Social Icons

Saturday, 30 April 2016

Hivi bado tunawahitaji viongozi wa Serikali za Mitaa?


SERIKALI za Mitaa zimekuwa zinalalamikiwa na wananchi wengi wa Tanzania kwa kutowajibika ipasavyo na utoaji huduma zisizoridhisha zikiwa ni pamoja na elimu, maji, barabara, afya, usafi wa mazingira, ulinzi na usalama.

Serikali hizo zilianza kufanya kazi nchini mwaka 1984 kwa lengo la kuwashirikisha wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo ili kuinua ustawi wao na uchumi wa Taifa  kwa jumla.

Serikali hizo zimeundwa katika mifumo mbalimbali ya Halmashauri. Kuna Halmashauri za Majiji, za Manispaa, za Wilaya na za Miji.

Hivi sasa kuna jumla ya halmashauri 168, kati ya hizo katika majiji kuna  halmashauri tano  -  Dar es Salaam, Tanga, Mbeya, Arusha na Mwanza; na kuna manispaa 18 baadhi yao ni Ilala, Kinondoni, Temeke, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Morogoro, Shinyanga na Tabora. Zilizobakia ni halmashauri za wilaya 132 na za miji 13.

Mfumo wa Serikali za Mitaa ulikuwapo kabla Tanganyika haijapata Uhuru mwaka 1961. Mfumo huo ulianzishwa mwaka 1926 wakati nchi ikiwa koloni la Waingereza na uliendelea hadi mwaka 1972.

Wakati huo, watu wengi walifurahia huduma zilizokuwa zikitolewa na serikali hizo, hasa kuanzia kipindi cha uhuru hadi zilipovunjwa mwaka 1972.

Huduma bora ambazo wananchi wanakumbuka walinufaika nazo katika kipindi hicho ni pamoja na za afya, mitaro ya maji machafu, barababara, tiba za mifugo na usafi wa mazingira.

Kwa mfano, kuhusu afya, hospitali zilitoa huduma bora, watumishi wa hospitali walizingatia maadili, kulikuwa na dawa za kutosha, magari ya wagonjwa yalikuwa tayari muda wote kutoa huduma; kulikuwa na ratiba maalumu za kupulizia dawa za kuua mbu na wadudu wengine hatari kwenye nyumba za kuishi, vyoo, mitaro, madimbwi na kadhalika.

Kuhusu mazingira, miji ilikuwa safi. Ilijengwa kwa mpangilio, mitaa ilipewa majina, kulikuwa na maeneo ya kutupia takataka na takataka, kulikuwa mitaro  ya maji machafu, na barabara za mitaani zilipitika kwa urahisi majira yote kwa kukarabatiwa mara kwa mara.

Kuhusu mandhari ya miji, ilikuwa ya kupendeza kwelikweli. Kulikuwa na taa za umeme za mitaani,  bustani za mapumziko zenye maua na miti ya kivuli zilizohudumiwa kila mara,  mabango ya majina ya mitaa kila mahali, barabara zilizopandwa miti kando, vibanda vya kupumzikia wasafiri katika stendi za mabasi na kadhalika.

Mwaka 1964, Tangayika iliungana na Zanzibar na jina la nchi kubadilika na kuwa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Upande mmoja ukiitwa Tanzania Bara na wa pili Tanzania Visiwani.

Serikali  ya Tanzania Bara  iliondoa mfumo wa Serikali za Mitaa mwaka 1972,  ikatwaa madaraka yote ya utawala na kuasisi mfumo wa “Madaraka Mikoani”. Lakini ilipoona mfumo huo umeshindwa kuwafikia walio wengi vijijini, mwaka 1982 aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Sokoine akaanzisha mchakato wa kugatua madaraka kwa wananchi kwa kurejesha serikali za mitaa.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ukafanyika mwaka 1983 na mwaka uliofuata zikaundwa halmashauri kuashiria kuanzishwa tena kwa Serikali za Mitaa nchini.

Madhumuni ya kuwapo kwa Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi na serikali hizo zitakuwa na haki na mamlaka ya kuwashirikisha wananchi katika mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao na nchi kwa jumla.

