Social Icons

Thursday 19 May 2016

Yanga mbele kwa mbele kimataifa

YANGA inaleta heshima kwa Watanzania. Pengine ndivyo unavyoweza kuzungumzia matokeo ya mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC), ambapo Yanga imeingia hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Imevuka licha ya kufungwa 1-0 na wenyeji wao, Sagrada Esperanca ya Angola katika mchezo uliofanyika katika mji wa Dundo.

Bao pekee la Waangola hao liliwekwa kimiani na mshambuliaji mkongwe mwenye umri wa miaka 37, lakini mahiri, Arsenio Sebastiao Cabungula `Love’ katika kipindi cha kwanza.

Yanga imenufaika na ushindi wa 2-0 ilioupata Mei 7 jijini Dar es Salaam kutokana na mabao ya Simon Msuva na Matheo Anthony, na hivyo kufuzu kwa jumla ya mabao 2-1.

Katika mchezo wa jana, Yanga ilicheza kwa nguvu zaidi karibu muda mwingi wa mchezo, ambapo washambuliaji wake wakiongozwa na Donald Ngoma walifika mara kadhaa langoni mwa wapinzani wao, lakini umaliziaji ulikuwa mbaya.

Dakika ya 90, kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ alipangua penalti iliyotolewa baada ya beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kumchezea madhambi mshambuliaji wa Sagrada.

Kwa kuingia hatua ya makundi Yanga imeandika historia mpya katika soka nchini kwa kuwa klabu ya kwanza Tanzania kufuzu hatua hiyo katika mashindano hayo, lakini ni mara ya pili kufuzu hatua ya makundi kwa mashindano makubwa Afrika baada ya kufanya hivyo mwaka 1998 katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ya Dar es Salaam nayo ilifuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 kwa kuitoa na kuivua ubingwa Zamalek ya Misri. Yanga imeangukia Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC), baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ililazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa mabao 2-1 Alexandria, Misri.

Ilizitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.

Kwa upande wao, Sagrada Esperanca katika Raundi ya Awali waliitoa Ajax Cape Town ya Afrika Kusini kwa mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani.

Katika raundi ya kwanza waliitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa mabao 2-1, ikishinda 1-0 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini na kwenda hatua ya 16 Bora, ambako waliitoa V.Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1 wakishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani.

Pamoja na Yanga katika hatua hii, timu nyingine zilizoingia na zimeshaanza kucheza mechi za mtoano – mbili, nyumbani na ugenini kabla ya nne kufuzu kwa hatua ya makundi zikichanganywa na zilizokuwamo ni Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Al-Merreikh ya Sudan.

Nyingine ni TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC); Etoile du Sahel ya Tunisia; Stade Malien ya Mali; Al-Ahli Tripoli ya Libya; MO Bejaia ya Algeria.

Kutokana na kusonga mbele huko na kuingia katika makundi, kama Yanga ikishika nafasi ya nne itavuna dola 150,000 (Sh milioni 315) huku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakilamba dola 15,000 (Sh milioni 31.5).

Wakishika nafasi ya tatu kwenye kundi wanachukua dola 239,000 (sh milioni 501) na TFF kupata dola 20,000 (Sh milioni 42).

Yanga hawa ambao kocha msaidizi ni Juma Mwambusi waliyemchukua Mbeya City baada ya Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ kwenda Taifa Stars wakishika nafasi ya pili kwenye kundi lao watapata dola 239,000 na shirikisho la Rais Jamal Malinzi yaani TFF linapata dola 25,000 (Sh milioni 52.5).

Yanga wakifika fainali; hata wasipolitwaa kombe basi watakuwa tayari mezani mwao wana dola 432,000 (Karibu Sh milioni 900) na TFF kupata dola 30,000 (Sh milioni 62) na ikiwa wanafunika bara zima kama Mlima Kilimanjaro ulivyo paa la Afrika, zao ni dola 625,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.3 za Tanzania) na TFF wanalamba dola 35,000 (zaidi ya Sh milioni 70).

Yanga; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko/ Deus Kaseke, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Kevin Yondan na Haruna Niyonzima.

No comments:

 
 
Blogger Templates