Social Icons

Monday, 25 April 2016

Dr. Kitima: kukataa mkate wa masimango ndio kujenga heshima yetu

SERIKALI ya Awamu ya Tano imeonyesha dhamira ya kuondokana na misaada yenye masharti ya fedheha, Mwandishi Wetu DEUS BUGAYWA, amefanya mahojiano na Dk. Charles Kitima kuhusiana na dhamira hiyo na utayari wa Watanzania kuachana na misaada ya aina hiyo. Endelea:
Raia Mwema: Rais John Magufuli ameweka bayana msimano wake kuhusu misaada ya masharti magumu, akiifananisha na ‘mkate wa masimango’, unadhani kama taifa tuko tayari kiasi gani kuvumilia wakati mgumu utakaotokana na msimamo huo?

Dk. Kitima: Niseme kwamba Tanzania ina historia ya kushirikiana na mataifa yote, kusaidiwa na kusadia, lakini pia haipendi kushinikizwa katika misaada. Taifa lolote linapoleta misaada kwa kushinikiza tunao uwezo wa kuamua cha kufanya. Tanzania sera yake ni ya kutofungamana na yeyote eti kwa sababu tunahitaji msaada wake, hiyo ndiyo inayotuongoza kufanya uamuzi ambao Rais amesema, kama tunataka kushirikiana tushirikiane wakati taifa lina heshima yake kwa maana kwamba ni taifa linalojitawala na haliko tayari kubadili sera au mitazamo yake ya kisheria kwa sababu ya misaada. Kwa hiyo haina maana kwamba msimamo uliotolewa na serikali wa kusema masharti magumu yanayowekwa na wafadhili yatufanye tukatae misaada, hapana, suala ni kwamba lazima taifa kama taifa tubaki na msimamo wetu na anayetaka kuendelea kushirikiana na sisi aangalie pia misimamo yetu, lakini tunaedelea bado kushirikiana na tumeweza kushirikiana kwa miaka yote tangu tuwe taifa huru, pamoja na kuwa na msimamo huo na nyakati ndiyo hizo kwamba mtu atakapoona hatutaki kulegeza masharti ya misimamo yetu ya kitaifa na hatutaki kubadili sera zetu basi akiamua kutunyima huo ni uamuzi wake, lakini sisi hatutamki ili atunyime tunatamka ili kuonyesha kwamba nchi inaogozwa kwa sera zake na sheria zake na ni taifa huru ambalo lina mamlaka ya kujipangia sheria zake na mambo yake.

Raia Mwema: Wahega walisema anayemlipa mpuliza zumari ndiye anachagua wimbo, na watoa misaada nao wanaongozwa na kanuni hiyo, ukitaka misaada kubali masharti yao.
Dk. Kitima: Ni kweli wanaotoa misaada au mikopo ambayo lazima tunaihitaji kwa ajili ya maendeleo, maana hata nchi zilizoendelea zinahitaji misaada, wana masharti yao lakini misaada ambayo inaletwa kwa masharti ya kufanya taifa lishindwe kujiamuria mambo yake na kuanza kukosa ule uhuru wa kujipangia mambo yake hiyo misaada kwa kweli inakuwa inakiuka hata ile haki ya watu kujitawala.
Raia Mwema: Msimamo huo unamaanisha upo uwezekano wa kukosa baadhi ya misaada ili kulinda uhuru wetu na haki ya kuamua mambo yetu, Watanzania ukiwaangalia unaona wanao uwezo wa kuvumilia kupata shida kwa ajili ya heshima ya uhuru na utu wao?

