Social Icons

Wednesday 20 January 2016

Hadithi: Usilie Nadia: 19

ILIPOISHIA
Huko chumbani wakati na mimi nabadili nguo nilikuwa nahangaika na utata wa simulizi hiyo yenye maswali mengi!!
 
Sasa Jesca na Nadia wamekutana Dar!! Hivi huu ndo mwisho wa simulizi ama? Lakini haiwezi kuisha maana hali niliyomkuta nayo Nadia Musoma haikuwa ya kawaida hata kidogo sasa alirudi lini Musoma na ni kwanini nilimkuta katika hali ile?? USIKOSE SEHEMU YA 19


SEHEMU YA KUMI NA TISA
Jesca alinieleza kuwa alikuwa na kiasi cha laki saba katika akaunti yake. Hii ilikuwa inatosha sana, ilikuwa ni wakati muafaka wa kumkabili Desmund ili nimpe salamu kutoka katika ile kuzimu ya baharini ambayo nilikuwa na kisha ikazushwa kuwa nimekufa.
Mzee Matata angeongoza mbio hizi za kunieleza ni nanji huyo alitaka kuniua kabla sijaonana na Desmund mume wangu, kila ambaye angenipa jibu hyakika angekuwa amenisaidia sana. Jesca na mwanaye walisinzia lakini mimi nilichelewa sana kulala.

Mwisho nikalala nikiwa na kauli mbiu, nipo hai ili Desmund akome!....mh!! we G wewe yaani ukinogewaga kusikiliza hata kula hunikumbushi au ndo unataka vidonda vya tumbo visimame hapa tuanze kukimbizana hospitali tena” alisema Nadia hapo nami nikakumbuka kuwa kulikuwa na chakula mbele yetu, nikakifunua.

