Social Icons

Wednesday 20 January 2016

Hadithi: Usilie Nadia: 20



“Jonas, sijui kama utamuona mama yako tena. Nasema sijui kwa sababu anajua mwenyewe ni wapi alipo. Hautakaa utulie tena maana utaandamana na mwenye laana Nadia, hautatabasamu tena kwasababu upo na nyumba ya kilio Nadia, hautakuwa na uhuru kwa sababu upo na mfungwa Nadia. Lakini kikubwa amini kuwa huyu mfungwa atakufa naye atakuacha, lakini hatakufa kizembe kama mmama yako, hatashikika kipuuzi kwa mapenzi na kubwa zaidi akifa atakuacha ukiwa katika mikono ya yeyote yule ambaye hajalaaniwa.

 Utamuita mama naye atakuita wewe mtoto wake. Sitakuacha Jonas hadi roho yangu itakapouacha mwili!!!” nilizungumza na kitoto kile kilichokuwa kinanitazama tu bila kusema chochote!!


Asubuhi nilikuwa mkimbizi kuelekea mahali pengine!! Mwanza haikunifaa tena, mropokaji aitwaye Jesca angeweza kunichoma. Nikazima simu yangu na kusahau kabisa kama niliwahi kuwa na simu!!!”…akasita Nadia akatazama kushoto na kulia.

“Wee G hapa huwa pabaya usiku wanakaba sana mwenzangu na hii afya yangu mgogoro wasije wakaniua bure….” Kauli hii ikanishtua, kweli palikuwa na giza na tulikuwa tumebaki watu wachache sana, tukasimama na kujikongoja tukapata teksi kwa ajili ya kuturudisha hotelini.
Kila mmoja alikuwa kimya!!

Nilikuwa na swali moja kubwa. Nadia alisema kuwa hatamwacha Jonas hadi yeye afe kwanza, sasa mbona Jonas hayupo na yeye yupo hai??
Nini kilitokea na kusababisha haya!!!
Na nini hatima ya Jesca…….

Tulifika hotelini, nikatarajia Nadia atakuwa amechoka na atahitaji kulala moja kwa moja. Lakini haikuwa kama nilivyotarajia, badala yake akaungana nami katika chumba changu kwa mara ya kwanza tangu tuwe katika hoteli ile ya G G jijini Mwanza.
“Nikajua unaenda kulala.” Nikamwambia, hapo akanitazama kisha akanieleza kuwa hakuwa na usingizi wa kulala mapema kiasi kile.
“Usingizi nilikuwa nao enzi zile lakini sasa hapana, yaani usingizi kitu cha ajabu mfano unakuwa unahitaji kulala lakini hauupati, na ukiwa na mambo ya msingi ya kufanya nd’o unakuandama. Leo nilitaka kulala mapema lakini ndo basi tena.” “Au kibaridi hiki kinakusumbua?” nilimuuliza huku akiwa amekaa kitandani nami nikiwa katika kiti.

“Hii nayo utaiita baridi, achana na Mbeya na Iringa. Kuna baridi kali sana kule, hili linaweza kuitwa joto na mtu anayetoka huko. Mara yangu ya kwanza kwenda niliteseka sana, na hata nilipokuja kuzoea nilikuwa nimesota haswa. Halafu bora basi ningeteseka peke yangu, mbaya zaidi nilikuwa na mtoto, mtoto asiyejua kusema badala yake analia tu. Unashindwa kuelewa kuwa huyu anahisi baridi ama ana njaa ama anaumwa, yaani nilikuwa najikuta nalia wakati mwingine, mbaya zaidi ya yote Nadia mimi sikuwahi hata kulea mtoto asiyekuwa wangu. Na kubwa zaidi sijawahi kuwa mama. Labda nililaaniwa hivyo ili laana ya mama iishie kwangu tu isimwandame na mtoto ambaye nitamzaa. Sasa nilikuwa na mtoto mdogo.