Serikali hizo zimepewa majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusimamia sheria, usalama na utawala bora;  kuandaa vipaumbele na mipango katika kuinua ubora wa huduma kwa wananchi kama vile elimu, afya, maji, nishati, miundombinu na huduma nyingine muhimu kwa jamii.

Majukumu mengine ni kufuatilia utekelezaji wa kila sekta kama vile kilimo, ardhi, nishati, maji na mawasiliano ili kuhakikisha ubora wa huduma za jamii.

Vilevile serikali hizo zinapaswa kujua chanzo cha mapato, kusimamia matumizi ya mapato,  na kuwapa wananchi nafasi ya kushiriki na kutoa maamuzi kuhusu shughuli mbalimbali za maendeleo.

Serikali za Mitaa pia zinatakiwa kuwahamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii na kwa kujituma ili kupambana na umasikini.

Mwaka 1993 mfumo wa chama kimoja uliondolewa na nchi ikawa na demokrasia ya vyama vingi vya siasa. Mpaka sasa Tanzania ina vyama 22 vya siasa, na uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi ukafanyika mwaka 1995. Tangu wakati huo chama tawala – CCM – kimekuwapo madarakani.

Kufuatia kuanzishwa kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, yalifanyika mageuzi makubwa katika sekta ya umma ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu ya mageuzi ya serikali za mitaa – Local Government Reform Programme.  Programu hiyo ikingali katika mchakato wa utekelezaji ikilenga kuboresha zaidi utendaji wa serikali za mitaa.

 Sasa ni miaka 30 tangu kuanzishwa tena kwa mfumo wa serikali za mitaa. Hata hivyo, baada ya kurejeshwa mfumo huo, utendaji sasa umetofautiana kabisa na ule wa zamani. Wananchi wamekuwa wakizilalamikia serikali hizo kwa utendaji dhaifu na ufisidi wa rasilimali pesa.

Pamoja na majukumu mazuri na ya kutia matumaini ya Serikali za Mitaa, ni ukweli ulio bayana kwamba mengi ya majukumu hayo yamebakia katika maandishi tu bila utekelezaji.

Ni wananchi wachache walio mijini na vijijini wanaojua kwa kina majukumu ya Serikali za Mitaa. Sana sana Serikali za Mitaa zitaonekana kupambana na wafanya biashara ndogo ndogo wajulikanao kama “Wamachinga” wanaofanyia biashara katika maeneo yaliyopigwa marufuku, kugawa viwanja vya ujenzi, kutoa leseni za biashara, kushughulikia migogoro ya ardhi, na kadhalika.

Lakini huduma kama maji, ukarabati wa barabara za mitaani, usafi wa mazingira, na tiba ya mifugo hufanywa na wananchi wenyewe kwa kujitegemea au kujitolea bila ushiriki au msaada wa watendaji wa Serikali za Mitaa.

Huduma za Serikali za Mitaa pia ni duni. Katika sekta ya afya, kwa mfano,  wananchi wanawalalamikia wahudumu wa afya kwa lugha chafu, ukosefu wa dawa na rushwa. Masuala kama uchafu wa mitaani na mazalia ya mbu hayashughulikiwi badala yake watakuja watu binafsi kufanya kazi hiyo na kutoza pesa na mradi huu utasemekana ni wa baadhi ya watendaji wa Serikali za Mitaa au watu wanaohusiana nao.

Katika sekta ya elimu, kuna ukosefu wa sare za wanafunzi katika shule za msingi, kuna tatizo la kutopata chakula kwa wanafunzi wa shule nyingi, pia kuna tatizo kubwa la upungufu wa madawati; na majengo ya shule hayakidhi viwango licha ya kutolewa pesa ya kutosha kwa ujenzi.

Kwa mfano, inakisiwa kwamba katika shule za msingi zilizoko katika Serikali za Miji na Vijiji nchini Tanzania, kuna upungufu wa madawati 3,302,678; yaliyopo ni 1,837,783 tu.  Pia shule hizo na zile za sekondari zina upungufu wa matundu ya vyoo.

Kuhusu mazingira, katika baadhi ya majiji na miji, kwa mfano, ni machafu, hakuna madampo ya takataka, zinatupwa ovyo; hakuna huduma ya magari ya kunyonya maji kwenye chemba za vyoo, hakuna huduma ya kupulizia mbu na wadudu wengine hatari katika makazi ya watu na kadhalika.

