Social Icons

Saturday 30 April 2016

Serikali za Mitaa ni kitu gani?



MAKALA yangu ya wiki iliyopita nilijadili juu ya serikali za mitaa. Nilifanya hivyo kwa sababu kulikuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na kulikuwa na taarifa kwamba  watu wachache walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo.

Uchaguzi umefanyika huku kukiwa na  malalamiko kwamba haukuwa huru. CCM tayari inatamba kwamba imeshinda kwa kishindo na wala haikerwi na idadi ndogo iliyojitokeza kupiga kura.

Kwa kuzingatia yote hayo, naendelea wiki hii kulijadili suala hilo hilo: Serikali za Mitaa ni kitu gani?


Baada ya kuzifuta Serikali za Mitaa mwaka 1972, Serikali Kuu ilianzisha utaratibu wa Madaraka Mikoani. Madaraka Mikoani ilikuwa na maana ya uhamishaji wa mamlaka kutoka makao makuu ya serikali na kuwapa maafisa wake katika ofisi za mikoani.


Sababu ya utaratibu huo ilikuwa ni kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi, na pia kuongeza nguvu na madaraka ya wawakilishi wao.

Utaratibu huu ulipokelewa kwa hisia tofauti. Kwanza, haikuwa rahisi kuona uwezekano wa nguvu na madaraka ya wawakilishi wa wananchi yakiongezeka juu ya watendaji wao ambao hawakuwa na uwezo wa kuwaajiri.


Baadhi ya maofisa walikuwa na madaraka makubwa na pia mishahara mikubwa. Kwa mfano, Mkurugenzi wa Mkoa (RDD) alilinganishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ambapo Afisa Mipango, Afisa Utumishi na Mdhibiti wa Fedha nao walipewa mishahara mikubwa. Hali hii ilisababisha manung’uniko kwa baadhi ya watendaji wa mikoani na wilayani.


Kutokana na maandalizi hafifu, watendaji waliteuliwa haraka haraka bila ya kuzingatia sifa zao kwa makini. Wengi waliandaliwa kupitia semina fupi za wiki moja au mbili. Kwa bahati mbaya, wengi wa watendaji wa halmashauri zilizovunjwa hawakuajiriwa katika utaratibu wa Madaraka Mikoani.


Kwa maana hiyo, dosari katika utendaji ziliweza kuonekana tangu awali. Kwa mfano, katika sehemu nyingi hati za makabidhiano hazikutayarishwa na pale zilipotayarishwa, watendaji wa Madaraka Mikoani hawakuzifuatilia. Hali hii ilisababisha upotevu wa mali na fedha nyingi za Serikali.


Kwa sababu madaraka yalibakia zaidi mikononi mwa watendaji  wakuu, hali ya utoaji huduma za jamii ilizorota. Utekelezaji wa Mpango wa Vijiji vya Ujamaa uliotekelezwa kati ya mwaka 1972 na 1975, chini ya Madaraka Mikoani, ulikuwa na kasoro nyingi.


Aidha, Mpango wa Elimu kwa wote (UPE) nao pia ulikuwa na matatizo pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kutaka kila mtoto aliyefikia umri wa kuingia shule ya msingi afanye hivyo.

Kwa ujumla, kipindi cha Madaraka Mikoani hakikuwa na mafanikio mengi katika kuleta maendeleo. Ni katika kipindi hiki nchi ilishuhudia kupungua kwa uzalishaji katika kilimo, na pia kushuka kwa viwango vya elimu katika shule zetu za msingi, sekondari na hata vyuoni. Aidha, hali ya usafi mijini ilizorota.


Chini ya utaratibu wa Madaraka Mikoani, wananchi hawakuwa wakishirikishwa katika taratibu za maamuzi. Hali hii ilisababisha wananchi kuitegemea Serikali ifanye kila jambo. Uwezo wa Serikali ulikuwa mdogo. Kwa hiyo, matokeo yake yalikuwa ni kudidimia kwa uchumi na kushuka kwa viwango vya maisha ya wananchi. Hali hii ilifanya serikali kufikiria upya umuhimu wa kuwepo kwa Serikali za Mitaa ili kuwawezesha wananchi kujiamulia mambo yao wenyewe bila ya kutegemea Serikali Kuu kuwafanyika kila kitu.


Mnamo mwaka 1978 Serikali iliamua kuzirejesha madarakani Serikali za Mitaa katika maeneo ya mijini. Hii ilitokana na ushauri wa kitaalamu wa mshauri wa Umoja wa Mataifa na taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu baada ya kuchunguza tatizo la mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu uliotokea mwaka 1976.


Sheria Na.11 ya 1978 ilizirejesha Serikali za Mitaa Mijini bila ya kutoa mamlaka kwa Halmashauri hizo kutumia mapato zilizokuwa zinakusanya. Kutokana na hali hiyo, Halmashauri hizo hazikuweza kuleta mabadiliko ya msingi katika utoaji wa huduma za jamii mijini.


Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1980, na kutokana na ushauri wa wataalamu walioteuliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Miswada mitano iliandaliwa kuhusu Serikali za Mitaa na kuwasilishwa Bungeni.

Miswada hiyo ni: Sheria Na. 7 ya Halmashauri za Wilaya, Sheria Na. 8 ya  Halmashauri za Miji, Sheria Na. 9 ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sheria Na.10 ya Utumishi katika Serikali za mitaa na Sheria Na.11 ya Usuluhishi katika Serikali za mitaa.


 Bunge lilipitisha sheria hizo tano Aprili 1982. Sheria hizo zilihalalisha kuundwa kwa mfumo kamili wa Serikali za Mitaa nchini, lakini kutokana na maandalizi mbalimbali yaliyohitajika kutimizwa, urejeshaji wa Serikali za Mitaa nchini ulianza kutekelezwa mwaka 1984.


Kimsingi, Sheria hizi zilifuta Sheria ya muda Nambari 11 ya mwaka 1978 ya Halmashauri za Miji. Kwa mujibu wa Sheria hizi ambazo zililenga kupeleka madaraka kwenye ngazi za chini za Serikali za Mitaa ili kuzingatia demokrasia shirikishi, Halmashauri zilipewa madaraka ya kuajiri watendaji wake, kupanga bajeti, zake na kutoza kodi na ushuru katika maeneo yako. Sheria hizo vile vile ziliwakataza watendaji wa Halmashauri kupiga kura kwenye vikao vya  Halmashauri ingawaje haki yao ya kuhudhuria na kushiriki kwenye majadiliano ya vikao ilibakizwa. Msimamo huu ulikuwa na maana kuwa katika Halmashauri maamuzi hufanywa na madiwani tu.


Sheria hizo pia zilitengua utaratibu wa Mwenyekiti wa Chama Tawala kuwa pia Mwenyekiti wa Halmashauri. Kuanzia kipindi hicho Mwenyekiti wa Halmashauri alichaguliwa miongoni mwa madiwani wa kuchaguliwa kwenye kikao chao cha kwanza cha Halmashauri.


Kutokana na uamuzi huo wa Serikali, na ili kuepuka mapungufu ya Serikali za Mitaa ya miaka ya nyuma, vuguvugu la kuwatayarisha watendaji wa Halmashauri ilianza miaka ya 1984. 


Katika kipindi hicho, semina mbalimbali ziliendeshwa nchini. Watumishi wengi walipelekwa masomoni ili kuhakikisha Halmashauri zinaendeshwa na watu wenye ujuzi. Ni kwa mantiki hiyo utaratibu wa kuwepo kwa mafunzo kwa waheshimiwa madiwani uliandaliwa na kutekelezwa ili kuwapa  upeo zaidi kuhusu wajibu na majukumu yao.


Hata baada ya kurejeshwa rasmi Serikali za Mitaa mwaka 1984, bado Serikali hizo za Mitaa ziliendelea kukabiliwa na matatizo kama haya yafuatayo :-


Matatizo ya kimfumo na kisheria; Utaratibu wa mfumo wa kisheria uliotoa mwanya kwa mwingiliano na migongano ya Sheria. Nyaraka; kanuni za kudumu na taratibu zilizotungwa chini ya sheria hizo.


 Matatizo yahusuyo majukumu, kazi na miundo; Halmashauri zilikuwa na mpangilio wa majukumu, kazi na miundo iliyofanana bila kujali hali halisi ilivyo baina ya Halmashauri. Aidha, Halmashauri zilikuwa na uwezo mdogo wa kuzishirikisha ngazi za chini za utawala na hivyo zilihodhi madaraka katika ngazi ya wilaya/mji na kuziacha hizo ngazi za chini bila madaraka makubwa.


 Matatizo yaliyotokana na mfumo wa utawala; Kulikuwa na uhusiano dhaifu kati ya viongozi wa kisiasa wa ngazi mbalimbali, watendaji, vikundi mbalimbali yaliyoishia kwenye malumbano na kuzorotesha utoaji wa huduma.


 Matatizo yaliyotokana na fedha; Serikali za Mitaa ziliendelea kukabiliwa na upungufu wa fedha ikilinganishwa na majukumu yao; idadi ya watumishi waliokuwa nao na viwango vya huduma vilivyotegemewa kutolewa :


Halimashauri ziliachiwa vyanzo vya mapato visivyotoa mapato ya kutosha na ukusanyaji wake ulikuwa mgumu; Viwango vya ruzuku vilivyokuwa vinatolewa kwa Halmashauri havikuwa vya uhakika na vilikua havitabiriki; Ukusanyaji wa mapato yao uliendelea kuwa duni ukifanywa na watendaji wasio na ujuzi wa kutosha wa kazi hiyo.


Matatizo ya utumishi na uendeshaji ;Watumishi walio wengi waliendelea kuajiriwa na kuwajibika kwa Wizara Mama badala ya kuajiriwa na kuwajibika kwa  Halmashauri. Hivyo Halmashauri zilishindwa kuwasimamia ipasavyo; Halmashauri ziliendelea kukabiliwa na uhaba mkubwa wa watumishi wenye ujuzi na uzoefu unaotakiwa.


Hali hii iliathiri kwa kiasi kikubwa ubora wa huduma zilizokuwa zinatolewa kwa wananchi; Halmashauri ziliendelea kukosa fedha za kutosha ili kuwafunza watumishi wa Serikali za Mitaa.


Matatizo yaliyotokana na umaskini uliokithiri kwa wananchi; Hali duni ya wananchi iliendelea kuwafanya wananchi washindwe kuchangia katika maendeleo ya  Halmashauri yao.

Matatizo ya Uadilifu; Ukosefu wa uadilifu uliwakumba viongozi walio wengi wa kuchaguliwa na utendaji kiasi cha kuzidisha uzito wa matatizo na kuzaa rushwa.


Tatizo la uhusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa; Kutozingatiwa kwa mipaka ya kazi zao katika maeneo mbalimbali; Kuendelea kwa uhusiano wa uhimili badala ya ule wa uwezeshaji.

Kutokana na mapungufu hayo yaliyoorodheshwa hapo juu na mengine mengi, baada ya Halmashauri kurejeshwa mwaka 1984 na mabadiliko mengi ya kisiasa na kiuchumi, Serikali kuanzia miaka ya 1990 ilianza kuandaa Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa. Utekelezaji wa mpango huu ulianza rasmi mwaka 2000.


Kwa kutambua athari na matatizo ya mfumo uliokuwepo wa Serikali za Mitaa, Chama cha Mapinduzi katika Ilani zake za Uchaguzi za mwaka 1995, 2000 na 2005 kimeeleza wazi azma yake ya kuziimarisha Serikali za Mitaa ili ziweze kuwa  vyombo madhubuti vya kutoa huduma bora kwa wananchi na kukuza demokrasia na uwajibikaji kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya wananchi kwenye maeneo yao.


Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau wakuu walikubaliana kuhusu taswira ya uboreshaji wa mfumo wa Serikali za Mitaa ambayo iliidhinishwa kama agenda ya kuboresha mfumo wa Serikali za Mitaa ya mwaka 1996-2000.


Mpango wa  uboreshaji wa mfumo wa Serikali za Mitaa uliandaliwa na kuidhinishwa na serikali mwaka 1998 ili kuimarisha mfumo wa Serikali za Mitaa ambao ungeziwezesha Serikali za Mitaa kutekeleza masharti ya utawala bora unaozingatia uwajibikaji, uwazi, demokrasia na ushirikishwaji wa umma na hivyo kuinua ubora na kiwango cha utoaji wa huduma kwa wananchi wote na, hasa walio maskini.


Vile vile, Serikali iliidhinisha Mkakati wa Upelekaji Madaraka, Majukumu na Raslimali kwa wananchi (decentralization by devolution) kupitia Serikali za Mitaa ambao ndio unaotumika katika kutekeleza maboresho yanayohitajika katika mfumo uliopo  wa Serikali za Mitaa.


Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa ulianza kutekelezwa rasmi mwezi Januari, 2000 katika Halmashauri 38 za awamu ya kwanza. Katika tathmini ya utekelezaji wa mpango huo ambayo ilifanyika mwaka 2001, pamoja na mambo mengine, ilishauriwa kuwa mpango utekelezwe nchi nzima kwa yale mambo ambayo hayakuihitaji matumizi ya fedha nyingi; na mambo mengine ambayo yalihitaji utafiti na fedha nyingi yatekelezwe hatua kwa hatua. 


Mpango ulitekelezwa katika Halmashauri zote 114 na utekelezaji wa mpango huu ulikwenda  sambamba na utekelezaji wa Mpango wa Uboreshaji wa Utendaji Serikalini (PSRP) ambao una upeo unaoishia mwaka 2011.


Lengo kuu la Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa ni kupunguza idadi ya Watanzania waishio katika umaskini kwa kuboresha wingi na ubora wa huduma zitolewazo kwa wananchi na hasa wale walio maskini.


Hivyo serikali za mitaa ni chombo muhimu sana, ni lazima tuwahimize watu kukiheshimu na kukubali kupiga kura.

mwandishi. Privatus Karugendo.


No comments:

 
 
Blogger Templates