Mama Aswile hakujali kama nilikuwa nina mtoto, alinilaza katika chumba kisichokuwa na chandarua na mbaya zaidi hata chakula kilikuwa kidogo sana na kisichostahili kuliwa na mtoto mdogo. Sikuweza kujilaumu kwa kuwa katika mkoa wa Mbeya bali nilijilaani tu kwa nini nilizaliwa.
Lakini zaidi nilimlaumu Jesca ambaye sikujua kama yu hai ama ni marehemu tayari, bila Jesca kunisaliti wala tusingekuwa hapo lakini Jesca akaendekeza mapenzi na hatimaye kilio kinakuwa cha mtoto, unadhani ghafla kiasi kile ningewezaje kupata akili ya ghafla ya kujua nini natakiwa kufanya?, mjini Musoma nilijua hapanifai ikiwa sijajipanga, Mwanza ndo hivyo Bryan atakuwa ananisaka, Dar es salaam napo hapakunifaa maana ndo yalikuwa makazi ya Bryan, hivyo nikajikuta katika sintofahamu. Nikaendelea kuishi na Bryan pale nyumba ya kulala wageni kwa siku zaidi ya tatu na hapo nikawa nimeamua kwenda katika wilaya ya Magu nje kidogo ya jiji la Mwanza. Na hapa nikaendelea kuitwa Maria mama mama Jonas.
Huku nilifikia nyumba ya kulala wageni na kisha nikawa nazurura na Bryan nikitafuta walau kazi za ndani ilimradi nipate sehemu ya kulala bure huku nikitafakari nini cha kufanya na pesa yangu ambayo ilikuwa inayoyoma.
Labda ningekuwa peke yangu ningeweza kwenda Musoma ama popote na kujificha nikifanya lolote niweze kula, lakini sasa nilikuwa na mtoto. Mtoto ambaye nilimuapia kuwa sitamwacha pekee hadi nife. Kiapo changu kikawa kinaniandama na kunifanya nijilazimishe kuizoea hali.
Nikabahatika kupata kazi katika banda la mama ntilie maarufu wilayani Magu, Mama Ntuzu. Nilimweleza shida yangu akanielewa na hapo nikaanza rasmi kushughulika katika banda lake, uzuri wa Jonas kama nilivyokwambia awali hana tabia ya kuchagua nani ambebe na nani asimbebe, yaani halii hovyo. Akilia ujue kuna jambo linamkabili. Hivyo nilikuwa namkabidhi kwa mtu ananisaidia kumbeba iwapo anataka kulala, na wakati mwingine anajumuika na watoto wenzake katikia kucheza, hapo akiwa na miaka takribani miwili.

Tatizo lilikuwa moja tu, kwa siku nilikuwa nalipwa shilingi elfu tatu na bado nilikuwa naishi nyumba ya kulala wageni, hapo nilikuwa nalipia chumba shilingi elfu tatu pia. Hivyo pesa yangu yote ilikuwa inaishia katika nyumba za kulala wageni.

Muda si mrefu nikapata rafiki akanieleza kuwa anaishi peke yake, akanizoea nikamzoea na mwisho akanikaribisha kwake. Kilikuwa chumba kimoja, nikajitoa mhanga nikamnunulia Jona kigodoro chake halafu mimi nikawa nalala na Hamida katika godoro moja. Hamida hakuwa mtu wa makuu, aliniheshimu nami nikamuheshimu na ni huyu aliyeniunganisha na mzee Aswile ambaye alinichukua hadi jijini Mbeya kwa ajili ya kufanya kazi za ndani. Nilimweleza kuwa nina mtoto lakini hakujali kuhusu hilo alionekana kumwamini sana Hamida ambaye alikuwa amempa sifa kemkem kuhusu mimi. 

Nikaagana rasmi na Hamida nikatoweka nikiambatana na mzee Aswile kuelekea Mbeya. Tulisafiri kwa kutumia gari lake binafsi, nilikuwa najiuliza maswali kwanini mzee yule atoke mbali kote huko na mwisho kunichukua mimi kwa ajili ya kumfanyia kazi za ndani lakini sikupata majibu. Nafsi yangu ilikuwa na amani zaidi kuishi mbali na sehemu zote ambazo nilikuwa na mikasa, na Mbeya ilikuwa sehemu nzuri zaidi.

Nilipokelewa kwa furaha na familia nzima, wakazoea kuniita dada, mama mwenye nyumba alikuwa kama mama yangu nilimweshimu na yeye akanionyesha heshima waziwazi.Mtoto wa Jesca ambaye alihesabiwa na kutambulika kama mtoto wangu alikuwa na furaha kama amezaliwa katika familia hiyo.

Tukuyu ikanizoea na mimi nikaizoea. Nikanawiri na kujiona mwanadamu mwenye baba na mama pamoja na wadogo na dada zangu. Familia ya mzee Aswile ikawa kama nyumbani nilipozaliwa.

Raha zile zikanifanya nisahau tetesi ambazo aliwahi kuniagusia mvulana wa kazi kuwa mzee Aswile na mkewe hawana maelewano mazuri sana baada ya mimi kufika pale, mkewe alikuwa akimtuhumu kuwa yule Jonas anayeaminika kuwa ni mtoto wangu, basi nilizaa na mzee Aswile tuhuma ambazo mzee Aswile alizikataa na kisha kumkanya mkewe asije akanibughuzi.

 Aliniambia pia kitu ambacho nilikuwa sikijui, kumbe wale watoto wote pale nyumbani si wa mama yule, bali mama wa wale watoto alikufa katika mazingira ya kutatanisha na mama huyu wa sasa hakubahatika kupata mtoto.
Niliyapuuzia na kuyasaha maneno yale hasahasa baada ya kijana yule kunitaka kimapenzi, hivyo nikagundua kuwa kumbe ile ilikuwa janja yake tu ya kunishawishi.
Maisha yakaendelea na yakasahaulika aliyonambia kijana yule, sikuona chuki yoyote kutoka kwa yule mama na familia nzima ilinipenda.

Jonas akamzoea sana mzee Aswile naye mzee akawa anamfanyia mambo ambayo hata watoto wake baadhi hakuwa akiwafanyia. Niliifurahia sana familia ile, lakini sikujua kama itafika siku ya mimi kuanza kulia tena na kuishi kama mkimbizi.

Usiku huu Jonas alikuwa mtu wa kulialia na kukosa raha, nilishangazwa sana na hali hiyo, si mimi hata mtoto mmoja wa mzee Aswile aliyekuwa anapenda sana kunitembelea chumbani kwangbu alishangaa, hatimaye akasinzia. Lakini saa tisa usiku akaamka tena na kuanza kulia huku akijinyonganyonga huku na kule, nikastaajabu, haikuwa kawaida hata kidogo kwa Jonas. Nikamuuliza alichokuwa anataka, sasa aliweza kusema neno moja tu ‘babuuu’ alikuwa akimtaka babu yake, nikajua ni mambo ya watoto haya kulilia hata visivyowezekana, nikambembeleza sana mwisho akalala, lakini hakudumu sana akaamka tena na kuendelea kunisumbua. Sasa nikaamini Jonas atakuwa anaumwa, nikafikiria kuwa pakikucha niangalie utaratibu wa kumpeleka hospitalini.

Kilio cha Jonas cha saa kumi na moja mara kikaambatana na kilio kingine kutoka kwa mtu nisiyemfahamu, mara mwingine na mwingine na hatimaye mimi naye nikaungana nao.
Tuliongana kumlilia mzee Aswile, kwani hakuweza kuamka tena tangu alivyolala usiku. Mzee Aswile alikuwa amekufa!!

Mwandishi, nililia sana lakini sikumfikia Jonas ambaye ni kama alijua jambo lililotaka kutokea tangu usiku wa manane. Mzee Aswile akazikwa huku tukisema kuwa sisi ni mavumbi na mavumbini tutarudi. Na hapo ukaanza ule wakati wa kujuta na kishga kukumbuka kuwa umelaaniwa, wakati wa kuyakumbuka maneno ya ‘;shamba boy’ juu ya yule mama. 

Ulianza ugeni, wakaja ndugu wa yule mama. Nikatolewa katika chumba nilichokuwa na lala na kisha kuhamishiwa chumba cha nje. Mara kila mara kugombezwa hata ninapofanya jema, baadaye inavyoonekana watoto walihoji kulikoni. 

Naam!! Yule mam akawaambia kuwa baba yao alikufa kwa kulishwa sumu, na chakula hicho nilikipika mimi, nilimlisha sumu ili Jonas aweze kurithi mali. Kwa kuwa wote walikuwa wasichana basi Jonas ambaye ni mtoto haramu ninayemsingizia kuwa wa marehemu angeweza kurithi mali zote. Maneno hayo aliniambia mtoto mkubwa wa marehemu siku moja baada ya kukasilishwa na uwepo wangu sebuleni, alisema kwa uchungu na kisha akaniita shetani. Mama mwenye nyumba alikuwa amewajaza sumu watoto wale.

Hapo sasa nikaanza kuchukiwa!!
Nikabaini kuwa nilibweteka na sikuwa na utaratibu wa kujitunzia pesa, nilijiona kama nipo nyumbani kwetu. Pesa ya nini?? Chumba nilichohamishiwa hakikuwa na kitanda na enzi za uhai wa Aswile katika chumba kile bata na kuku wagonjwa walitengwa na wengine kwa kuhifadhiwa ndani ya chumba kile.

