Raia Mwema: Umeingia kuongoza Bunge katika wakati ambao linakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo ukosefu wa nidhamu bungeni kama ilivyoshuhudiwa kwenye Bunge la 10. Unalitazamaje hilo, na nini utafanya kurejesha nidhamu ya Bunge.
Dk. Tulia: Unajua kwa Bunge hili la 11, huu ndio mkutano wa kwanza. Kwa kuzingatia kwamba wabunge wengi ni wapya, wengi hawajajua taratibu za Bunge na namna shughuli zinavyofanywa, ni rahisi sana akiambiwa afanye chochote anafanya.
Lakini ni imani yangu kwamba tutakapofanya semina za kuwaelekeza namna ya shughuli za Bunge zinavyoendeshwa, taratibu zilivyo, kanuni za nani anaongea saa ngapi muda gani, likifanywa jambo gani ufanye nini? Tukiwaelekeza hayo ninaamini watatumia utashi wao kuamua cha kufanya.
Lakini umeeleza kwamba mambo haya yalipata kutokea katika Bunge la 10 pia na kwamba watu walikuwa wakilalamika, kwa sababu vikao vinaonyeshwa moja kwa moja na wananchi wanapata fursa ya kujua nini kinaendelea. Sababu moja inaweza kuwa ni hulka ya mtu. Yaani ni wa aina hiyo hiyo.
Lakini nyingine inakuwa si hulka, kwa sababu wabunge wanapoingia bungeni wanatumia tiketi za vyama. Kwa hiyo, chama kikitoa msimamo fulani, ni lazima wabunge wa chama hicho wote wafuate. Kwa sababu asipofuata, inamaanisha kwamba anaweza kufukuzwa uanachama. Ukifukuzwa uanachama ubunge pia unakuwa huna. Hilo ni tatizo pamoja na kwamba watu wanapotoka bungeni na wanapofanya vurugu, wanafanya kama kundi, lakini wengine wanafanya kwa kutokufahamu taratibu zinatakaje.
Kwa sababu wewe unajua kwamba Katiba inaeleza nani anaweza kuwa Mbunge, yeyote anaweza kuwa mbunge ili mradi anajua kusoma na kuandika. Sasa si kila mtu anaweza kuwa amesoma hizi kanuni za kuendesha Bunge na akajua katika mazingira haya nifanyeje, huyu ni yule atakayetumia utashi wake, na mimi naamini tukifanya utaratibu wa kuwaeleza kwamba mabunge yanaendeshwa vipi wapo watakaotumia utashi wao, na kuna wale ambao ni hulka yao na kwa sababu taratibu zipo mimi nitajaribu kuwaeleza, kanuni zinasemaje naamini watasikiliza kama hawakusikiliza sasa ndiyo inakuja ile hoja kwamba kanuni hizihizi zinataka uchukue hatua fulani kama mtu hataki kusikiliza maelekezo. Kwa sababu usipochukua hatua hakuna jambo linaweza kufanyika.
Sasa kama hili lililotokea (Ijumaa iliyopita wakati Rais Dk. John Magufuli alipokwenda kuzindua Bunge) kimsingi zile nyimbo zisingekwisha.
Unatarajia, katika hali ya kibinadamu, mtu anaweza kuchoka kuimba, lakini anaweza asichoke, kwa sababu anaweza kuwa ana nguvu za ziada au anaweza kuwa amejipanga kufanya hivyo. Kusipokuwa na kanuni za kuleta utulivu inakuwa ni shida.
Maana yake Rais asingeweza kuhutubia na wananchi wangekosa fursa ya kujua vipaumbele vyake alivyokusudia kuvitoa. Kwa hiyo, kanuni zinaruhusu ikitokea hali kama hiyo unawaondoa wabunge wanaoanzisha vurugu. Wapishe wengine wasikilize na kwa hilo Ijumaa wananchi walipata fursa ya kumsikia Rais wao.
Lakini pia wabunge waliobaki walipata fursa ya kusikia vipaumbele vya rais ili waweze kuvifanyia kazi.
Raia Mwema: Ikitokea wamekaidi. Hawataki kutoka pia?
