Social Icons

Friday, 20 May 2016

Hadithi. KIUMBE WA USIKU. 4


Akiwa katika usingizi mzito alishtushwa na hodi, alisimama kivivuvivu na kuufungua mlango. Alikuwa ni shoga yake Batuli, aliyeingia akiwa ananuka pombe. Inawezekana ikawa ni ofa za wanaume zake wa baa.
Kitu cha kwanza alichogundua Batuli mara baada ya kuingia mle ndani ilikuwa ni vile vitambulisho  vya Joy kwenye dressin tebo, akavichukua na kuanza kuviangalia na kuguna.
“Joy huyu nani?” aliuliza Batuli na sauti yake ya kilevi huku akikagua ile waleti.
“simjui,” alijibu Joy akiwa bado na usingizi mzito.
“danga nini shosti? tena anaonekana mtu wa ofisini,” alisema Batuli, alikuwa kidogo hawezi kusoma vizuri kutokana na kuishia darasa la tano, laiti angejua angegundua ni mtu wa benki.
“hahaa danga shoga,” alidanganya Joy na kumficha shoga yake.
“Mh lakini siyo vizuri shoga, inabidi mnitambulishe bwana,”aliongea Batuli kiasi cha kumboa Joy aliyekuwa bado anatamani kulala.
“Sasa ilikuwaje mpaka akasahau vitambulisho!” alizidi kuhoji Batuli kiasi cha Joy kuinuka na kumpokonya Batuli vile vitambulisho na kuviweka ndani ya pochi yake, akiazimia kuvichoma moto mara baada ya kuamka maana hakutaka ushahidi wa vile vitu ili asije akagundulika bure kama alimuibia pochi kaka wa watu.
Japo jua lilikuwa tayari limechomoza na hiyo ikionekana kuwa tayari ni saa 3 asubuhi lakini viumbe hawa wawili ndiyo kwanza walikuwa wakikoroma, wakilipiza usingizi wa jana yake ambao waliukeshea, lakini kwa Joy huenda akawa analipiza usingizi aliohifadhi kuanzia siku za nyuma maana jana yake hakukesha kwa bahati aliyoipata.

Mara nyingi huwa ni njaa peke yake ambayo huwaamsha la sivyo wangeweza kulala mpaka jua lizame ndiyo waende makazini kwao.
Wa kwanza kuamka alikuwa ni Joy ambaye alianza kwa kutazama saa yake kwenye simu yake tena kwa jicho moja kama vile alikuwa hataki kuamka. Alishtuka baada ya kugundua ilikuwa ni saa 10 jioni.
Akasimama na kwenda chooni, akaoga na kurudi tena chumbani. Hapo akavaa dela lake na kutoka nje akielekea kwenye kibanda cha M-pesa maana alikumbuka alipaswa kutuma hela kijijini kwa ajili ya matumizi ya mtoto wake mdogo aliyemuacha kwa mama yake.
Aliingiza hela yote kwenye simu na kutuma shilingi elfu hamsini, akahakikisha tayari imefika kisha akaelekea baa kununua chipsi kuku na kuzila hapohapo baa kichoyo maana hakutaka rafiki yake Batuli amuombe.
Hiyo ilitokana pia na vita baridi waliokuwa nayo wawili hawa; Batuli hakutaka kujiuza, kila siku alikuwa akimshauri rafiki yake aachane na biashara hiyo, wakati huohuo Joy naye alikuwa akimshutumu mwenzake kuwa kazi yake ya baa ina umalaya ndani yake na mbaya zaidi haina hela ya kutosha.
Mara zote ubishi wao huishia kwa kila mmoja kusimamia upande wake.

Lakini ukweli ulibakia palepale kuwa pamoja na kasumba hiyo bado Batuli huwa ndiyo wa kwanza kumuomba Joy hela zake na suala hilo lilikuwa likimuuzi Joy ambaye aliona rafiki yake anamnyonya juhudi zake, si unajua tena kuvumilia purukushani za wanaume ambaye kila mmoja ana ukuni wake, halafu mwenzake anajifanya mlokole baridi, hata mimi nisingekubali kumpa chochote.
Kwa kisasi hicho, Joy alikula chipsi zake na kurudi chumbani,  akamkuta bado mwenzake amelala, akamkagua kwenye pochi yake akaona shilingi elfu 5 tu. Akajichekea kimyakimya na kujisemea kimoyomoyo; “Utakuja tu kujiuza kenge wewe.”
  ITAENDELEA WALA HAUTAKIWI KUIKOSA HATA KIDOGO

Chanzo. Fredynjeje

No comments:

 
 
Blogger Templates