Ewalaa!! Mapaja mawili ya kuku wa kienyeji, wali mweupe na vidikodiko vingine.
Nadia sahani yake na mimi yangu!!!
Kila mtu kwa mwendo wake akaanza kula!!
 Kila mmoja alikuwa na njaa na hakika tulikisosoa chakula kwa wingi, hata Nadia ambaye hawezi kula chakula kingi alijitahidi sana siku hiyo katika kiwango cha kuridhisha. Kama kawaida hakuna aliyesema na mwenzake hadi tuliporidhika, kijana muhudumu akaleta bili nikalipia.
Hapo sasa hapakuwa mahali sahihi pa kuendelea kukaa, nilimwonyesha ishara Nadia nasi tukasimama na kuondoka tukiwa na chupa za maji yetu. Hatukuelekea chumbani, bali siku hii nilimwongoza Nadia hadi katika fukwe za Ziwa Viktoria, jirani na lile jiwe maarufu ama tuseme mwamba maarufu wa Bismark….
Bismark rock!!
Hapakuwa na jua kali hivyo tukaamua kutembea kwa miguu tukapita kona kadha wa kadha hadi tukafika mahali tulipohitaji. Haikuwa mara ya kwanza kwa Nadia kufika eneo lile, lakini wakati wa mwisho kufika hapo labda alikuwa alikuwa katika kipindi kigumu, sasa mimi nilimpeleka pale kwa dhumuni la kupunga upepo na kuendelea kubadilishana mawazo mawili matatu kama yangetokea.
Hapakuwa na watu wengi sana eneo lile hivyo tulipata nafasi ya kujivinjari tuwezavyo kona kadha wa kadha. 
“Mwenzako nayaogopa maji balaa.” Nilimweleza Nadia baada ya kuwaona vijana kadhaa wakiogelea kwa raha kabisa katika maji yale. Nadia alitabasamu kisha akanieleza kuwa yeye ni rafiki wa maji. Nilikumbuka katika mazungumzo alinieleza juu ya namna alivyoweza nkuogelea na kuwakimbia maadui wale waliokuwa wamemteka na kisha kumtumia katika kusafirisha madawa ya kulevya.
“Yaani hapa ningekuwa na nguo za ziada ungeshtukia tu nipo ndani ya maji.” Aliniambia huku akionekana dhahiri kuwa anayatamani yale maji.
“Wewe jifanye kuyazoea maji, maji ni rafiki na ni adui pia…”
“Unajuaje wakati maji ni rafiki na unajuaje kuwa wakati huu ni adui yakiwa yametulia katika namna ile.” Aliniuliza swali ambalo sikulichukulia uzito hata kidogo.
Lakini nilipotaka kulijibu ndipo nikagundua kuwa swali lile ni gumu.
“Kwa kuyatazama huwezi kujua, lakini ukipatwa na kiu na ukayanywa utautambua uzuri wake na ukukizama humo yakakuua utatuachia nafasi tulio hai kuutambua uadui wa maji.” Nilijaribu kumjibu.
“Kwa hiyo huwezi kutambua kwa kuona sivyo.”
“Naam!!” nilimwambia. 
Hapa akafanya tabasamu kidogo.
“Maji ni kama mwanadamu tu, huwezi kuyatambua madhaifu yake mpaka akufanyie jambo fulani.” Akasita kisha akaendelea huku akiyatazama maji. “Wasichana sisi huwa ni wapumbavu sana, yaani wapumbavu wa mwisho kabisa. Si wote lakini hao wapumbavu wanasababisha wote tuonekane sawa. Lakini ‘ishu’ ipo katika kumjua nani mpumbavu na nani si mpumbavu!! Upumbavu huu kwa silimia kubwa huja tukiwa katika mapenzi yaani kama mazezeta vile, basi wanaume wanatufanya watakavyo. Mwandishi unajua Jesca naweza kumuita mjinga ama mpuuzi wa mwisho. Yaani tumehangaika weee tumeshakaa kwenye mstari tunataka kusonga mbele na maisha yetu yeye anafanya mambo ya kijinga na kusababisha turejee tulipotoka.
Mwandishi, tumesafiri vizuri sana yaani wote tukiwa na lengo moja tu kuanza safari yetu ya kimaisha tukitambua kuwa mtoto anatutegemea sisi hivyo kwa ile pesa iliyokuwepo tulitakiwa kufika na kutulia tujue nini tunafanya. Hakika wote tukaunganisha mikono yetu na kuwa kitu kimojha na wazo moja.