Dk. Tulia: Taratibu zipo. Kanuni pia zipo. Ukisema watoke nje wakakaidi kutoka, kuna kutumia nguvu. Sasa ile kutumia nguvu haimaanishi kwamba watu wanaanza kupigwa. kinachomaanishwa ni kwamba mtu akikaidi amri halali atatolewa nje, kwa hiyo, badala ya yeye kuwa amesimama pale amekaidi kutoka, atasindikizwa nje, na watu wenye kufanya hilo wapo.
Kanuni zinaposema kutumia nguvu hazimaanishi kutumia nguvu kwamba watapigwa, lakini atasindikizwa pale anapotakiwa kwenda.
Raia Mwema: Wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walilalamika kwamba mmeingiza askari wenye sare bungeni na kwamba hicho ni kinyume cha taratibu na kanuni zinazoongoza Bunge, hiyo ndiyo tafsiri ya matumizi ya nguvu? Na unasemaje kuhusu malalamiko hayo?
Dk. Tulia: Wale wapambe wa Bunge ni askari. Wanaruhusiwa kuingia. Si kwa majina yao. Wanaruhusiwa kwa sababu ni askari, na kazi yao mojawapo ni kulinda usalama wa maeneo ya Bunge, wabunge wenyewe na vitu kama hivyo.
Askari, wawe wa Field Force Unit (FFU) ama Jeshi la Wananchi ama Polisi, niseme vyombo vinavyoitwa vya ulinzi, wanaruhusiwa kuingia bungeni. Hoja si kwamba waliingia na uniform (sare) au kitu gani, la msingi ni kwamba wao wanaruhusiwa kuingia bungeni. Hali ilivyokuwa ndiyo ilisababisha waingie kwa ile idadi ambayo watu wanasema waliingia wengi.
Kwa sababu watu ambao ni zaidi ya 100 hawawezi kutolewa na askari watatu. Na wao lazima wawe wengi ili waweze kuwatoa pale ambapo watakaidi.
Raia Mwema: Umezungumza habari za siasa za vyama bungeni, matarajio ya wananchi ni kwamba wakiwa bungeni wabunge wanatarajiwa kujadili masuala kwa maslahi ya Taifa, si vyama vyao, Rais pia alisisitiza kuondoa u- vyama bungeni. Tunawezaje kulifanya Bunge liwe la kitaifa badala ya kivyama kama ambavyo tunashuhudia sasa?
Dk. Tulia: Kimsingi ni wananchi, ukiondoa nafasi za kuteuliwa ambazo zinategemea utashi wa huyo anayekuteua na ushauri aliopewa, Wabunge wengi ni wabunge wa kuchaguliwa na wananchi. Kwa hiyo, wananchi wanayaona mambo haya. Wanaona viongozi wao wanavyofanya.
Kama wananchi wanaona hayo ni sawa ataendelea kuwa kiongozi kwa sababu huna namna ya kumzuia. Kila mtu akitimiza yale masharti ya jumla anayo haki ya kugombea, wananchi wakiona kwamba huyu huwa hafanyi tuliyomtuma bungeni, watamchagua mwingine, yeye hawatamchagua.
Lakini kama akijitokeza na wananchi wakamchagua, maana yake ni kwamba wananchi waliomchagua wanakubaliana na hayo aliyofanya. Kwa sababu hakuna maelezo mengine ninayoweza kutoa kuhusu mtu anayefanya vurugu na bado anachaguliwa.
Kwa ujumla sisi viongozi tunatarajia kuwa mtu aliyechaguliwa atakuja bungeni kufanya yale ambayo wananchi wake wana tabu nayo. Kama wananchi wake hawana shida anaweza kutoka wakati Rais anahutubia.
Lakini yale maangizo aliyotoa Rais kwa watendaji, kwa mfano, ni kazi ya Bunge kufuatilia. Kwa sababu, maagizo ya Rais anaiagiza serikali, na kazi ya Bunge ni kufuatilia na kusimamia serikali. Kwa hiyo Bunge litakuwa linauliza kwenye afya aliagiza mambo haya, serikali imefanya nini?
