Na. Joseph Mihangwa
Kila mgombea alijinadi kwa kuahidi maisha na huduma bora kwa Mtanzania bila kumung’unya maneno: elimu bure kuanzia chekechea hadi Chuo Kikuu, huduma bora ya tiba na afya kwa kila mtu na hata hifadhi ya jamii kwa kila mwananchi; kufufua viwanda pamoja na kujenga vipya, maji, barabara na mengine yenye kugharimu mabilioni ya fedha tunazoambiwa leo hazipo kwa kuwa tu “masikini” wa kutupwa.
Wagombea wote walilikataa hilo wakisema uwezo huo tunao ila kwa sababu tu ya ufisadi unaolifukarisha taifa kwa kuporwa rasilimali zake na tabaka la wachache.
Hatuna sababu ya kutowaamini wagombea hao kwani tumeshuhudia tunavyoporwa kupitia mikataba mibovu ya uwekezaji kama ule wa umeme wa IPTL uliolitafuna taifa kwa miaka 20 bila umeme stahiki, na sasa imeagizwa tuuhuishe ili fisadi azidi kutukamua; wizi wa dhahiri katika taasisi za umma na utoroshaji wa rasilimali uliokithiri bila hofu kufikia kutoroshwa kwa twiga kwa ndege; ubinafsishaji na “uwekezaji” usiojali kufikia viongozi kujimilikisha migodi na rasilimali zingine za taifa.
Ilitarajiwa tabia hii, ya wenye nguvu kupora kadri ya ukali wa meno yao, ingekomeshwa kupitia Katiba mpya kwa kuweka maadili ya taifa, wajibu na miiko ya viongozi kama ilivyopendekezwa na Tume ya Katiba ya Jaji Joseph Sinde Warioba; lakini mafisadi wenye ushawishi wa kisiasa na rushwa ndani ya mfumo, wakafanikisha kunyofolewa kwa vipengele hivyo kuruhusu ufisadi uendelee.
Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani bila mkakati wenye kueleweka dhidi ya ufisadi huu; na kama tutaendelea kuuchekea, tujiandae kwa machafuko yaliyosambaratisha Zaire (sasa DRC) ya Jenerali Mobutu Seseseko mwaka 1997 kwa tabia na mazingira yanayoshabihiana, kama tutakavyoona katika makala haya.
Aliponyakuwa madaraka kwa njia ya mapinduzi kutoka kwa Rais Joseph Kasavubu, mwaka 1965, Jenerali Mobutu alitoa sababu za kufanya hivyo: kwamba, “Wanasiasa wameiteketeza nchi kiuchumi na kijamii kwa uchu wa kujaza mifuko na matumbo yao, na kuiweka rehani kwa ubeberu wa kimataifa”. Siku hiyo, mawaziri wanne wa serikali iliyopinduliwa walihukumiwa kifo na Mahakama ya Kijeshi, na siku mbili baadaye walinyongwa mbele ya umati wa watu 50,000.
Huu ulikuwa ukatili wa pili wa aina yake, uliofanywa na Mobutu, kufuatia ule wa kuuawa kikatili kwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo, Patrice Emery Lumumba mwaka 1961 na Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA), wakati huo Mobutu akiwa Mkuu wa Jeshi.
Mobutu alikuwa wakala wa CIA nchini Kongo tangu mwaka 1961ambapo Shirika hilo lilimgharamia mafunzo ya uandishi wa habari kumwezesha kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, na alibakia hivyo hata baada ya mapinduzi ya 1965.
Mwanzoni, wananchi wa Congo waliweka matumaini yao kwa Mobutu; amani na utulivu vikarejea, uchumi ukaanza kuimarika ukipewa nguvu na utajiri wa madini – shaba, chuma, kobalti na Almasi. Mobutu akaanzisha sera ya uwekezaji kwa masharti yaliyolegezwa kuvutia wenye mitaji kutoka nje kama tunavyofanya hapa kwetu, na akapongezwa na Rais Richard Nixon wa Marekani mwaka 1970kwa hilo.
Kufikia mwaka 1974, Congo ilikuwa kivutio kwa wenye mitaji kutoka Marekani na Ulaya hivi kwamba pambano la dunia la Wanamasumbwi wawili Wamarekani wenye asili ya Kiafrika, Muhamed Ali (zamani Cassius Clay) na George Foreman, likafanyikia Congo na kupewa jina “Rumble Jungle”.
Na kadri utamu wa madaraka na matarajio ya kisiasa yalivyozidi kuongezeka huku “wawekezaji” wakipasua anga la Congo na mithili ya askari wa miavuli, ndivyo Mobutu alivyozidi kujiona kuwa yeye ndiye alikuwa Congo na Congo ilikuwa ndiyo yeye. Akapiga marufuku vyama vya siasa vya upinzani na kubakiza chake cha “The Movement Populaire de Revolution” (MPR) kikiongozwa na itikadi ya “Authenticity”, yaani “Uasilia” au “Mobutuism” – Umobutu.
Kwa itikadi hiyo, aliagiza kubadilishwa kwa majina ya kigeni, ambapo Congo iliitwa Zaire; Mji Mkuu Leopoldville ukaitwa Kinshasa; Stanleyville ukapewa jina Kisangani na Jimbo la Katanga likaitwa Shaba.
Akapiga marufuku majina ya watu ya kigeni; kwamba kasisi aliyebambwa akibatiza watotowa Kizaire kwa majina hayo, adhabu yake ilikuwa kifungo cha miaka mitano jela.
Na kwa kuanzia, yeye akabadili jina lake la Joseph Desire Mobutu na kuitwa Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu Wa Zabanga, maana yake, shujaa wa vita asiyeshikika na asiyejua kushindwa; jogoo lisiloweza kumwacha kuku jike salama.
Alipiga marufuku pia suti za Kiulaya, badala yake akaagiza Wazaire wavae vazi la mtindo wa Mao Tse Tung, maarufu kama “abacost”; kisha akaagiza atambuliwe kama “Baba wa Taifa, Mpiganaji, Mwanamikakati Mkuu na Mkombozi wa watu”. Vipindi vya televisheni vilitanguliwa na kifungua pazia cha picha yake akishuka kutoka mawinguni kama “Masiya”.
Akiwa tayari amelewa madaraka, Mobutu alianza kujimilikisha utajiri wa nchi na kuhodhi madaraka; alidhibiti na kusimamia ajira na mgawo wa mapato ya taifa yeye mwenyewe. Na katika kile alichoita kuipa Zaire uhuru wa kiuchumi, mwaka 1973 aliagiza kunyakuliwa kwa kampuni 2,000 za kigeni, mashamba, ranchi, viwanda na maduka makubwa bila kutoa fidia kwa wenyewe; kisha mali hizo zikakabidhiwa wanafamilia wake na nduguze, ambapo mashamba makubwa kumi na manne akajimilikisha na kuyaundia Kampuni iliyoitwa “Cultures et Elevages du Zaire”, kwa kifupi “Celzas”, iliyozalisha asilimia 25 ya Kakao na zao la mpiranchini na kuajiri watumishi 25,000, wakiwamo wa kigeni 140 kufanya kuwa mwajiri mkubwa wa tatu Zaire.
Kufikia mwaka 1976, theluthi moja ya mapato ya Taifa yalikuwa mali ya Mobutu, akimiliki pia hisa katika Benki ya “Banque du Kinshasa” ambamo mashirika yote ya umma yalitakiwa kuweka pesa zake. Alimiliki pia mashirika makubwa mawili ya madini ya Sshaba na migodi – “Gecamines na Sozacom” mbali na kujihusisha na biashara ya Almasi ya Zaire kwa ubia na rafiki yake kipenzi, Maurice Tempelsman.
Kila mwaka, Mobutu alipora na kuhamishia nje mabilioni ya fedha. Kwa mfano, kwa mkupuo mmoja tu mwaka 1976, moja ya mashamba aliyojimilikisha lilihamishia kwenye Benki ya Uswisi zaidi ya dola za Kimarekani milioni moja; na mwaka 1977, kampuni zake 50 zilihamishia nje ya nchi zaidi ya dola milioni 300.