Kuhusu maendeleo katika baadhi ya manispaa, masoko, pamoja na kutokuwa na vyoo, yamejengwa na wananchi wenyewe kwa miti, mbao, maturubali au mabati chakavu badala ya kujengwa kisasa na Serikali za Mitaa. Lakini bila soni wafanyakazi wa halmashauri huingia ndani ya masoko hayo kutoza ushuru.

Pesa hiyo ni kwa huduma gani? Barabara za mitaani ni mbovu na hakuna anayejali kuzifanyia ukarabati, pia hakuna taa kando ya barabara na stendi za mabasi hazina vyoo.

Ni nadra kwa watendaji wa Serikali za Mitaa kuitisha mikutano kujadiliana na wananchi kuhusu kero za maeneo yao na ufumbuzi wake.

Kuhusu ulinzi na usalama, kuna migogoro isiyoisha katika maeneo ya Serikali za Mitaa. Kuna migogoro inayotokana na mipaka kati ya wananchi na hifadhi, wananchi na wawekezaji, wakulima na wafugaji.  Pia kuna maeneo ambayo yameonesha dalili za migogoro ya kidini, kikabila na ubaguzi kwa misingi ya dini.

Kuhusu viwanja, kuna uchelewaji wa kupima viwanja au kuchelewesha kutoa vibali vya ujenzi, hali inayosababisha ujenzi holela katika majiji, miji na manispaa.

Aidha watendaji wa halmashauri wanalaumiwa kwa kufisidi rasilimali pesa. Kuna vikao vingi visivyokuwa vya lazima vinavyoitishwa maofisini kujadili shughuli za maendeleo lengo lake kubwa likiwa kujipatia posho tu.

Pia vitendo vya wizi, uzembe na ufisidi wa fedha za umma vimelalamikiwa kukithiri katika halmashauri mbalimbali. Kwa mujibu wa taarifa ya  Ofisi ya Waziri Mkuu, hadi kufikia katikati ya mwaka 2014, wakurugenzi watano wa halmashauri za jiji la Arusha, na  wilaya za Ileje, Maswa, Ikungi na Momba, walifukuzwa kazi kwa makosa hayo.

Kutokana na makosa hayo, pia Mkurugenzi wa Wilaya ya Kaliua alipewa onyo, wakuu watatu wa idara walivuliwa madaraka, na watumishi saba wa halmashauri za Arusha, Maswa, Masasi na Bukombe walifukuzwa kazi na wengine waliteremshwa vyeo.

 Pia watumishi 13 wa halmashauri za Bunda, Kyela, Mafia, Mpanda na Bukombe wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na kesi zinazohusiana na wizi, rushwa, mauaji, na ubadhirifu. Kesi zao zingali zikiendelea.

Baadhi ya wabunge - ambao ni wajumbe wa kamati za maendeleo katika serikali za mitaa - na madiwani nao wamedaiwa kukwepa kukutana na wananchi kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za maendeleo au kujua na kutafuta ufumbuzi wa kero zao.

 Akifunga mkutano wa 30 wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT) uliofanyika mjini Tanga hivi karibuni, Waziri Mkuu, Mizengo  Pinda, alisema pamoja na hatua zilizochukuliwa kuondoa mapungufu katika Serikali za Mitaa, bado kuna changamoto na kero katika serikali hizo. Changamoto hizi zinahusiana na utoaji wa huduma na uendeshaji wa halmashauri kwa ujumla, alisema.

“Tatizo kubwa ninaloliona katika halmashauri zetu ni kutokuwapo kwa uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali fedha zinazotolewa na pia kutokusimamiwa ipasavyo miradi inayotekelezwa ndani ya halmashauri hizo,” alisema Pinda.

Ni matarajio ya wananchi kwamba  matamshi hayo ya waziri mkuu hayatakuwa ya kisiasa tu bali yatafuatiwa na kuchukuliwa kwa hatua za dhati kuwawajibisha watendaji wabovu katika halmashauri ili kuboresha huduma za halmashauri hizo ambazo zinategemewa na Watanzania walio wengi.

Chanzo. Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates