Uhusiano wa cRais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu umepata pigo jipya baada ya Netanyahu kukataa mwaliko wa Marekani masaa machache kabla ya Makamo wa Rais Joe Biden kuwasili Israel.
Uamuzi wa Netanyahu kukataa mwaliko wa Marekani kwa mazungumzo na Rais Obama mjini Washington baadae mwezi huu umeishangaza Ikulu ya Marekani ambayo imefahamu juu ya uamuzi huo kupitia taarifa za vyombo vya habari.
Ofisi ya waziri mkuu wa Israel imetetea uamuzi huo kwa kusema Netanyahu alikuwa hataki kujiingiza katika uchaguzi wa mchujo unaoendelea kufanyika nchini Marekani kuteua wagombea watakaowakilisha vyama vyao katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwezi wa Novemba.
Kinyume na kile kilichorepotiwa na vyombo vya habari Ikulu ya Marekani imesema ilikuwa imepangwa Netanyahu akutane na Obama Machi 18 kabla ya rais huyo kuanza ziara ya kihistoria nchini Cuba tarehe 21 na 22 Machi.
Kuanza kwa tafrani
Hapo mwaka 2012 Netanyahu alimkaribisha nchini Israel mgombea wa urais wa chama cha Demokrat Mitt Romney kwa kile Wademokrat wengi walichokiona kuwa ni jaribio la kumvurugia Obama asifanikiwe kuwania muhula wa pili.
Gazeti mashuhuri nchini Israel la Yediot Ahronot limekariri duru zilio karibu na Netanyahu zikisema sababu nyengine inayomfanya waziri mkuu kutokuwa na hamu ya kukutana na Obama ni kwamba anataka kuahirisha utiaji saini makubaliano ya msaada wa kijeshi na Marekani na kwamba angependelea kufanya shughuli hiyo na rais mpya ajaye.
Uhusiano kati ya viongozi hao ulifikia kiwango cha kuharibika kabisa hapo mwezi wa Machi mwaka jana wakati Netanyahu alipolihutubia bunge la Marekani na kushutumu vikali makubaliano ya nyuklia yaliofikiwa na Iran mwaka huo.Hatua hiyo ilichukuliwa kuwa ni kutaka kuudhofisha utawala wa Obama ambao ulikuwa ukishinikiza kufikiwa kwa makubaliano hayo na ni kuingilia kati siasa za Marekani.
Ziara ya Biden
Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden alipoutembelea Msikiti Mkuu wa Sheikh Zaid Umoja wa Falme za Kiarabu (07.03.2016)
Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa kuwasili Tel Aviv baadae Jumanne na kuwa na mazungumzo na Netanyahu hapo kesho pia anatarajiwa kukutana na Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas.
Ziara ya mwisho ya Biden nchini Israel hapo mwaka 2010 ilichafuliwa na tangazo la mradi mkubwa wa makaazi ya walowezi huko Jerusalem ya Mashariki ambayo Israel inaikalia kwa mabavu.
Ziara yake safari hii inafanyika wakati Obama akikiri kwamba hakutakuwepo kwa makubaliano kabambe kati ya Waisrael na Wapalestina kabla ya yeye kuondoka madarakani mwezi wa Januari mwaka 2017.
Ikulu ya Marekani imesema Biden hatojishughulisha na juhudi zozote zile kuu za kutafuta amani wakati wa ziara yake hiyo licha ya kuibuka kwa wimbi la matumizi ya nguvu tokea mwezi wa Oktoba ambapo watu 200 wameuwawa.
Alipokuwa Umoja wa Falme za Kiarabu hapo Jumatatu Biden amesema Marekani itabidi ilisambaratishe kundi la Dola la Kiislamu na kulitokomeza kutoka Iraq na Syria.
Chanzo: Dw.de
No comments:
Post a Comment