Mwandamanaji mmoja apigwa risasi mjini Kisumu. Shughuli za biashara, usafiri na masomo zimetatizwa katika mji huo kufuatia maandamano yanayoongozwa na upinzani CORD kushinikiza tume inayosimamia uchaguzi iundwe upya.
Mzozo kuhusu tume inayosimamia uchaguzi nchini Kenya IEBC umeendelea kutokota. Waandamanaji katika miji mbalimbali wameendeleza maandamano yao ya kila Jumatatu kushinikiza tume hiyo ivunjwe na iundwe upya, kama upinzani unavyosisitiza.
Katika mji wa Kisumu mtu mmoja amepigwa risasi na kukimbizwa katika hospitali. waandamanaji wamechoma matairi kwenye barabara hali ambayo imetatiza shughuli za usafiri. Katika jiji kuu la Nairobi waandamanaji wamejitokeza wakilenga kufika katika afisi za tume ya IEBC zilizoko katikati ya mji huo.
Mapema Jumatatu mahakama kuu ya Nairobi ilikataa kupiga marufuku maandamano hayo yanayoongozwa na muungano wa upinzani CORD. Mahakama hiyo ilisema maandamano yanakubalika kisheria na ni wajibu wa polisi kuhakikisha kuwa yanafanyika kwa amani. Baadhi ya wabunge wa chama kinachotawala Jubilee walitaka mahakama kuharamisha maandamano hayo.
Mkutano kati ya rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa Upinzani Raila Odinga katika Ikulu ya Nairobi wiki iliyopita haukuzaa matunda kuhusu namna ya kutatua mzozo huo.
Raila anasema walikubaliana kuunda jopo litakalojadili uundwaji upya wa tume hiyo. Lakini serikali inasema hawakukubaliana kuhusu kuundwa kwa jopo lolote, na kwamba mazungumzo kuhusu suala hilo sharti yafanywe kikatiba.
Makamishna wa tume hiyo (IEBC) wameshikilia msimamo kuwa hawatang'atuka, wakisema hawana hatia wala upendeleo, na hatua yoyote ya kuwatimua sharti ifuate sheria za kikatiba, ambayo ni kuwasilisha mswada bungeni ili kujadiliwa.
Hali ya usalama imeimarishwa huku idadi kubwa ya polisi ikishuhudiwa katika miji ya Nairobi, Kisumu na Mombasa. Katika maandamanao ya wiki zilizopita, kumetokea makabiliano makali kati ya polisi na waandamanaji. Waandamanaji watatu waliuawa katika miji ya Kisumu na Siaya, magharibi mwa Kenya baada ya kupigwa risasi na polisi. Polisi wamelaumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi.
Idara ya polisi ilionya kuwa italazimika kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji hao wakijaribu kutatiza shughuli katika makao makuu ya ofisi za IEBC.
Sikiliza ripoti za waandishi wetu hapo chini.
Mwandishi: John Juma
Mhariri: Iddi Ssessanga
Chanzo. Dw.de
No comments:
Post a Comment