Hakuwa na muda wa kusubiri, ilipofika majira ya saa moja na nusu usiku akaanza kujipara na kuvalia viguo vyake vya mawindoni. Akapendeza sana na ukichangia shepu yake na sura yake nzuri, unaweza kudhani hajazaa kumbe amepitia mambo magumu sana katika maisha yake tena angali akiwa binti mdogo sana.
Mwenyewe akikumbuka haya huishia kumwaga machozi, akajifuta na kujipaka make up kisha juu ya kile kiguo chake akavaa mtandio mwepesi bila kusahau kubeba kanga ambayo siku zote huwa haiachi ndani ya pochi yake.
Akanyanyua simu yake na kumpigia dereva wake wa bajaji. Wakati anamsubiria ndipo kisirani wake akaamka; “nakuona hapo changudoa unaenda kukiuza!” aliropoka Batuli akimtania mwenzake.
“Bora mimi kuliko wewe malaya mkimyakimya unatembea na mizee kwa ofa za bia! utakufa maskini. Halafu hela ya umeme zamu yako wiki hii,” alijibu mashambulizi Joy.
Akasikia bajaji inanguruma nje akachungulia na kugundua ni bajaji akatoka na kwenda kupanda.
“Joy, kwa hiyo hatuli dada angu!” alisema Batuli kwa unyonge lakini Joy aliondoka kimyakimya kama hajamsikia, akasahau kabisa kuhusu kuchoma vile vitambulisho na business card ya yule mteja wake wa jana aliyempa bingo ya laki mbili.
Akashuka windoni kwake akakiachia kimini chake, akatazama saa yake ya mkononi akagundua ni saa 3 usiku ni muda muafaka kwa ajili ya kazi, Akanunua kiroba kwenye duka la karibu na kujibust nacho ili kukata aibu. Akasimama uchochoroni, akapata mteja wa kwanza, kisha wa pili, lakini wakati anajiandaa kwa ajili ya watatu ghafla akajikuta ameshikwa mkono.
‘Loh ni askari tena wakiwa na defenda, ndani yake wakiwa wamewajaza wenzake kibao, naye akapakiwa ndani na safari ya kuelekea Oysterbay kituo cha Polisi ikaanza.
Walipofika kituoni na kuingizwa selo ilikuwa ni kawaida kwa Joy na wenzake ambapo walimalizia masaa machache ya usiku huo na asubuhi ikawa safari ya kuelekea mahakama ya jiji pale Posta karibu kabisa na Kanisa katoliki la St Joseph.
Hapo hutozwa faini ya shilingi elfu hamsini au jela miezi mitatu kwa kosa la uzurulaji na hiyo inatokana na ukweli kwamba sheria ya Tanzania haisemi chochote kuhusu biashara ya ngono hivyo, hata kama polisi watawakamata machangudoa ni lazima wawashtaki kwa kosa la uzurulaji na si vingine.
Hizo ndiyo hatua ambazo Joy akiwa na machangu wenzake walitazamia kuzipitia. Kwa kuwa wengi wao wamezoea kupandishwa mahakamani mara kwa mara na kutoa faini hiyo ya shilingi elfu hamsini, waliona ni jambo jepesi kwao na kuhakikisha hakuna changudoa mwenzao ambaye atakwenda jela, machangudoa kwenye kijiwe cha Joy walikuwa na mfuko wa kusaidiana yaani kama vile vicoba ambapo kila mmoja huchangia shilingi elfu tano kwa wiki ili iwasaidie kwenye masuala kama hayo.
Yaani hata kama changu mwenzao amefiwa hao ndiyo humchangia shughuli nzima za mazishi, sasa vuta picha msiba umedhaminiwa na machangu!
Walikaa ndani ya selo ya mahaka wakiwa na wafungwa wengine wa kike toka sehemu mbalimbali, wakitarajia kesi yao itasikilizwa mapema saa 2 kamili ili saa 4 waondoke hapo mahakamani, lakini tofauti na walivyotarajia hadi majira ya saa 6 asubuhi, hakukuwa na dalili yoyote ya kesi yao kusomwa.
Ilipofika saa 8 mchana walisikia afande mmoja wa magereza akizungumza na wenzake; “Sasa kama hakimu hajaja na hawa machangu si nao tuwapeleke Keko, wakalale hadi kesho?”
“Nini tunapelekwa jela?” aliropoka Suzy akiangua kilio. Kama ulikuwa haujui Suzy mmoja wa machangu wakubwa kijiweni kwa akina Joy na alikuwa mke wa mtu. Hivyo kwa vyovyote hofu aliyokuwa nayo yeye ilimzidi kila mtu hapo ndani maana kama mumewe akimtafuta na kugundua kumbe aliwekwa ndani kwa kujiuza itakuwaje!
Je nini kitafuata Usikose Jumatatu
Chanzo. Fredynjeje
No comments:
Post a Comment