Vikosi maalum vya jeshi la Iraq vya kupambana na magaidi vimeanza hatua ya kuingia mjini Fallujah, na vinatarajia kupata upinzani mkubwa kuwahi kutokea katika kampeni ya kulikomboa eneo hilo kutoka kwa kundi la IS.
Mji huo ulioko kilometa 40 magharibi ya Baghdad umekuwa chini ya udhibiti wa wanamgambo kwa muda mrefu kuliko sehemu yoyote ya Iraq, na wapiganaji wa IS wamekuwa na zaidi ya miaka miwili kujiimarisha katika eneo hilo.
Njia kadhaa za chini ya ardhi kama zile zinazopatikana katika maeneo mengine yanayoshikiliwa na IS tayari zimekwisha gunduliwa katika kitongoji chake cha kaskazini mashariki.
Wapiganaji wanaounga mkono serikali wakishangiria kukombolewa kijiji cha al-Sejar karibu na Fallujah
Vikosi vya jeshi la Iraq, ambavyo pia vinajulikana kama vikosi vya kupambana na ugaidi, vinaongoza mashambulizi hayo dhidi ya mji wa Fallujah, taratibu vikisogea kutoka eneo la kusini katika msafara wa magari yenye silaha.
Hatua ya kusonga mbele inatarajiwa kuwa ya taratibu kwasababu mamia kwa maelfu ya raia wameendelea kukwama katika mji wa Fallujah na mabomu yaliyofichwa yanaaminika kuachwa katika sehemu mbali mbali za mji huo, kwa mujibu wa makamanda wa vikosi hivyo maalum katika eneo hilo.
Upinzani mkubwa
Wanatarajia upinzani mkubwa kutoka kwa wapiganaji hao wa Jihadi , ambao hawana sehemu ya kukimbilia.
"Hii ni vita muhimu kwetu na kwa Daesh," amesema jenerali Saad Harbiya kiongozi wa operesheni ya Fallujah katika jeshi la Iraq, akitumia neno la Kiarabu lenye maana ya kundi la Dola la Kiislamu.
Imam wa mji wa Fallujah Baahjet Ibrahim amesema watu wanateseka kutokana na vita hivyo.
"Kwasababu ya vita mjini Fallujah familia zetu na watu wetu wanaathirika. Wako kati ya nyundo ya jeshi na wanamgambo na jiwe la Daesh. Wale walioko ndani hawawezi kukimbia na wale walioko nje hawawezi kusaidia. Nina maana , hakuna chakula kabisa."
Gunia la ugna linapatikana kwa dola 854 na zaidi. Na huwezi hata kulipata. Ndugu zangu ambao bado wapo katika mji huo wanalipa hadi dola 683 kwa kilo 20 za mchele na kilo 20 za unga.
Mashambulizi hayo , yakisaidiwa na mashambulizi ya anga ya muungano unaoongozwa na Marekani, yalianza wiki moja iliyopita.
Mji huo ambao unaishi wasunni wengi katika jimbo la Anbar ni moja kati ya ngome ya mwisho kuu ya kundi la IS nchini Iraq. Kundi hilo la itikadi kali bado linadhibiti maeneo upande wa kaskazini na magharibi, pamoja na mji wa pili kwa ukubwa wa Mosul.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Hamidou Oummilkheir
Chanzo. Dw.de
No comments:
Post a Comment