Sasa wewe ambaye hukupata fursa ya kusikiliza na kijijini kwa wananchi wako hakuna zahanati, lakini Rais amezungumzia mipango ya zahanati, sasa wewe hilo utalifuatilia vipi?
Hapo ndipo linapokuja tatizo. Naamini wananchi wanaelewa, wanao utashi mkubwa na wanapomtuma mtu huku wanatarajia atafanya kazi ya kutatua changamoto zao, ikiwa ni kuifuatilia serikali.
Kwa sababu wabunge si wao wanafanya, ni serikali ndiyo inafanya (shughuli na miradi ya maendeleo), wabunge wote, awe wa Upinzani au chama tawala (CCM), kazi yao ni kufuatilia zile ahadi zinazohusu jimbo lake ili zitimizwe, na anayetimiza ni serikali, mbunge anatarajiwa kufuatilia ili serikali itimize wajibu wake.
Raia Mwema: Liko suala la Kiti cha Spika kutenda haki. Baadhi ya wabunge wa Upinzani wamekuwa na malalamiko ya kutotendewa haki na Kiti. Ulikuwa ukifuatilia Bunge kabla na sasa wewe ni kiongozi wa Mhimili huu, unadhani upendeleo huo upo? Kama ndiyo kuna namna gani ya kuonyesha haki inatendeka na ionekane imetendeka?
Dk. Tulia: Kama ulivyosema, pamoja na kwamba sikuwa mbunge au kiongozi wa Bunge, nilikuwa nalifuatilia. Kimsingi Bunge linandeshwa na Katiba, sheria zilizopo na kanuni.
Kanuni, kwa mfano, inasema Spika akisimama Wabunge wote wanapaswa kukaa. Mbunge yeyote, hata kama alikuwa anatoa hoja, akisimama Spika, Mbunge anapaswa kukaa.
Sasa Spika amesimama, nawe Mbunge unaamua na wewe kusimama, maana yake unakwenda kinyume cha kanuni. Akikuambia ukae, ukikaidi, maana yake hawezi kuendelea na shughuli zake.
Hawezi kuendelea kuzungumza wakati wewe umesimama. Kwa hiyo inabidi akutoe nje, wewe utaona kwamba umeonewa lakini kanuni ndivyo inavyosema. Mkisimama wote wawili akikuacha, atakuwa ameshindwa kuonyesha uongozi ili kikao kiendelee.
Lakini kwamba Kiti kinachukua upande, nadhani hata wewe huwa unafuatilia. Sijapata kuona mahali ambapo Kiti kimechukua upande. Sababu ni hii. Kuchukua upande inategemea wewe umesimamia upande upi. Kama unataka kuangalia sheria inasemaje hutaona kimechukua upande. Kwa sababu hakuna mtu anafukuzwa bungeni bila sababu.
Kiti hakisemi tu we pale mwenye shati ya bluu toka nje. Lazima uwe umefanya jambo linalostahili kutolewa nje, lakini ukifuata maelekezo ziko nyakati hata wanaolalamika mambo yanaenda vizuri. Iko mijadala inaenda vizuri tu, watu wanatoa hoja zinajibiwa na mambo yanaenda vizuri.
Lakini pale kanuni zisipofuatwa Kiti lazima kionyeshe uongozi ili mambo yaende vizuri. Tusipofanya hivyo Bunge litashindwa kufanya kazi yake.
Raia Mwema: Rais Magufuli ana ari kubwa ya kutaka kukabili kero za Watanzania, unadhani Bunge hili liko tayari kumsaidia kutimiza azma hiyo?
Dk. Tulia: Mimi nadhani litamsaidia. Kwa sababu wabunge hawa, wengi ni wapya na kuna wakongwe wengi hawajarudi. Matarajio hayo ya wananchi si tu kwa serikali lakini pia ni kwa wawakilishi wao waliowatuma. Wanajua kabisa kwamba kumfikia Rais wamueleze matatizo yao ni ngumu, lakini wanatumia mwakilishi wao ayafikishe. Mwakilishi amesikia mwelekeo wa serikali kuhusu afya, elimu, na kuhusu mambo yote, mbunge huyu huyu atasimama asubiri kwenye afya bajeti inasemaje, inanifikia au hainifikii.
