Marekani imeishutumu serikali ya Sudan Kusini kwa kuhujumu juhudi za kuwasili kwa kiongozi wa waasi Riek Machar mjini Juba ili kuunda serikali ya mseto. Machar anatarajiwa kuwasili leo.
Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar alitarajiwa kuwasili mjini Juba siku ya Jumamosi akitokea Ethiopia lakini serikali ya Rais Kiir iliizuia ndege ya Machar kutua katika uwanja wa ndege wa Juba.
Machar ambaye anatarajiwa kuchukua wadhifa aliokuwa akiushikilia kabla ya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe wa makamu wa Rais katika serikali ya muungano sasa anatarajiwa kuwasili hii leo.
Pande zote mbili haziheshimu makubaliano
Hata hivyo mjumbe maalumu wa Marekani nchini Sudan Kusini Donald Booth amesema kuchelewa mara kwa mara tangu wiki iliyopita kwa kiongozi huyo wa waasi kuwasili Juba kunazusha mashaka kuhusu kujitolea kwa pande zote mbili zinazozana kuheshimu makubaliano ya kuleta amani.
Booth amesema kutowasili kwa Machar siku ya Jumamosi ilikuwa ni mara ya tatu katika kipindi cha wiki moja iliyopita ambapo mipango ya kuwasili kwake ilitibuka kutokana na sababu moja au nyingine.
Wiki iliyopita Machar alikataa kurejea Juba kuunda serikali na Rais Kiir kutokana na kukataliwa kwa matakwa yake ya kuwasili na wanajeshi zaidi na silaha nzito. Baadaye serikali ya Sudan Kusini ilitoa taarifa kuwa sasa Machar na walinzi wake wanaweza kuwasili katika uwanja huo wa ndege bila ya pingamizi lolote.
Je Machar na Kiir watasikilizana?
Utekelezaji wa makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwezi Agosti mwaka jana yanahitaji kuundwa kwa serikali ya muungano ya mpito ambayo inahitaji kuwasili kwa Machar mjini Juba.
Marekani imeonya kuwa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana hapo kesho kuujadili mzozo huo wa Sudan Kusini na huenda pande zote mbili zikawekewa vikwazo zaidi na Jumuiya ya kimataifa.
Vita vilizuka katika taifa hilo changa zaidi duniani mnamo mwezi Desemba mwaka 2013 baada ya Rais Kiir kumshutumu aliyekuwa makamu wake wa Rais, Machar kwa kupanga njama ya kumpindua madarakani.
Jumuiya ya kimataifa ikiongozwa na Marekani, Uingereza, China na Norway ilikuwa imeweka muda wa mwisho kwa Machar kuwasili Juba kuwa Jumamosi la sivyo uchukue hatua dhidi ya viongozi hao wa Sudan Kusini.
Maelfu ya watu wameuawa na zaidi ya watu milioni mbili wameachwa bila ya makaazi kutokana na vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe.
Mamia ya raia wa Sudan Kusini hapo jana walifanya maombi maalamu ya kuliombea taifa lao amani. Waumini wa kanisa parokia ya Emmanuel mjini Juba wamesema wanatumai kuwaisli kwa Machar kutaashira ukurasa mpya wa kukomeshwa kwa vita.
Chanzo. Dw.de
No comments:
Post a Comment