Social Icons

Tuesday, 7 June 2016

Nyerere aligoma kukutana na Muhammad All

Makala: Nyerere agoma kukutana na Muhammad Ali

nyerer

Maziko ya bondia huyo mzungumzaji sana yatafanyika Ijumaa huko Louisville. Ali ambaye alisumbuliwa na maradhi kiharusi kwa miaka 32, alifariki duniani mjini Phoenix, Arizona, jioni ya Ijumaa iliyopita baada ya kulazwa tangu Jumatatu kwa matatizo ya kupumua.

Mazishi yake yatafanyika katika mji wa kwao Louisville, Kentucky, Ijumaa ijayo ambako bendera zimekuwa zikipeperushwa nusu mlingoti tangu kifo chake kilipotangazwa. Mwili wake utapitishwa Muhammad Ali Centre, utasafirishwa kupitia barabara ya Muhammad Ali Boulevard na utaishia katika makaburi ya Cave Hill kwa shughuli za maziko.

Wakati dunia ikiomboleza kifo cha gwiji huyo, miaka 36 iliyopita aliwahi kufanya ziara ya kuja Tanzania. Lakini, ziara yake hiyo haikuwa ya masuala ya masumbwi. Bondia Ali alikuja Tanzania kwa shughuli za kidiplomasia. Aliingizwa kwenye siasa za vita baridi zilizokuwa zikifanyika Afrika kwa wakati huo.

Ilikuwa Februari 2, 1980. Ali aliwasili Dar es Salaam katika ziara yake ya siku tatu kuishawishi Tanzania kugomea mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika Moscow mwaka 1980. Ali alipokewa kishujaa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Tovuti moja ya Kimarekani, Politico ilitoa ufafanuzi juu ya ziara ya bondia huyo katika makala yake iliyotoka Februari 2014.

Katika taarifa yake hiyo ya Politico, Ali alipokewa kwa shangwe na kelele za ‘Ali, Ali, Ali’ wakati alipokuwa akijiandaa kushuka kutoka kwenye ndege.
Nyerere agoma kukutana naye

Mbwembwe zote za kushangiliwa ziliishia uwanja wa ndege. Ziara yake hiyo ilishindwa kuzaa matunda. Si tu kwanza Tanzania iliamua kupuuzia mpango wa kugomea michezo ya Olimpiki, bali pia Mwalimu Julius Nyerere aligoma kukutana na bondia huyo licha ya jitihada nyingi zilizofanywa na ubalozi wa Marekani. Walipanga kumkukutanisha Mwalimu Nyerere na Ali uwanja wa ndege wakati akielekea Mwanza, lakini jaribio hilo lilifeli pia. Imeelezwa kwamba wasiwasi mkubwa uliibuka kwamba kama Nyerere angekutana na Ali basi pengine kungesababisha kuwapo kwa mgomo.

Badala yake, Ali alikutana na aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Vijana na Michezo wakati huo, Chediel Mgonja. Kuna ripoti mbalimbali zilizobainisha kwamba Nyerere aligoma kukutana na Ali kwa sababu alihisi kuwa ni kama dharau ya Rais Carter kumtuma bondia kuja kuzungumzia naye suala la kugoma kwenda Russia.

Pamoja na hilo, Ali mwenyewe alitia shaka juu ya ziara yake hiyo ya kisiasa. Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema hakuwa na ufahamu mzuri kuhusu ujumbe huo wa serikali yake ya Marekani kwa nchi za Kusini mwa Afrika ambapo, Tanzania na nchi zingine ziligomea mpango wa kugomea mashindano ya Olimpiki ya Moscow.

“Hawakuniambia kule Marekani kwamba Russia inazipa sapoti nchi hizi. Pengine nimetumika kufanya kitu kisichokuwa sahihi. Mmeniuliza maswali mazuri ambayo yananifanya nianze kutazama jambo hilo kwa mtazamo tofauti,” ilielezwa Ali kusema maneno hayo katika mkutano huo.

Rating: 9.7/10 (3 votes cast)
Rating: +1 (from 1 vote)
Makala: Nyerere agoma kukutana na Muhammad Ali9.7 out of 10 based on 3 ratings

Share this post:

Related Posts



No comments:

 
 
Blogger Templates