Kwa hiyo, ninaamini usimamizi wa shughuli za serikali utakuwa ni mkubwa safari hii. Rais ameeleza mambo mengi. Bunge kazi yake ni kusimamia, je, serikali imefanya?
Kwa sababu wamemsikia aliyoahidi kwa wabunge, naamini wabunge wamemsikia Rais na aliyoyasema watayatekeleza kwa maana ya kwamba wataisimamia serikali ili ifanye aliyoahidi. Kwa hiyo ninaamini Bunge hili litajiweka vizuri kwa ajili ya zile ahadi alizoahidi.
Raia Mwema: Rais ameonyesha matumizi yasiyo ya maana kwa maslahi ya Taifa na wananchi. Bunge ni taasisi aliyoitaja kuongoza kwa matumizi ya aina hiyo, utalisaidiaje Bunge lisiingie tena katika matumizi ya aina hiyo?
Dk. Tulia: Rais amelieleza jambo hilo vizuri sana. Kuna zile safari za kujifunza na kuna safari za matibabu. Tukishaisimamia serikali, tukaboresha afya, safari za kumpeleka mbunge kwenda kutibiwa nje maana yake hazitakuwapo. Kwa hiyo, matumizi yatapungua. Safari za kwenda kujifunza nje, Rais si kwamba kazikataza. Amesema watu watajifunza ndani na nje, cha kuangalia ni huyu kile anachoenda kujifunza hawezi kujifunza hapa? Kile ambacho hakiwezekani kujifunza hapa wabunge bado wataendelea kwenda, kile kinachowezekana kujifunza hapa basi wataalamu wataletwa.
Niseme kwa ujumla kwamba Rais ametoa mwelekeo wa matumizi ya fedha. Na matumizi ya fedha sasa hivi yako kisheria. Huwezi kufanya matumizi nje ya bajeti. Kwa hiyo mambo yote ambayo ulikuwa umeyabajeti ndivyo utakavyofanya matumizi.
Ni imani yangu kwamba bajeti ya mwaka ujao wa fedha itatoa huo mwelekeo wa namna ya kuondoa matumizi yasiyostahili. Nimetoa mfano katika maeneo ya afya na mafunzo, kama tutaweza kuleta mtaalamu hapa kwa mambo ambayo hatuna utaalamu basi ataletwa. Ametushauri vizuri sana na sisi tutakaa haya mambo tutayaangalia tutayaweka vipi.
Lakini kwa yale ambayo wabunge wetu waende kujifunza huko uzoefu basi tutawapeleka. Maana hatutaweza kuubeba ule uzoefu kuuleta hapa. Lakini kimsingi ni kwamba wazo kubwa katika haya yote ni kupunguza matumizi ili fedha zielekezwe maeneo ya maendeleo, lakini pia tukumbuke maendeleo yanakuja kwa wale watendaji kujua cha kufanya.
Mwanzoni nilisema wabunge wengi ni wageni, ili uende kujifunza mabunge mengine yanafanyaje, ili uweze kujua hayo ni lazima uone wanajadili vipi, sasa huwezi kuleta wabunge wale huku ili wakuelekeze, kwa hiyo inabidi tu uende ukaone wao wanajadili vipi. Katika mazingira hayo safari zitakuwa ni za lazima lakini pale ambapo ni kujifunza kwamba kanuni hizi zinasemaje, huhitaji mtu kutoka nje kukuelekeza, hizi tutajifunzia hapa hapa.
Raia Mwema: Kumekuwa na mazoea ya kutunga sheria na baada ya muda mfupi zinarejeshwa tena bungeni kufanyiwa marekebisho. Utalisaidiaje Bunge kutunga sheria ambazo zinaishi muda mrefu bila kulazimika kubadilishwa mara kwa mara?
Dk. Tulia: Kimsingi marekebisho ya sheria yanatokea siku zote na sababu zake zipo, moja inaweza kuwa ni hiyo, kwamba wakati wa kutunga kuna jambo hawakuliona vizuri au waliliona kwa namna tofauti lakini baadaye utekelezaji wa sheria umeleta shida. Jingine ni sheria kubadilishwa kutokana na mazingira. Pengine mazingira yamebadilika, lazima sheria iendane na mabadiliko hayo, jambo ambalo halikuwa kosa mwaka jana mwaka huu unaweza kulifanya kuwa kosa kwa sababu ya mazingira yaliyotokea.
Kwa mfano, kuna mambo mengi yanasemwa kuhusu ile Sheria ya Makosa ya Mtandao. Kuna mambo ambayo unaweza kusema hapa kidogo utekelezaji wake ni shida, lakini yako mazuri mle, kwa hiyo huwezi kusema sheria yote ni mbaya.
Inapotokea katika utekelezaji kwamba hili jambo litiliwe mkazo, hili liondolewe kabisa kwa sababu wananchi wanaonewa, linaondolewa. Kwa hiyo mabadiliko ya sheria katika hii tasnia ya sheria huwa ni ya kawaida sana. Hata Katiba, ndiyo maana huwa inabadilishwa muda kwa muda, kutegemea jambo lenyewe mnataka kubadilisha kwa sababu gani.
Mfano mwingine ni huo aliosema Rais kuhusu Sheria ya Manunuzi. Wakati ikitengenezwa kulikuwa na sababu za msingi za kuifanya iwe hivyo ilivyo. Lakini katika utekelezaji wake inaonekana kuna vifungu vinaleta matatizo zaidi na kufanya matumizi ya fedha yawe makubwa zaidi kuliko kupunguza.
Mazingira kama hayo si kwamba Bunge lililopita lilikuwa halijaona mambo kama hayo. Ni kwamba wakati ikitengenezwa ilikuwa sawa sawa lakini wakati wa utekelezaji inaonaekana ni lazima mambo kadhaa yabadilishwe.
Raia Mwema: Katika kutimiza vipaumbele vya Rais kunaweza kutokea usaliti, unadhani Bunge litamsaidia vipi hali hiyo ikianza kutokea?
Dk. Tulia: Rais ameahidi kupasua majipu, Bunge litamsaidia kwa maana ya kushirikiana naye na kama alivyosema, ametaja sheria chache, lakini ziko sheria nyingi zitakazopaswa kubadilishwa ama nyingine kutungwa ili kuweza kuyafanya yale yote aliyoyasema, si yote kwamba sheria ipo na itaunga mkono namna yeye anavyotaka kwenda.
Kwa hiyo sisi tutamuunga mkono kwa kuweka mazingira ambayo serikali inaweza kuyafanyia kazi kwa sababu serikali haiwezi kufanya jambo ambalo halijatungiwa sheria na Bunge. Lakini pia tutamsaidia kwa maana ya kwamba vile vyombo alivyosema ataanzisha, kwa mfano ametaja Mahakama ya Mafisadi, kwa hiyo mswada wa sheria inabidi uje, sisi tutamsadia kuitengeneza hiyo sheria kuwa vizuri ili wale watu wakamatwe.
Umeuliza kuhusu usaliti mimi ningependa kuamini kwamba watu wataangalia mwelekeo wa Rais ni upi, kwa hiyo ule usaliti wao lazima tu utadhibitiwa. Naamini watamwelewa Rais na watafanya yale ambayo ameagiza. Kama mtu anajishughulisha na dawa za kulevya ataacha kwa sababu Rais yuko serious, kama mtu anafanya ufisadi ataacha, kwa sababu katika hali ya kawaida hutegemei kwamba Mkuu wa nchi anatoa maagizo halafu hayo maagizo hayatafuatwa.
Lakini kama mtu atakwenda kinyume basi adhabu ya msaliti itajulikana. Sheria ipo. Watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria, watapelekwa mahakamani, wengine watafungwa, sidhani kama kuna mtu atakuwa amejipanga mahali anasubiri yeye afungwe.
Raia Mwema: Imezoeleka kwamba viongozi wa Bunge wanatoka katika majimbo ya uchaguzi, wewe umetoka nje ya eneo hilo, unafikiri ni sifa gani imekufikisha hapo?