Saa saba za usiku tukaingia Mwanza. Nikasimamia jukumu la kutafuta chumba yeye Jesca na mtoto wakabaki stendi wakiningoja. Baada ya dakika kumi na tano nilikuwa nimelipia chumba tayari.
Safari yetu ya kufika Mwanza ikawa imetimia haswa!! Na palipokucha maisha yetu jijini hapo yakaanza rasmi. 
Nilikuwa namuamini samba Jesca na nilimwona ni mwanamke wa shoka lakini kilichokuwa kinanikosesha amani ni hali yake ya kulialia mara kwa mara na kukosa amani.
Moyo wa mtu ni kiza kinene huwezi kujua nini kinajiri humo ndani. Nami sikujua mwenzangu alikuwa anawaza nini, mimi nilijisikia ama kuishi katika nyumba ya kupanga jijini Mwanza hata kama haikuwa na umeme lakini tulikuwa na uhuru lakini mwenzangu alionekana kama maisha yale haridhiki nayo. Nilijiuliza kama alipenda kulawitiwa ili aendelee kuishi maisha bora nyumbani kwa Bryan ama ni kipi kilikuwa kinamnyima amani. Nilitambua kuwa labda kukatisha chuo ghafla nd’o jambo lililoiathiri akili yake nikajipa moyo kuwa labda atakuja kubadilika.,
Kweli ikawa kama nilivyotaraji!! Lakini ilikuwa ghafla sana
Jesca akaanza kupata furaha tena kama kawaida!! Lakini hii furaha ilikuja ghafla sana mwandishi hadi ikanitia mashaka, inakuwaje furaha kama hiyo upesi kiasi hicho? Sikutaka kumuuliza maana swali langu lingemaanisha kuwa mimi nataka awe mpweke kila siku. Wakati huo tulikuwa hatujaanzisha rasmi kitu cha kutuingizia pesa lakini nilikuwa katika michakato ya kufanya biashara ya ushirikiano na mwanamama jirani aliyekuwa anatengeneza supu ya makongoro.
Furaha ya Jesca ikanifanya nikumbuke kila mtu ambaye nimewahi kumuamini na mwisho kunifanya nijute kumuamini. Nikaamua kuchukua tahadhari, na nilijua kama hiyo furaha ina sababu basi sababu ile haitakuwa mbali sana, yaani ikiwa moyoni basi kuiona ni kazi ngumu sana lakini moyo mwingine usiokuwa na siri ni simu ya mkononi. Siku hiyo nikamtegea Jesca alivyoenda kuoga nikaikwapua simu yake bahati nzuri hakuwa ameifunga kwa namba za siri.
Nikakimbilia katika jumbe alizopokea na kutuma, nikakutana na jina baba watoto!!
Ina maana amepata kimwanaume hapa mtaani ama?? Nilijiuliza.
Lakini nikaamua kuzisoma meseji zile ili niweze kupata jibu.
Walikuwa wanajadiliana juu ya safari ya huyo baba watoto kuja jijini Mwanza. Nikaichukua nama upesi nikahifadhi katika simu yangu ambayo nilikuwa nimeinunua siku chache zilizopita.
Meseji nyingine zilitaja jina langu!! Mariam! Nikashangaa ni nani huyo anayenijua mimi.
Meseji ya muhimu kwangu ikawa kwamba yule mtu hakutaka mimi niambiwe kama anakuja eti kisa anataka kunishtua tu!!
“Mimi nilishasamehe mpenzi wangu na ninawapenda sana, kama Mary lazima nimpe zawadi baada ya kumwomba msamaha.” Aliandika huyo baba watoto. 
Nikairejesha simu baada ya kumsikia Jesca anafunga bafu.
Mwandishi, hakuna kitu kibaya katika haya maisha kama kusalitiwa na yule unayempenda, tena ni heri afanye usaliti na uhadithiwe tu lakini sio kushuhudia. Yaani nilihisi kuwa yuyle anayewasiliana na Jesca atakuwa ni Bryan tu, lakini niliamua kuthibitisha nikatafuta simu nyingine nikampigia ili tu kuhakikisha.