Mwaka 1981, aliagiza Benki Kuu kuhamishia kwenye akaunti yake ya nje dola milioni 30, na kipindi hicho hicho aliuza kwa manufaa binafsi, tani 20,000 za shaba zenye thamani ya dola milioni 35, mbali na kolbati na almasi alizosafirisha Ulaya kwa kutumia ndege yake binafsi.
Kufikia mwaka 1979, Mobutu alikuwa mmoja wa watu matajiri kupindukia duniani, mwenye mali zilizozidi thamani ya dola bilioni tano; akimiliki pia majumba Ufaransa, Uswisi, Spain, Italia, Corte d’Voire, Senegal, Morocco na Brazil.
Makazi yake ya Kinshasa lilikuwa jumba lenye thamani ya zaidi ya dola 120m; na makazi mengine yalikuwa katikati ya msitu mzito mahali paitwapo Gbadolite, maili 700 kaskazini mashariki mwa Kinshasa, yenye mazingira ya nakshi za kila aina na uwanja wa ndege mkubwa kuwezesha kutua ndege kubwa aina ya “Supersonic Concordes” alizotumia kwa safari za nje.
Wakati akiendelea kujilimbikizia mali, viongozi wenzake nao walifuata mkumbo, kila mmoja akipora kwa urefu wa kamba yake; fedha za bajeti ya serikali hazikutolewa tena, waalimu na watumishi hospitalini wakakosa mishahara kwa muda mrefu, huku asilimia 40 ya bajeti hiyo ikipotea au kutumika kwa madhumuni yasiyokusudiwa, huku asilimia 60 ya bajeti ya mishahara ikilipwa kwa watumishi hewa.
Wanajeshi waliuza chakula cha jeshi; wale wa Jeshi la Anga wakageuza ndege kwa usafiri wa kiraia kibiashara kwa manufaa yao kwa nusu nauli ya Shirika la Ndege la Taifa, huku watumishi wa hospitali nao wakiuza dawa na vitendea kazi na kupelekea hospitali kufungwa kwa kukosa dawa. Ubadhirifu huu na kutowajibika vilipokithiri katikati ya baa la njaa, uchumi ukaporomoka, huku bei ya mafuta ikipaa na mapato ya nchi kushuka; biashara ya mashirika ya Mobutu aliyojimilikisha nayo ikatifuka.
Kwa mwaka 1977 pekee, riba kwa madeni ya nje ilitafuna zaidi ya asilimia 50 ya mapato ya serikali. Juhudi za Benki za Ki-Magharibi kujaribu kuokoa hali kwa njia ya mikopo zaidi hazikufua dafu. Alibembeleza wawekezaji wa kigeni aliowapora vitega uchumi vyao warejee kuwekeza, lakini wakagoma.
Kwa kujifanya kwamba alichukizwa na ufisadi, wizi na rushwa; Mobutu aliitisha kikao cha Baraza la Mawaziri na Wakuu wa MPRkutoa onyo, akasema: “…..kama utaiba, usiibe kingi kwa mara moja, unaweza ukakamatwa; (akasema: “yibannamayele”) – iba kwa ujanja na kwa maarifa, kidogo kidogo”.
Kufikia hapo, tayari Zaire ilikuwa kwenye mtafaruku: uchumi kuporomoka, jeshi kupoteza nidhamu na kupora raia ovyo, uwajibikaji duni wa Serikali huku njaa ikitafuna nchi na kukaribisha machafuko ya kisiasa; mapigano ya kivikundi vya kikabila kugombea madaraka na utajiri yakazuka.
Wakati huo, Zaire ilikuwa kimbilio mafichoni na makazi (hasa eneo la Kivu) ya vikundi vya kiharakati vilivyofanya mashambulizi kutaka kuangusha serikali za marais Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda, ambao nao kwa kutumia udhaifu wa Mobutu, walituma vikundi vyao kupora madini na rasilimali zingine kutoka Zaire kutajirisha nchi zao.
Mwaka 1981, kwa kuchukizwa na tabia ya Kagame na Museveni, Mobutu alifuta sheria iliyoruhusu uraia kwa “Banyarwanda” na kufungua manyanyaso kwao, hatua iliyomkasirisha Kagame nakudhamiria kuvamia Zaire akiungwa mkono na Museveni. Kutekeleza hilo, alihitaji kutumia sura ya Mzaire; na mtu waliyemteua kuongoza uvamizi huo alikuwa Laurent Desire Kabila, kiongozi wa zamani wa vita vya msituni dhidi ya Serikali ya Mobutu, aliyegeuka mfanyabiashara ya magendo ya dhahabu, pembe za ndovu na ngozi za chui kati ya Dar es Salaam na Kampala.
Kwa hiyo mwaka 1996, Kagame akaendesha mafunzo ya kijeshi kwa wakimbizi wa kabila la Banyamlenge na Watusi kutoka Kivu; akaandaa pia vikosi vya Jeshi la “Rwandan Patriotic Army” (RPA) kwa ajili ya uvamizi huo.
Siku hiyo ikawadia, Oktoba 8, 1996. Ilikuwa hivi: vikosi vya Banyamulenge vilipambana na Jeshi la Mobutu Mkoa wa Kivu Kusini. Kutokana na uchokozi huo, Naibu Gavana wa Jimbo hilo, Lwasi Ngabo Lwabanji, aliamuru wa-Banyamulenge wote kuondoka Zaire kwa hiari ndani ya wiki moja, vinginevyo wangeuawa au kufukuzwa kwa nguvu.
Jibu la Kagame likatoka hima, akasema: “Tuko tayari kuwanyuka vibaya na ipasavyo; kisha tutafanya mambo matatu muhimu”; kwanza, kuwaokoa Wanyamulenge na si kuwaachia waendelee kuuawa; pili, kuwawezesha wapigane, na ikibidi kuwapigania; kuyavunja makambi na kuwarudisha Rwanda na kuwaangamiza wanamgambo; na tatu, kuibadili kabisa hali ya kisiasa nchini Zaire”.
Wakati Kagame akitangaza hayo, Jenerali Mobutu alikuwa akitumbua alivyopora katika Ikulu ndogo ya Gbadolite katikati ya msitu mnene wa ki-Ikweta, bila kuelewa yaliyokuwa yakitokea Kivu.
Inakadiriwa, kwa mwaka mmoja pekee, familia ya Mobutu ilifungua zaidi ya chupa 10,000 za Shampeini (champagne) kwa sherehe lukuki; na aliposafiri nje, alikodi ndege kubwa aina ya “Concorde” iliyosubiri daima kwenye uwanja wa Gbadolite.
Hata hivyo, Mobutu alikuwa mdhoofu kwa ugonjwa. Agosti 1996, madaktari wake waligundua alikuwa akisumbuliwa na kansa ya kibofu; akatumia muda mwingi kwa matibabu huko Ufaransa na Uswisi, huku ghasia zikizidi kupamba moto huko Kivu.
Kwa msaada wa Jeshi la Kagame la RPF, lakini kwa kisingizio cha maasi ya Wanyamulenge, mapigano yalienea kutoka Kivu ya kusini hadi kaskazini kwa kasi kubwa kwamba Oktoba 24, 1996 mji wa Uvira ukatekwa na waasi; siku sita baadaye, Oktoba 30, 1996, mji wa Bukavu nao ukasalimu amrikabla ya mji wa Goma kufanya hivyo hapo Novemba mosi, 1996.
Ndipo Laurenti Kabila alipojitokeza kwa mara ya kwanza, akajitangaza kama kiongozi wa “Liberation Movement” na Mkuu wa Jeshi jipya la Muungano la Ukombozi wa Kongo/Zaire – “Alliance des Forces Democratique de Liberation du Congo – Zaire [AFDL]; akazungumza na vyombo vya habari kwenye Makao ya Mobutu mjini Goma, akasema, “Lengo ni kukamata Kinshasa”.