Dk. Tulia: Wakati nikigombea hii nafasi, niligombea pia nafasi ya Uspika, na Katiba inasema mtu yeyote mwenye sifa za kuwa mbunge anaweza kugombea Uspika na ndicho nilichokuwa nimegombea. Kwa sababu niliona sifa ninazo.
Lakini katika kinyang’anyiro hicho nikapata bahati ya kuteuliwa kuwa mbunge, tofauti na nafasi ya Spika, nafasi ya Naibu Spika inataka mtu awe mbunge.
Nilivyokosa nafasi ya Spika nikagombea Unaibu Spika kwa sababu nimepata ubunge, kimsingi Katiba haisemi ni mbunge wa aina gani na ndiyo maana watu wengi wanapata tabu wanapoona wanafanya fujo bungeni.
Kwa sababu mnapokuja bungeni vyama vinapaswa kubaki nje ya uzio. Mkija hapa mnakuwa chombo kimoja cha kuisimamia serikali iliyoko madarakani, serikali ya chama chochote. Ukiweka tofauti ya vyama bungeni maana yake chama kinachotawala kiitetee tu serikali wakati haitakiwi kuwa hivyo.
Mbunge, hata wa chama tawala, pale ambapo serikali haifanyi sawa sawa lazima aisimamie.
Ukishaweka huo ufa huyu mbunge wa chama tawala atetee kila kitu kwa sababu ile ni serikali yake na wewe chochote serikali inacholeta lazima upinge kwa sababu wewe ni mpinzani, mambo hayaendi.
Mnaokuja bungeni wote mna sifa sawa. Mbunge wa Jimbo, Viti Maalumu, wa Kuteuliwa, wote ni wabunge na mna sifa moja basi, na sifa hiyo ndiyo iliyonifanya mimi kupata nafasi ya Naibu Spika.
Mnaokuja bungeni wote mna sifa sawa. Mbunge wa Jimbo, Viti Maalumu, wa Kuteuliwa, wote ni wabunge na mna sifa moja basi, na sifa hiyo ndiyo iliyonifanya mimi kupata nafasi ya Naibu Spika.
Raia Mwema: Katika kupata nafasi ya Naibu Spika ni kama umepita kwenye tanuru la moto na iko dhana, hata miongoni mwa baadhi ya wabunge wenzako, kwamba umebebwa kufika hapo ulipo. Kwa dhati ya nafsi yako, unasemaje kuhusu hilo?
Dk. Tulia: Unajua kila mtu anaruhusiwa kuwaza au kutoa mawazo yake. Mtu anayeweza kusema maneno kuwa mtu mwingine amebebwa mimi inanishangaza sana. Amebebwaje? Kwa sababu wote tunajua kubebwa maana yake nini.
Mtoto huwa anabebwa kwa sababu hawezi kutembea, ama anaumwa au amechoka. Wewe mwandishi unayeniuliza hilo swali, baada ya kunisikiliza na baada ya kuona sifa zangu wewe umeona ni eneo gani nitakuwa mimi nimebebwa?
Yaani ni eneo gani ambalo mimi sikuwa naliweza sasa nimewezeshwa nionekane nimebebwa? Nitakuwa nimebebwa kwa kushindwa kipi? Lakini hilo la kupita kwenye tanuru la moto kila chama kina utaratibu wa kupata viongozi wao, viko vyama ambavyo utaratibu wake ni mrefu kwa sababu ni chama kikubwa ni cha siku nyingi, kina mizizi tangu chini mpaka juu, kina taratibu zinazoeleweka. Hizo taratibu za vikao vyote lazima vipitiwe watu wachujwe waone nani anafaa kwenye nafasi hiyo.
Hiyo ni tofauti na vyama vingine ambavyo mtu leo anapewa kadi kesho anapewa ubunge. Leo amekwenda kwenye mkutano akaonwa huyu anaweza kufaa, anapewa. Wapo wabunge humu wamepata kwa namna hiyo.
Lakini kama unafuatilia, hata Viti Maalumu vya CCM ni mchakato mrefu mpaka mtu kufika hapo. Anagombea na kupigiwa kura kwenye mlolongo mrefu. Lakini huku kwingine mtu tu anakuja na majina yake mfukoni yanawekwa pale.
Kwa hiyo binafsi nisingependa kuendeleza hizo hoja kwa sababu najua mtu anyesema ni kwamba haelewi anachokisema. Hata akisema nimebebwa, labda aseme sina sifa, hapo ndiyo aniambie nimebebwa.
Anayesema atakuwa ameamua tu kwa sababu hajui au anajifurahisha. Ni kama sasa hivi kuna picha nyingi zinatumwa kwenye mtandao kwamba ni mimi, sijui labda kwa sababu hao watu ni weusi lakini si mimi. Watu wanakaa mapozi ya aina tofauti kwamba huyu ni nani alipokuwa anasoma wapi lakini its simply not me.
Sasa kwa kuwa wanaona mtu mweusi basi wakaona ni lazima ni mwenyewe lakini si mimi.
Raia Mwema: Dk. Tulia atakuwa Naibu Spika wa aina gani?
Dk. Tulia: Kazi ya Naibu Spika ni kumsaidia Spika kuliongoza Bunge katika vikao vyake na kutimiza wajibu wake kwa hivyo, huyu Tulia atakachofanya ni kusaidiana na Spika kuendesha Bunge kwa mujibu wa kanuni, sheria na Katiba ili kwanza kutimiza yale ambayo Bunge ni kazi yake.
Unajua yako mazingira ya Bunge kufikiri linaweza kuwa Mahakama na linaweza kuwa Serikali. Katiba imeweka mipaka ya mihimili ili kila mhimili ufanye kazi yake.
Kwa hiyo ile kazi ambayo kikatiba ni ya Bunge ndiyo hiyo nitalisaidia Bunge kufanya kazi nikimsaidia Spika. Kazi ambayo siyo ya Bunge nitakachofanya ni kuwakumbusha wabunge hilo tunalofanya tunaweza kujadili kama mtu mwingine anavyojadili lakini kama wabunge shughuli yetu kwenye hili ni hii kwa sababu Katiba inatutaka tufanye hili na siyo lile.
Ninaamini hili litakuwa Bunge la kufuata sheria kanuni na taratibu likiheshimu mihimili mingine ya Dola.
Raia Mwema: Hiyo ndiyo kusema Dk. Tulia atakuwa Naibu Spika mkali sana, wa wastani, mpole au wa namna gani hasa?
Dk. Tulia: Kusema ukweli nadhani yote hayo uliyoyataja yatakuwapo kulingana na mazingira yatakavyokuwa. Siwezi kusema nitakuwa mpole ikiwa mtu atakuwa amekaidi kufanya yale ambayo sheria inataka, lakini pia sitaweza kuwa mkali kama hakuna sababu ya kuwa mkali, sasa unamkalipia nani.
Niseme sisi wote ni binadamu ninachomuomba Mwenyezi Mungu ni kwamba anisaidie nisiwe na hasira wakati wa kufanya maamuzi, niweze kufanya haki kwa kila mbunge, kwa sababu siyo jambo jema mtu akifanya kosa unamwadhibu mwingine akafanya kosa hilo hilo unamwacha, hilo linaleta shida. Natamani niwe Naibu Spika atakayeweza kutenda haki kwa wabunge wote.
Raia Mwema: Umri wako wa miaka 39 na majukumu uliyonayo, mtu anajiuliza umevukaje vikwazo vyote vikiwemo vya unyanyasaji wa kijinsia, mpaka kufikia nafasi hiyo, vijana wanaweza kujifunza kitu gani kutoka kwako?
Naibu Spika: Kuna mambo mawili. La kwanza mimi naamini katika Mungu. Kwa sababu ya imani hiyo huwa naamini kwamba Mungu ameweka mwisho wa kila mwanadamu. Njia ya kufikia ule mwisho pia huwa anaitengeneza.
La pili ni ile njia anayoiendea huyu mwanadamu kufikia njia aliyowekewa na Mungu, ni bidii katika kazi. Si kwamba watu wengine ambao hawatapata fursa ya kufika nafasi hii kwamba hawafanyi bidii, si maelezo ninayotaka kutoa.