Hakika alikuwa ni Bryan yule mwanaharamu aliyetaka kumlawiti Jesca. Yaani leo hii huyu Jesca ambaye niliumia moyo na kuamua kumwepusha na balaa lile kisha tukatoroka na kujiwekea ahadi kuwa hatutakaa tuwasiliane na Br4yan ama familia yake iwapo atakuwa amekufa!
Sasa Jesca anawasiliana na mwanaharamu……
Si nilisema wasichana sisi ni wapumbavu, wapumbavu wa kutupa mwandishi, hivi unamwamini vipi mtu aliyetaka kukulawiti bila huruma, unaanza vipi kumwamini mtu ambaye tulitaka kuupoteza uhai wake?? Kibaya zaidi sasa tulikubaliana kwa pamoja kuwa hatutawasiliana na Bryan lakini katika kuwasiliana naye akaamua kufanya mwenyewe, kwa hiyo mimi sikuwa na maana tena baada ya hayo yote tuliyopanga.
Nililia sana mwandishi. Nililia sana kwa sababu nilikuwa nimesalitiwa, tena nimesalitiwa na mtu ambaye ninamuamini.
Niliamua kujifanya naumwa ilimradi tu Jesca asijue ni kiasi gani amenikwaza na kunitia jeraha!!
Wanawake!! Dhaifu sana sisi, yaani dhaifu hadi kero.
Yaani mapenzi huwa yanakuwa mzigo sana kwetu, nd’o maana wasichana hujikuta wakiwaamini wapenzi wao kuliko wazazi wao wa kuwazaa. Eti kisa tu mpenzi amemuahidi kumuoa. Nayasema haya kwa sababu hata mimi niliwahi kuwa mpumbavu!!
Sikutaka Jesca naye awe mpumbavu, lakini ni kama alikuwa mpumbavu tayari. Ningeanza vipi kumwambia kuwa nilichukua simu yake na kusoma meseji zake. Angenionaje??
“Mariam…kesho nitatoka kidogo mwenzako yaani kuna rafiki yangu nilisoma naye jana kama mchezo nimejaribu anapatikana kwenye simu anakaa huko Airport. Ngoja nikaonane naye dada yangu, maana haya maisha hatutaweza na pesa hiyoo inaisha” Jesca aliniambia wakati tunapata chakula. Nilijisikia hasira sana kwa sababu alikuwa ananidanganya. Kwa nini Jesca ananidanganya wakati mimi nilikuwa muaminifu kwake nikamwokoa asikamatwe na majibu ya mtihani ilhali simjui?? Mbona niliendelea kuwa muaminifu kwake na nikaiweka roho yangu rehani ilimradi nimwokoe asilawitiwe?
Yaani ameshindwa kulipa uaminifu kidogo tu!! Jesca Jesca!!
Sikuweza kuendelea kula tena, nikasingizia kichwa kinaniuma. Nikajitupa katika godoro nikalala.
Nilisinzia nikiwaza jambo moja tu, kama Jesca ameamua kujipeleka katika domo la mamba basi mimi sitakubali hata kidogo Jonas naye atumbukie humo. Alikuwa mtoto mdogo sana kuingia katika kashkash.
 Kesho yake majira ya saa nne asubuhi nikamwona Jesca akimwandaa Jonas, nikamsubiri niisikie kauli yake, majira ya saa tano akataka kutoka na Jonas. Nikamzuia, hakuna kwenda na mtoto huko kwa rafiki.
“Jesca jicho linanichezacheza hautaenda na mtoto kwa kweli kama jicho linanicheza kwa mabaya basi yakusibu wewe mtu mzima utajua kujiokoa lakini Jonas tutakuwa tunamwonea” niliunda uongo.
Alidhani natania lakini kwa mara ya kwanza nikamkunjia sura. Akaogopa akaniaga akiahidi kuwa akirejea nitatabasamu na jicho litaacha kucheza.
“Nakupenda Jesca.” Hilo lilikuwa neno la mwisho kumwambia, akaondoka na sikuwahi kumwambia neno jingine tena.
Alipoondoka na mimi nikaondoka nikiwa na Jonas na akiba ya pesa yote iliyokuwa imebaki. Nikaufunga mlango vyema, nikaweka funguo mahali anapopafahamu Jesca kisha nikaondoka. Nikampeleka Jonas kwa mama ambaye nilikubaliana naye kuungana katika biashara ya makongoro. Uzuri wa Jonas hakuwa akichagua mtu, hakuwa mtoto wa kulialia hovyo labda awe anaumwa.