Jenerali Mobutu alirejea Zaire Desemba 1996 kutoka nje alikokwenda kwa matibabu. Huku akionekana kudhoofu dhahiri, alijaribu kujiweka sawa kujibu mapigo ya RPA. Alijihimu kusafiri umbali wa maili 20 kutoka uwanja wa ndege wa Kinshasa hadi Makao Makuu ya Divisheni Maalum ya Jeshi lake, TSha Tshi (Division Speciale Presidentielle –DSP); na kwa shida sana, aliweza kusimama wima kwenye gari lake la wazi la kifahari kuwapungia mkono wananchi. Mobutu, kwa msaada wa Ufaransa, aliajiri askari mamluki 300 wa Kisebia kutoka uwanja wa mauaji huko Bosnia lakini bila mafanikio kuweza kupunguza kasi ya RPA na Wanyamulenge (AFDL chini ya Kabila), huku Jimbo baada ya Jimbo likisalimu amri na kuungana na wapiganaji hao.
Kufikia hapo, uwanja wa mapambano ulihusisha si Rwanda na Uganda pekee, bali Angola pia dhidi ya Mobutu, kutokana na nchi hiyo kuchukizwa na Mobutu kumuunga mkono muasi Jonas Savimbi na Jeshi lake la UNITA dhidi ya Serikali halali ya Angola.
Machi 1997, mji wa Kisangani nao ulitekwa na waasi wa AFDL; na kufumba na kufumbua, Aprili 1997, miji ya Mbuji Mayi na Lubumbashi nayo ikaangukia mikononi mwa wapiganaji wa Kabila.Huku Jeshi la Mobutu (FAZ), lenye majenerali 50 na makanali 600, likijaribu kujihami kurejea Kinshasa, ni wapiganaji wa UNITA na vikosi vya Interahamwe vya Kinyarwanda (wahasimu wa Kagame) pekee ndio walioendelea kupigana.
Katika hali iliyoonesha kuasi kwa Jeshi lake, Mobutu na familia yake walinusa harufu ya kifo; haraka haraka wakakimbilia kwenye ndege ya mizigo aina ya “llyushin” iliyomilikiwa na Jonas Savimbi (wa UNITA) na kutoroka nchi, huku risasi za wapiganaji wa AFDL zikirindima, nusura zipige kiunzi cha ndege (fuselage) hiyo wakati ikiondoka kasi.
Saa chacha baadaye, Jeshi la Laurent Kabila (AFDL) liliuzingira mji wa Kinshasa, kisha likaingia kwa madaha kama wafalme katikati ya nderemo, vifijo na vigelegele vya wakazi wake, miezi minane tangu maasi yalipolipuka kwa mara ya kwanza huko Kivu Kusini.
Mei 17, 1997, Laurent Desire Kabila aliapishwa kama Rais wa pili wa kiraia wa Kongo/Zaire tangu Joseph Kasavubu. Na katika hali ya kuchukizwa na mengi yaliyofanywa na Serikali ya Mobutu kwa nchi ambayo kabla ya Mobutu ilijulikana kama Congo Brazaville, Kabila alifuta jina la Zaire, ikaitwa “Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo” (DRC). Miezi minne baadaye, Mobutu alifariki uhamishoni nchini Morocco.
Kwa Mobutu, tunajifunza nini kuhusu uongozi na maendeleo ya nchi? Ni kwamba, tamaa ya mali (ufisadi) huzaa maovu na udikteta, mambo ambayo ni sumu ya uongozi. Mambo haya hukua gizani, hujilisha kwa damu ya jamii isiyo na hatia; na inapotaka kujitanua kuwaangamiza wengi wasio na hatia, hujiangamiza yenyewe.
Na kuhusu ufisadi tunaweza kusema mengi; lakini itoshe tu kwamba, umasikini wa mtu husababishwa na utajiri haramuwa mwingine. Hadi hapo utajiri wa huyo mmoja (au kikundi cha watu) utakapokatishwa kwa kifo kwa kuuawa (ghadhabu ya umma) au kwa nguvu ya kisheria kuwatetea masikini (ujamaa); umasikini, taabu na mateso yataendelea kuwaandama walio wengi katika ujumla wao. Nasi hapa kwetu, kwa sera hizi za ubinafsishaji na uwekezaji usiojali tulipofikia, rushwa na ufisadi; tutarajie kipi kutoka Serikali ya Awamu ya Tano kuepusha shari?.
Chanzo: Raia mwema
No comments:
Post a Comment