Ninachotaka kusema ni kwamba katika hali ya kawaida ninaweza kusema labda mimi nina bahati. Kwa sababu wapo watu wengi ambao wamefanya bidii sana katika mambo wanayoyafanya lakini hawajafika pale nilipo.
Mambo mawili haya nimeyaweka pamoja kwa sababu kule mwisho ili uweze kufika na ile njia unayopita inahitaji bidii, siyo kila mtu atakuwa amewekewa njia kama ya kwangu, kwa sababu Naibu Spika kwa miaka mitano atakuwepo mmoja tu, kwa hiyo hamuwezi kuwa wote mmewekewa hiyo njia kwa kipindi hicho.
Ukiwa na imani kwa Mungu katika hilo hilo unalolifanya ukifanya bidii utafika kule ulikopangiwa kwenda. Pengine si katika umri wangu lakini mimi naamini kwa bidii tu utafika.
Niseme kwa vijana na wengine ambao ninaweza kuwa inspire, cha kwanza wamuamini Mungu, lakini cha pili wafanye bidii katika chochote wanachofanya.
Raia Mwema: Uanachama wako kwa CCM umezua mjadala mkubwa, ni lini ulianza kuwa mwanachama wa chama hicho?
Dk. Tulia: Katiba inataja makundi matatu ambayo hayaruhusiwi kuwa kwenye vyama vya siasa. Unachoruhusiwa ni kitu kimoja tu, kushiriki kwenye uchaguzi kwa kupiga kura.
Kundi la kwanza ni majeshi yote, kundi la pili ni Mahakama, mahakimu na majaji wa ngazi zote hawaruhusiwi kuwa wanachama wa chama cha siasa. La tatu ni wafanyakazi wa Tume ya Uchaguzi.
Mimi kama Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Katiba haijanikataza. Kwa hiyo swali la kwamba nilijiunga lini na CCM halipo kwa kuwa Katiba hainikatazi. Lakini utasema ziko sheria za Utumishi wa Umma, sheria zile hakuna mahali zinanikataza mimi kuwa mwanachama wa chama chochote.
Kilichopo ni masharti ya mimi kushiriki siasa, wakati huo mimi kama mtumishi wa umma sipaswi kushiriki siasa (active participation) yaani kupanda majukwaani au kumnadi mgombea au kuzungumza mambo dhidi ya chama fulani, lakini sikatazwi kujiunga na chama.
Lingine ambalo kama mtumishi wa umma huruhusiwi kufanya ni kujishughulisha na siasa muda wa kazi, au kuvaa sare za chama katika muda wa kazi.
Raia Mwema: Katika njia yako kuelekea hapa ulipofika ni jambo gani ambalo unakumbuka lilikupa wakati mgumu na pengine hutalisahau kirahisi?
Dk. Tulia: Katika mambo ambayo yalikuwa magumu kwangu ni wakati nafanya shahada ya tatu ya Uzamivu (PhD). Hiyo ilinipa changamoto kwa sababu ndiyo nilikuwa nimeolewa halafu ikabidi niache mume na kwenda shule.
Katika hali ya kawaida huwa si jambo jepesi hivyo. Watu huwa wanakwenda kusoma shahada ya tatu akiwa hana familia kabisa au akiwa nayo anakuwa ameshazaa halafu anaanza kusoma tena.
Lilikuwa gumu si tu kwangu lakini pia kwa mume wangu na familia, lakini lilienda vizuri. Haya mengine ni changamoto za kawaida.
Raia Mwema: Watanzania wangepeda kujua maisha ya kijamii ya Naibu Spika wao yakoje na namna anavyoweka uwiano kati ya majukumu ya familia na kazi.
Dk. Tulia: Mimi ni mke wa mume mmoja. Tuna mtoto moja ana miaka minne. Namna ya kuweka uwiano wa majukumu ya kitaifa na familia ziko support structures (miundo saidizi), tunasaidina na baba yake kulea. Pamoja na kwamba anafanya kazi lakini muda mwingi anashiriki malezi ya mtoto kwa karibu.
Chanzo: Raia mwema
No comments:
Post a Comment