Nikamwomba mama yule amuhifadhi pale hadi nitakaporejea, akakubali nikamwachia shilingi kadhaa kwa ajili ya dharula kama tu itajitokeza.
Sasa nikarejea kuwa shuhuda wa kitu ambacho kitaenda kutokea, imani yangu ilikuwa ndogo sana kumwamini Bryan niliyempasua na chupa kichwani, lakini ningemsaidia nini Jesca wakati wahenga walisema mkataa pema pabaya panamuita!!
Nilijiweka mahali pazuri nikawa natazama ugeni huo kama utakuja kwa amani.
Muda ulizidi kwenda bila matokeo yoyote.
Saa tisa za alasiri ndipo nikapokea simu kutoka katika namba ya Jesca.
“Mambo dada Mariam, nitachelewa kurudi, si Jonas yupo, niwaletee nini nikija.?” Alijiumauma Jesca, nikajikuta natabasamu kwani nilijua kuwa tayari hakuwa huru tena Jesca. Kitu nilichokuwa nawaza.
Majira ya saa kumi na mbili akanipigia simu akaniuliza kama nipo nyumbani. Kitu ambacho hakikuwa cha kawaida kabisa kwa Jesca, nami nikaendelea kutulia tu. Majira ya saa mbili usiku gari mbili zikafunga breki katika nyumba tuliyokuwa tumepanga. Wakaruka wanaume kwa fujo!! Jicho langu likamuona Jesca, alikuwa amelowa damu, na kisha nikamuona Bryan alikuwa ameiva kwa hasira kali. Nikajilazimisha kutabasamu maana sikuweza na nafsi iliniambia kuwa nitakuwa mjinga kumsaidia mpumbavu!!
Nikatoweka kimyakimya huku nikiwaachja wajinga hao wakitangaza kuwa ‘Mariam popote pale ulipo jitokeze’
Nikaondoka huku nikiumia sana hakika kwa hali aliyokuwanayo Jesca, usiri wake na kuamini mapenzi ya kijinga kulimponza. 
Nilifika nyumbani kwa yule mama majira ya saa nne usiku, nikamchukua Jonas na kuondoka naye. 
Hapo nikakumbuka kuwa nilikuwa nimelaaniwa na huenda ile laana ya mama ilisema kuwa nitaishi kama kivuli sitatulia wala kupata amani, hakuna atakayenipenda hata kidogo licha ya kujipendekeza kwake.
Naam!! Nilikuwa mkimbizi tena.
Nikalala nyumba ya kulala wageni pamoja na Jonas!!
“Jonas, sijui kama utamuona mama yako tena. Nasema sijui kwa sababu anajua mwenyewe ni wapi alipo. Hautakaa utulie tena maana utaandamana na mwenye laana Nadia, hautatabasamu tena kwasababu upo na nyumba ya kilio Nadia, hautakuwa na uhuru kwa sababu upo na mfungwa Nadia. Lakini kikubwa amini kuwa huyu mfungwa atakufa naye atakuacha, lakini hatakufa kizembe kama mmama yako, hatashikika kipuuzi kwa mapenzi na kubwa zaidi akifa atakuacha ukiwa katika mikono ya yeyote yule ambaye hajalaaniwa. Utamuita mama naye atakuita wewe mtoto wake. Sitakuacha Jonas hadi roho yangu itakapouacha mwili!!!” nilizungumza na kitoto kile kilichokuwa kinanitazama tu bila kusema chochote!!
Asubuhi nilikuwa mkiimbizi kuelekea mahali pengine!! Mwanza haikunifaa tena, mropokaji aitwaye Jesca angeweza kunichoma.
Nikazima simu yangu na kusahau kabisa kama niliwahi kuwa na simu!!!”…akasita Nadia akatazama kushoto na kulia.
“Wee G hapa huwa pabaya usiku wanakaba sana mwenzangu na hii afya yangu mgogoro wasije wakaniua bure….” Kauli hii ikanishtua, kweli palikuwa na giza na tulikuwa tumebaki watu wachache sana, tukasimama na kujikongoja tukapata teksi kwa ajili ya kuturudisha hotelini.
Kila mmoja alikuwa kimya!!
 Nilikuwa na swali moja kubwa. Nadia alisema kuwa hatamwacha Jonas hadi yeye afe kwanza, sasa mbona Jonas hayupo na yeye yupo hai?? 
Nini kilitokea na kusababisha haya!!!
Na nini hatima ya Jesca…….

No comments:

 
 
Blogger Templates