Dk.Kitima: Watanzania wote ninaamini wako pamoja na Rais katika kulinda uhuru na haki yetu ya kujiamuria mambo yetu, na hata wale wafadhili ambao wanataka kushirikiana na sisi katika jitihada za kutatua matatizo yaliyoko katika nchi yetu kwa ajili ya malengo yao, wanatambua kuwa sisi ni taifa linalojitawala na tuna malengo yetu na Watanzania wana haki ya kutofungamana na masharti yoyote, maana kukubali masharti yanayovunja haki yetu ya kuamua mambo ni kuonyesha kwamba taifa linahama katika utawala wa watu wenyewe na wa kidemokrasia. Kwa hiyo Watanzania wako na Rais kwa kweli, hatuna hofu yoyote juu ya hilo kwa sababu hakuna mtu atakayeacha kushirikiana na sisi kwa sababu ya msimamo huo, kwa sababu kukataa misaada ya masharti yanayoingilia uhuru wenu (makate wa masimango) huo ni msimamo wa mataifa yote makini na ndiyo maana hata sasa hivi mmoja atajitoa mwingine ataendelea, kwa taifa linaloheshimu utashi wa watu halitaacha kusaidia watu kwa sababu wamesimamia msingi ambao unaongoza utawala wa kidemokrasia duniani, kwa hiyo anayeweka masharti yeye mwenyewe ndiyo anakuwa anakiuka utawala wa watu katika kujiamuria mambo yao na amsharti yake kama hayaheshimu zile haki za kisiasa za raia, haki za kiraia za wananchi, huo msaada na hilo taifa wanakuwa wanakiuka haki za wengine. Busara za kidemokrasia zinataka watu wajiamurie mambo yao ili mradi wanaongozwa na haki za binadamu na utawala wa kidemokrasia lakini kila nchi inaongozwa na utekelezaji wake, ile uniqueness (upekee) wa nchi, kwa hivi sidhani kwamba tukiwa na msimamo huo tukakosa wafadhili si kweli wao wanatuhitaji na sisi tunawahitaji na mataifa yote yanahitajiana, hawawezi kufikia malengo yao bila sisi na sisi hatuwezi kufikia malengo yetu bila wao.

Raia Mwema: Kwa mantiki hiyo unauzungumziaaje uamuzi wa Baraza la Changamoto za Millenia (MCC) kuikatia Tanzania misaada, uliofikiwa hivi karibuni?
Dk. Kitima: Tanzania ni kati ya nchi ambazo ziko kwenye harakati za kuendelea, ni nchi inayoendelea, katika kuwa hivyo inahitaji ushirikiano na nchi zilizoendelea. Kwa sababu kiuchumi nchi zilizoendelea na zinazoendelea, kwa mfumo wa uchumi tuliounda, umefanya kila nchi inayohitaji kuendeea kutakiwa kushirikianana wenzake, tunapata uhalali wa kusaidiana na kushirikiana, siyo kwamba tunashirikiana kwa sababu hatuna mahali pa kushika, hapana, tuna uhalali kwa sababu haya mataifa makubwa yaliyoendelea bado yananeemeka kutokana na rasilimali za dunia nzima, zikiwemo za Tanzania. Uhalali wa kushirikiani unatokana na mfumo wa uchumi tangu baada ya mapinduzi ya viwanda. Kwa hiyo huo msaada wa MCC una uhalali wake kutokana na matakwa ya kushirikiana. 

Lakini pia kujitoa katika kutupatia msaada huo kunaleta changamoto kwa pande zote, Tanzania na Marekani, kwamba labda wao wana masharti yao na sisi kama nchi huru tuna masharti na taratibu zetu, kushirikiana hakumaanishi nchi moja iwe mtumwa wa nchi nyingine bali kunatakiwa kuheshimiana kati ya nchi zote mbili, mmoja anapofanya maamuzi yake kadiri anavyojisikia bila kuangalia walichokubaliana mwanzoni na vile vile bila kuzingatia uhuru wa nchi katika kuamua mambo yake, kunaleta changamoto katika uhusiano. Sisi kama Watanznaia tunapaswa kusimama na kuangalia kwamba kwenda kinyume na uhuru wetu wa kujiamuria mambo kulinganisha na maamuzi ambayo wanaweza kuyafanya, la msingi ni kuzingatia kwamba hatupaswi kuwa watumwa katika misimamo yao ambayo huenda haitusaidii katika kusonga mbele, hasa ukizingatia mtazamo wa serikali ya sasa kujenga taifa la viwanda na katika kujenga viwanda tunategemea pia tutunze tunu za amani na umoja na mashikamano wa taifa, kama tunaweza tukaheshimu hilo na hilo likalindwa kwa namna yetu, kwa sababu tangu tupate uhuru tumejenga taifa hili kwa namna yetu, hatukuongozwa na mtu mwingine tulijiamuria sisi wenyewe hali iliyosababisha tukajikuta katika nyakati ambazo baadhi ya mataifa yalijitenga na sisi kutokana na misimamo yetu, na nchi ambazo daima zimekuwa zikituyumbisha ni hizi ambazo hazielewi namna yetu ya kulinda umoja na amani ya nchi yetu, hizi wakati mwingine zinatugharimu. Lakini sisi tunaona hizi ni tunu kubwa ambazo hatupaswi kujinyeyekesha kwa mtu tukaziweka chini ili tu tupate fedha, utu wetu na tunu zetu kama taifa ziko juu ya fedha yoyote ile.
Raia Mwema: Ukisema hivyo MCC waliweka wazi sababu za kusitisha msaada wao, ikiwemo kutoridhishwa na namna tunavyoshughulikia suala la Uchaguzi wa Zanzibar na sheria ya makosa ya mtandao, kwa mtazamo wako unadhani mambo haya yako sawa kiasi kwamba kuyafanya vigezo vya kuzuia msaada wao ni kupuuza utu na uhuru wetu kama taifa?

