.
Ufa huu kati ya viongozi hao wawili juu ya Muungano, ndio uliosababisha kamati ya kupendekeza Katiba (Constitutional Committee) isiundwe na Bunge la Katiba (Constitutional assembly) lisiteuliwe ndani ya muda wa mwaka mmoja tangu Muungano, kama ilivyotakiwa chini ya Mkataba wa Muungano wa Sheria ya Muungano ya 1964.
Wadadisi wa mambo ya siasa wanakubaliana kuwa, kama Karume angeendelea kutawala miaka kadhaa baada ya 1972, Muungano ungefikia kikomo kwa njia ya kutisha na kusikitisha.
Kufikia mwaka 1972, upinzani kwa Serikali ya Karume ulikuwa umechukua harakati za uasi wa umma, chini kwa chini kwa mara ya kwanza tangu Hanga na wenzake wanyongwe mwaka 1969.
No comments:
Post a Comment