Niatakiwa kuishi mule, ni hapo nikagundua kuwa sikuwa na ile thgamani tena iliyokuwepo awali. Maneno ya shamba boi yakaendelea kujirudia kichwani mwangu, nikajua moja kwa moja kuwa mama yule alikuwa amemuua mumewe kutokana na wivu mzito wa kimapenzi. Lakini nani angeniamini iwapo nilikuwa nimerushiwa kesi ile.

Ugumu wa maisha ukaanzia hapo, nikahesabiwa siku niwe nimeondoka pale. Nikaomba nipewe mwezi mmoja. Hakika ulikuwa mwezi mmoja lakini ni kama mwaka mzima kwa tabu nilizopitia. Nilitukanwa mimi na Jonas, tulilishwa makapi, sikuruhusiwa kuingia sebuleni na mbaya zaidi sikutakiwa hata kupika chakula. Watoto wakadai nitawaua wao pia.

Wakavuka mipaka wakaanza kumuita Jonas mwanaharamu. Hapo sasa wakaitibua hasira yangu na kunirudisha miezi kadhaa nyuma miezi ambayo hasira ilikuwa kando nami na iliweza kufanya kazi muda wowote.
Jonas mwanaharamu!!!

Monica, mtoto mkubwa wa marehemu mzee Aswile alikuwa wa kwanza kutambua upande wa pili wa Nadia. Siku hiyo Jonas akiwa mtoto hajui kama tumekatazwa kuingia sebuleni aliingia na kujibweteka katika kochi akawa anaangalia luninga, mimi nilikuwa nafua nguo zake na zangu.
“Mwanaharamu mkubwa wewe unakanyaga hayo makochi unasaidia kufua??” nilisikia sauti ya Monica akigomba. Nikasita kufua nikatazama huku na huko, Jonas hayupo. Kule ndani nikazidi kusikia Monica akigomba. Masikio yangu mara yakasikia Jonas akitoa kilio kikali.

Mbiombio nikakimbilia ndani, Jonas alikuwa analia kwa uchungu huku akiwa amejishika shavu. Aliponiona akanikimbili na kunikumbatia huku akiwa analia, aliponikumbatia akawa ameachia lile shavu.

Macho yangu yakaona alama za vidole vya mtu mzima.
Monica alikuwa amemnasa kibao Jonas.
Na hapo nikaisikia sauti ya Jonas akilaumu kitoto toto.
“Mama huyu pigaaaa….” Ilikuwa ni sauti ya kitoto lakini iliyotangaza uchungu. Nikanyanyua macho yangu na kumtazama Monica, nikamkuta akiwa ametingwa katika kufanya lolote alilokuwa akifanya katika luninga.
Mbiombio nikamvamia, yeye na luninga wakaenda chini, nikamweka vyema uso wake, na hapo nikamgeuza kitoweo changu. Nilimpiga haswa!!

Akaja na mdogo wake nikawachanganya wote, nilikuwa na hasira kali kupita nyingine zilizopita.
Nilijua kuwa sihitajiki tena katikia mji ule, nami niliomba mwezi mmoja niweze kuondoka wakanikubalia. Sasa wanamuita Jonas mwanaharamu!!
Gusa pengine usimguse mtoto huyu, nililaaniwa mimi na si Jonas!!

Wakati natoka mlangoni nikakutana na mama Aswile. Sikujali lolote nikaelekea katika chumba changu, nikakusanya nguo zangu huku nikiwa natetemeka, Jonas akiwa mgongoni. Nikasikia chumba kikivamiwa, ni jambo nililolitarajia. Haraka nikageuka nikakutana na mama Aswile. Alikuwa amevimba huku akiwa ameshika mwiko. Taratibu nikamshusha Jonas. Halafu nikahamishia balaa kwa mama mAswile, nilimpiga huku nikimtuhumu kuwa amelaaniwa kwa kuwafanya watoto wake wanichukie bila sababu. Nilihakikisha amenyooka.

Baada ya hapo nikabeba kilicho changu na kuingia katika mitaa ya Tukuyu nikiwa na shilingi elfu tano tu!!
Pesa niliyoipata baada ya mama Aswile kuiangusha akijaribu kukabiliana na mimi!!
Jonas mgongoni, kibegi kidogo mkononi!!
Nikaingia katika mitaa yenye baridi kali. Sina ndugu wala rafiki!!.........USIKOSE SEHEMU YA 21

No comments:

 
 
Blogger Templates