Mwanasiasa machachari nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Moise Katumbi, anayetarajia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Novemba, amefunguliwa mashtaka ya kuhatarisha usalama wa Taifa
Kwenye taarifa iliyotolewa Alhamisi wiki hii, Moise (MOIZ) Chapwe Katumbi anashutumiwa kwa kutishia usalama wa taifa wa ndani na nje ya nchi, na anakabiliwa na waranti wa muda wa kukamatwa, Mwendesha mashitaka wa serikali amesema.
Tarehe mahsusi ya kusikilizwa kesi dhidi ya Katumbi, ambaye pia ni Milionea anayemiliki timu maarufu ya soka ya TP Mazembe ya mjini Lubumbashi na Gavana wa zamani wa jimbo lenye utajiri mkubwa wa madini la Katanga, bado haijapangwa.
Adhabu ya mashitaka kama hayo ni kifo, ambayo hata hivyo ilibadilishwa na kuwa kifungo cha maisha jela, tangu serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ilipoondoa adhabu hiyo,
Taarifa hizi zinakuja wakati ambapo kuna ongezeko la wasiwasi kutoka ndani na nje ya nchi hiyo kwamba Rais aliye madarakani, Joseph Kabila atachelewesha uchaguzi huo uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, wakati muhula wake wa miaka mitano utakuwa unakamilika.
Katumbi mwenye umri wa miaka 51, amekuwa hasimu namba moja wa Kabila katika kinyang'anyiro hicho cha urais, baada tu ya kutangaza nia yake ya kugombea nafasi hiyo dhidi ya kiongozi huyo wa nchi aliyehudumu kwa muda mrefu.
Mnamo tarehe 4 ya mwezi Mei, baada ya Katumbi kutangaza kuwania nafasi ya urais, mamlaka za kimahakama zilimfungulia madai ya kuwaajiri mamluki wa kigeni.
Katumbi aliwahi kuwa swahiba wa Kabila kisiasa
Katumbi alisema madai hayo, yaliyofuatiwa na kukamatwa kwa walinzi wake binafsi, ambao ni pamoja na raia wa Marekani ilikuwa ni hatua iliyoshinikizwa kisiasa.
Alipotakiwa kuzungumzia matamshi hayo ya Katumbi, msemaji wa serikali Lambert Mende ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, "anaweza kukutwa na kifungo cha nyumbani ama jela".
Msemaji wa karibu na Mfanyabiashara huyo Milionea, amesema Katumbi alikuwa akipata matibabu katika hospitali moja iliyopo kwenye mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Lubumbashi. Amesema alipigwa na polisi alipokuwa katika mahakama ya Lubumbashi Mei 13, baada ya kuzuka kwa makabiliano kati ya polisi na maelfu ya wanaomuunga mkono, alipokwenda kusikiliza kesi yake. Hata hivyo, polisi imekana madai hayo.
Taasisi ya kimataifa ya masuala ya haki za binadamu, Human Rights Watch imeyaita madai hayo kama "hatua dhidi ya mgombea huyo wa urais pamoja na wafuasi wake." Mjumbe maalumu wa Uingereza kwenye Ukanda wa Maziwa makuu Barani Afrika Danae Dholakia, amesema anatumaini madai hayo dhidi ya Katumbi, hayatokuwa ni kuongezwa kwa vizuizi vya uhuru wa kisiasa nchini humo. Kuna viashirio vingi vinavyotia wasiwasi, amesema Dholakia.
Wafuasi wa Kabila wanataka uchaguzi mkuu wa urais usogezwe mbele kwa miaka miwili kutokana na madai ya hali ngumu ya fedha na matatizo ya maandalizi.
Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman
Chanzo. Dw.de
No comments:
Post a Comment