Social Icons

Friday, 19 August 2016

Kwa nini hali ya wasiwasi imerejea Ukraine?

KIEV, UKRAINE – HALI ya wasiwasi imeongezeka katika Jimbo la Crimea ambalo lilijitenga kutoka nchi ya Ukraine ili kuujiunga na Urusi. Hali hiyo ya wasiwasi imezidi katika wakati ambao Ukraine inaimarisha jeshi lake tayari kwa vita.

Amri hiyo ya kuliweka ‘sawa’ jeshi hilo imetolewa baada ya Urusi kuishutumu Ukraine kwamba siku ya Agosti 10 mwaka huu ilipanga kushambulia miundombinu muhimu nchini humo.

Hili linaashiria kuanza kwa kipindi kingine kibaya katika uhusiano baina ya mataifa hayo mawili, uhusiano ambao hata hivyo umekuwa mbaya tangu Urusi ilipotwaa Jimbo hilo la Crimea, miaka miwili iliyopita, yaani 2014.

Ofisa mmoja wa NATO aliliambia Shirika la Habari la CNN kwamba chombo hicho cha ulinzi wa kujihami kina wasiwasi  kuhusu kuongezeka kwa vitendo vya fujo huko mashariki mwa Ukraine na kuitaka Urusi kuacha ukwapuaji wa eneo la Crimea ambao amedai umefanywa kinyume cha sheria wa Crimea.

Ni kitu gani kimesababisha matatizo ya sasa na ni kipi kinaweza kutokea baadaye? Nick Paton wa CNN anajibu maswali muhimu kuhusu mgogoro huo katika makala hii kama ifuatavyo.

Kwa nini hali tete?

Ni vigumu kujua. Ikulu ya Urusi maarufu kwa jina la Kremlin inapenda kuweka nia yake hivyo. Lakini bila shaka tumeona miezi mingi ya taarifa za kuongezeka kwa silaha katika maeneo ya wanaotaka kujitenga na maeneo ya mstari wa mbele wa Ukraine.

Matendo haya hutokea kwa vipindi lakini wiki hii Shirika la Kijasusi la Russia – FSB – linadai kufanikiwa kuzuia jaribio la Shirika la Kijasusi la Jeshi la Ukraine kushambulia eneo la Crimea na kwamba askari wake wawili walishambuliwa walipojaribu kuingia Ukraine.

Ukraine inasema kuwa madai hayo ni upuuzi mtupu. Lakini Rais wa Urusi, Vladimir Putin ametumia kisingizio hicho na kutangaza kuwa mazungumzo zaidi ya amani hayana maana na Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko, ameamrisha majeshi yake kuwa katika hali ya tahadhari. Hali haijawahi kuwa mbaya kiasi hiki tangu vita vya mwaka 2015.

Nini kinafuata?

Nje ya suala la Crimea, wachambuzi wa Urusi wanasema kuwa kwa muda mrefu nchi hiyo imekuwa ikitamani kuwa na sehemu ya ardhi kati ya maeneo ya Donetsk wanayomiliki na Crimea. Kuihudumia Crimea imekuwa ni vigumu kwa sababu njia pekee ya kupeleka bidhaa kutokea Urusi ni kwa kutumia vivuko vya maji.

Pichani hali ilivyo mashariki mwa Ukraine

Kama ni kitu cha kuamini, kwamba sehemu ya ardhi ndiyo mpango hasa ya Urusi ni kwa nini hili la kuitwaa Crimea liwe sasa hivi? Urusi imejihusisha na mgogoro mwingine ambao nchi za Magharibi zingependa uishe – ambao ni Syria. Labda ni kitu chenye uzito na umuhimu mkubwa kwa Ikulu ya White House – Marekani kuliko Ukraine kutokana na uhusika wa kundi la kigaidi la ISIS.

Kremlin inaweza kudhani kuwa inaweza kuwa na msaada huko zaidi ili kupunguza vikwazo vya kiuchumi itakavyoweza kuwekewa na nchi za magharibi iwapo itaamua kuivamia Ukraine.

Ukichanganya na hayo, Ukraine imekuwa ikifanya mabaya pia. Wazalendo wamekuwa ni sehemu kubwa ya askari ambao wako katika mstari wa mbele wa mapambano wa Ukraine na hasira dhidi ya vyombo vya habari imeongezeka kiasi cha kusababisha ofisa mmoja wa ngazi za juu wa Ukraine kujiuzulu baada ya taarifa juu ya waandishi wa habari wanaofanya kazi katika maeneo ya waasi kuvuja na kuchapishwa kwenye internet.

Marafiki zake wa Ulaya wamechoshwa na mbio ya mabadiliko. Yote hayo yataibua maswali mengi zaidi kuhusu ni uungwaji mkono wa kiasi gani Ikulu ya Kiev huko Ukraine inaweza kutegemea iwapo vita itaibuka tena.

Nani ana nguvu zaidi?

Miaka yote Urusi imekuwa na jeshi lenye nguvu zaidi linalowasaidia waasi wa Ukraine. Ukraine imeimarisha jeshi lake lakini limebaki kuwa na ukosefu mkubwa wa fedha na kukosa msaada wa kutosha kutoka nchi za magharibi. Kumekuwa na mauaji ya viongozi muhimu wa waasi vile vile.

Hata hivyo, waasi wamekuwa na muda wa zaidi ya mwaka mzima kuweza kujiimarisha kwa silaha tangu mapigano ya mwisho ya Debaltseve – jiji la mstari wa mbele huko mashariki mwa Ukraine. Kwa upande mwingine ni kama vile Ukraine imekuwa katika migogoro kiasi cha kuikwamisha kumudu kujiandaa vizuri.

Nani wahusika wakuu?

Rais Putin wa Urusi hutoa amri na kiongozi wa waasi Alexander Zakharchenko anatajwa kutii amri hizo. Poroshenko kwa upande wake atazidi kukabiliwa na shinikizo kwamba asikubali kushindwa huku sauti ya wazalendo wa nchi hiyo ikiongozwa na mfungwa wa zamani wa kivita Nadia Savchenko ikizidi kutoa hamasa kwake.

Vikwazo vya kiuchumi vya nchi za magharibi dhidi ya Urusi juu ya suala la Crimea bado vipo. Lakini Urusi inaonekana kuathirika zaidi ndani ikilaumu kuharibika kwa uchumi wake kuwa ni njama za nchi za magharibi.  

Waangalizi kutoka Taasisi ya Ulinzi na Ushirikiano ya Ulaya (OSCE) hawana nguvu na sehemu kubwa ya mapambano hutokea usiku wakati ambapo wao hawapo. Kwa kifupi, hakuna anayefanya lolote kuhusiana na hali hiyo na ndiyo maana hali ya mambo inaharibika kwa haraka kiasi hicho. Unaweza kusema hii ni vita ya ardhini dhidi ya bara la Ulaya ikihusisha taifa lenye silaha za nyuklia, lenye chuki na mataifa ya NATO. Hatari ni kubwa, hata kama mataifa ya magharibi hayana nia ya kujihusisha.

Chanzo. Raia mwema

 

No comments:

 
 
Blogger Templates