Dk. Kitima: Uchaguzi ni kitendo cha kuweka Serikali madarakani kwa kuzingatia sheria zilizowekwa, inapoonekana kwamba nchi inaona utaratibu haukufuatwa vizuri, sheria zinaongoza au kama mtu anasusia sheria inasemaje katika kususia. Kwa sababu ukiangalia walielezwa wote wakapige kura sasa kama kuna wengine walisusia hilo ni tatizo ambalo sisi wenyewe kama taifa tutaona tulitatuaje, wao kuondoa msaada huu kwa sababu watu wengi hawakushiriki uchaguzi ule ilibidi watuulize tuna mkakati gani ili ambao hawakushiriki watapata haki zao za kidemokrasia katika kujitawala. Hilo lilifanyika na tulitoa jibu gani? Mimi sioni kama lilifanyika.

 Kwa sababu suala siyo kushinikiza tu kwamba hawa hawakushiriki, halafu wao hawapaswi kutupangia sisi kama nchi huru namna gani tushughulikie matatizo yote ya kidemokrasia ndani ya nchi yetu, sisi tuna sheria zinazooongoza demokrasia na hakuna demokrasia ambayo ina ukamilifu, kila demokrasia ya nchi yoyote ile ina upekee wake, inategemea mazingira ya nchi husika ndiyo maana tuna demokrasia za aina mbali mbali na demokrasia ya Magharibi haina maana ndiyo mfano wa demokrasia bora duniani, ziko za aina mbali mbali na Tanzania tuna demokrasia yetu kwa sababu tunaongozwa na utawala wa watu kwa manufaa ya watu na sisi manufaa yetu tunyayaweka kwenye maendeleo yetu bila kuchezea amani na umoja wetu, sasa kama misaada ya maendeleo itatufanya tukose vitu ambavyo sisi tunaona ni tunu zetu hilo shinikizo hatuko tayari kulipokea.

Raia Mwema: Kwa kusema hivyo unaamini uchaguzi wa Zanzibar ni kiini macho tu na kwamba kuna agenda iliyojificha katika hili?

Dk.Kitima: Ni ngumu kuelewa kuelewa sababu zao halisi, lakini ninavyoelewa wao wana kanuni zao za kidemokrasia ambazo zikikiukwa wanakuwa hawaumi maneno, lakini suala linakuja demokrasia yao ni yao lazima wakubali tofauti, wao wana mambo yao ambayo wanayafanya, kwa mfano, wanapotetea au kulinda masharti ya raia wao katika nchi mbali mbali wamekuwa wakikiuka kanuni za Umoja wa Mataifa, lakini kwa sababu wao wana uwezo wa kujitegemea wanafanya tu, sisi pia tuna uhuru wa kujiamuria vitu vyetu kama tunaona kwamba uamuzi tunaofanya ni kwa maslahi ya mapana zaidi ya taifa na yatawafaa watu wengi zaidi na vitu vingine vina gharama kubwa tusipovipa kipaumbele tunaingia kwenye matatizo makubwa zaidi, kwa hiyo suala ni kwamba wao wana namna yao ya kuendesha demokrasia ya uchaguzi lakini vile vile lazima waelewe pia kwamba sisi tuna mtazamo wetu na namna ya kujitawala kwa kadiri Tanzania tulivyo. Sisi ni nchi ambayo tuliamua kutofungamana na upande wowote, hakuna mtu anapaswa kutuwekea sisi masharti ya namna tunavyopaswa kujitawala. 

Chanzo. Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates