Na Joseph Mihangwa.
Miaka 40 iliyopita, Aprili 7, 1972; Rais wa Serikali ya awamu ya kwanza ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, ambaye pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abeid Amani Karume, aliuawa kwa kupigwa risasi katika mazingira na sababu za kutatanisha.
Risasi nane zilitolewa mwilini kwake mwili wake ulipofikishwa kwenye Hospitali ya V. I. Lemin, mjini Unguja kwa uchunguzi, sawa na idadi ya miaka minane ya utawala wake tangu 1964 hadi kifo chake.
Ilikuwa hivi: Rais Karume na Makomredi wenzake wa Chama cha Afro-Shirazi (ASP) alikuwa na mazoea ya kucheza karata, damma au dhumuna kwenye ukumbi wa ofisi za makao makuu ya Chama hicho Kisiwandui, kila jioni kama sehemu ya mapumziko. Siku hiyo alifika saa 11.00 jioni akiwa na walinzi wake, akaingia ndani nao wakabaki nje kulinda.
Ikafika zamu yake kucheza; akawa anacheza na Mzee Maalim Shaha Kombo ambaye alionekana kulemewa. Ndipo Karume akamwita Mzee Mtoro Rehani ajitayarishe baada ya Kombo, naye akaitikia kwa kuaga kwanza aende msalani kujisaidia.
Sekunde chache baada ya hapo na kabla Mzee Mtoro Rehani hajarejea kutoka msalani, ghafla watu wawili wenye silaha walivamia chumba alimokuwa Karume na wenzake na kumimina risasi wakimlenga; na kufumba na kufumbua, akawa katika dimbwi la damu kimya, amepoteza uhai. Hakuna mtu mwingine aliyeuawa mbali na kujeruhiwa tu, mmoja wao akiwa Katibu Mkuu wa ASP, (sasa) Hayati Thabit Kombo Jecha.
Risasi uaji (the fatal bullet), mbali ya risasi zote, iliyochukua uhai wa Karume ilitoka kwenye bunduki ya Luteni Hamoud Mohammed Hamoud wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT), ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa uvamizi huu na aliyefyatua risasi ya kwanza wakati Karume akicheza na wenzake. Inasemekana, Hamoud aliuawa papo hapo na mlinzi wa Karume.
Wauaji wengine waliofuatana na Hamoud katika uvamizi huo ni Kapteni Ahmada Mohamed, Koplo mmoja wa jeshi ambaye jina lake halijafahamika hadi leo, na raia mmoja aliyekwenda kwa jina la Ali Khatibu Chwaya, ambao inaelezwa wote hao waliuawa kwenye mapambano ya silaha nje ya eneo la tukio.
Dakika chache baada ya mauaji kutokea, alifika Kanali Ali Mahfoudhi na askari mwingine, Kapteni Makame Hamis, wakauchukua mwili wa Karume na kuukimbiza hospitali.
Itakumbukwa, Kanali Mahfoudhi ni mmoja wa vijana wa Umma Party (UP) cha Abdulrahman Mohamed Babu, kilichoungana na ASP baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na kuunda Serikali ya mseto. Ni kati ya vijana waliopelekwa Cuba kwa mafunzo ya kijeshi, na ni mmoja wa wapiganaji walioendesha mapambano ya kisayansi usiku wa Mapinduzi na kukamata uwanja wa ndege mchana Aprili, 1972.
Ni mmoja wa wanaharakati wa siasa za mrengo wa Kikomunisti ambao hawakutakiwa Zanzibar wakati wa utawala wa Karume, hivi kwamba kufuatia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26, 1964, Karume alishinikiza kwa Nyerere wapewe kazi Tanzania Bara aweze “kupumua” ambapo Mahfoudhi alipewa cheo cha Mkurugenzi wa Operesheni katika JWT.
Wengine ambao hawakutakiwa ni pamoja na Babu mwenyewe aliyepewa Uwaziri wa Mipango ya Uchumi, na kama tulivyoona makala zilizopita, hasimu mwingine wa Karume, Othman Sharrif, ambaye alifanywa Afisa Mifugo wa Mkoa, Mtwara au Mbeya, na Balozi Salim Ahmed Salim wakati huo Balozi wa Zanzibar nchini Misri ikaridhiwa aendelee kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano nchini humo.
Tuache hayo, lakini hapa swali linazuka: Kwa kuwa Kanali Mahfoudh hakuwa kipenzi cha utawala wa Karume tangu mwaka 1964, ilikuwaje akawa Afisa wa kwanza kuwa kwenye tukio kabla ya maafisa wengine vipenzi, kama vile Kanali Seif Bakari ambaye alikuwa pia Mkuu wa Usalama wa Taifa Zanzibar ambalo halikuwa jambo la Muungano, na wengineo?
Je, alikuwa katika ziara ya kikazi wakati mkasa huu ukitokea au alijua kilichotarajiwa kutokea? Kwa nini alikuwa mmoja wa washitakiwa zaidi ya 100 kwa tuhuma za mauaji hayo, na mmoja wa watuhumiwa 18 miongoni mwa hao walioshitakiwa wakiwa Tanzania Bara, Abdulrahman Babu akiwa mmoja wao.
Kuna dhana mbili kinzani kuhusu jinsi Karume alivyouawa na hatima ya wauaji. Dhana moja inadai kwamba, watu wanne walivamia mahali alipokuwa Karume na wenzake, wakamimina risasi mara nne au mara tano hivi, risasi ya kifo ikampata Karume shingoni akafa, huku zingine zikiendelea kumiminwa kulenga meza walipokuwa.
Inadaiwa kuwa Hamoud aliuawa kwenye eneo la tukio, ambapo wawili waliuawa baadaye na vyombo vya usalama (kwa mapambano?) na mmoja alijiua.
Dhana ya pili inadai kwamba Hamoud alikufa kwenye eneo la tukio katika mazingira ya kutatanisha, ama kwa kujipiga risasi kuepuka kukamatwa hai na kuteswa baada ya kuona asingeweza kutoroka; au alijeruhiwa vibaya na walinzi wa Karume, kisha Ahmada akampiga risasi na kumuua kumwepusha kuteswa na kutoa siri kama angekamatwa hai, kisha (Ahmada) akaweza kutoroka kwenye eneo la tukio.
Juu ya utata huu kuhusu hatima ya wauaji, ni ukweli kwamba ni Luteni Hamoud pekee aliyeuawa kwenye eneo la tukio na washiriki wengine katika mauaji waliweza kutoroka eneo la tukio na baadaye kuuawa katika mazingira yasiyofahamika.
Kufuatia mauaji hayo, watu 1,100 walikamatwa na kuhojiwa juu ya kuhusika au kutohusika kwao na mauaji, wengi wakiwa viongozi na wanachama wa zamani wa Umma Party, chama cha Babu na wanachama mashuhuri wa ASP wenye siasa za mrengo wa kikomunisti.
No comments:
Post a Comment