KIPINDI cha kiasi wiki tatu zijazo kinaweza kuamua hatma ya kisiasa ya chama kikuu cha upinzani nchini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuhusu endapo mkakati wake mpya wa kisiasa utafanikiwa au kufeli.
Chadema kimezindua mkakati wake mpya wa kisiasa, Operesheni Ukuta (Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania); ambao kilele chake kimepangwa kuwa Septemba Mosi mwaka huu.
Mkakati huo wa kisiasa unahusisha kufanyika kwa maandamano na matukio mengine ya kisiasa nchi nzima; katika kipindi ambacho serikali imepiga marufuku baadhi ya shughuli za kisiasa.
Katika kipindi cha takribani muongo mmoja uliopita, Chadema kimekuwa ikijinasibisha na walau operesheni moja katika kila kipindi cha miaka mitano na zote zimekuwa na mafanikio.
Katika kipindi cha kati ya mwaka 2005-2010, kiliibuka na Operesheni Sangara ambayo ilikipa umaarufu kiasi kwamba kiliweza kushinda ubunge wa majimbo mawili katika majimbo ya Mwanza Mjini na maeneo mengine ya Kanda ya Ziwa.
Kati ya mwaka 2010-2015, kiliibuka na kilichoitwa Movement for Change (M4C) ambayo inasifika kwa kukaribisha vijana wengi kujiunga na chama hicho.
Mwaka huu, katika awamu ya kwanza ya kipindi cha miaka mitano ya Rais John Magufuli, Chadema kimeibuka na mkakati mpya wa Ukuta ambao utakuwa kwenye majaribio makubwa katika kipindi cha siku 21 zijazo.
Kama Ukuta ikipata mafanikio yanayotarajiwa, Chadema kitakuwa sasa kimejisimika kama chama kikuu cha upinzani hapa nchini lakini baadhi ya wachambuzi wana hofu kwamba kama Ukuta utayumba, chama hicho kinaweza kujikuta kwenye hali ngumu zaidi.
Operesheni Sangara
Operesheni ya kwanza kukipa umaarufu Chadema ilifahamika kwa jina la Operesheni Sangara (OS) iliyofanyika kwenye awamu ya kwanza ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, wazo la kuwa na OS lilitokana na kazi za kisiasa na kijeshi zilizokuwa zikifanywa na chama cha Frelimo cha Msumbiji.
“ Wazo la kuwa na Operesheni Sangara lilikuwa la kwangu. Nilikuwa nasoma kitabu kilichoandikwa na Rais Yoweri Museveni cha Sowing the Mustard Seed ambako niliona kitu kinachoitwa Frelimo Operations.
“ Kwamba wakati wa vita ya Ukombozi wa Msumbiji, majeshi ya Frelimo yalikuwa yakifanya mambo mazuri katika maeneo ambayo walikuwa wameyatwaa kwa ajili ya kufanya wengine nao watamani kuwa chini yao.
“Chadema ilikuwa imetoka kupata jimbo la Tarime kwenye uchaguzi mdogo na nikaona kwamba tunaweza kutumia mbinu za Frelimo (ukiondoa zile za kijeshi) kwenye maeneo ambako tumeshinda uchaguzi. Wakati huo tukataka kuanzia Kanda ya Ziwa.
“ Mwaka 2009, tukakuta Sangara ni jina murua; kwani ni samaki aliye katika Ziwa Viktoria, na ni samaki anayeliingizia taifa mapato mengi sana. Takwimu za Hali ya Uchumi wa Taifa zinaonyesha kuwa samaki wa Ziwa Viktoria wanachangia takriban asilimia nane ya mauzo yetu nje ya nchi. Thamani ya mauzo ya samaki kutoka Ziwa Viktoria ni karibia Tshs. 150 bilioni kwa mwaka.
“Siku moja nilikuwa kwenye ndege tukiwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe na tukawa tunazungumza na nikamwambia kuhusu hilo wazo langu. Kwa bahati nzuri akalipokea vizuri na kunitaka niandike andishi kulihusu.
“ Nikaandika kama alivyonishauri na likajadiliwa kwenye vikao vya chama na wenzangu na kupitishwa. Nakumbuka mimi na John Mrema tulifanya kazi kubwa sana mkoani Mwanza wakati huo,” anasema Zitto ambaye wakati huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema.
Operesheni M4C
Akizungumza na Raia Mwema wiki hii, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema John Mrema, alitoa maelezo mafupi kuhusu operesheni za nyuma za Chadema, malengo yake, mafanikio na matarajio kupitia Ukuta.
Katika maelezo yake, Mrema alisema; “M4C ilianzia kwenye vuguvugu la kudai Katiba mpya mwaka 2011 tulipoanza maandamano Kanda ya Ziwa na tulipofika Arusha wazo likazaliwa la Vuguvugu la Mabadiliko: M4C -Movement for Change . Hii iliendelea mpaka mwaka 2015 na ilikuwa na mafanikio kama ifuatavyo;
“Mwaka 2012 ..tuliweza kushinda uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki. Tulishinda kata nyingi za marudio na pia tuliweza kuimarisha chama kwenye ngazi za chini na hasa kwenye programu ya Chadema ni msingi.
“Tuliweza kuimarisha chama kikawa na wagombea kwenye ngazi za Serikali za Mitaa 2014 na kuweza kushinda kwa kiwango kikubwa na kuvuta wanachama wapya kwa maelfu nchi nzima.
“Tuliweza pia kuunganisha nguvu na kuunda Ukawa iliyozaa matunda kwani uchaguzi wa 2015 tuliweza kupata wabunge 117 kama Ukawa huku Chadema tukipata wabunge 73 na madiwani 1,189 nchi nzima na kura zaidi ya milioni sita za urais.
Operesheni Ukuta
Kwa mujibu wa Mrema; “Hii ilitokana na tafakuri ya kina juu ya kilichowahi kumkuta mchungaji Martin Niemoller wa huko Ujerumani wakati wa utawala wa dikteta Adolf Hitler.
“Wakati Hitler alipoanza hatua za kuminya demokrasia, mchungaji huyu alikaa kimya. Alikaa kimya pia wakati makundi mbalimbali katika jamii yalipokuwa yakiadhibiwa. Dikteta huyo wa Ujerumani kwanza alianza na wakomunisti huyu Martin hakusema lolote kwani alijiona si mkomunisti.
“Alipokwenda kwa kundi la vyama vya wafanyakazi mchungaji hakusema kitu kwa kuwa yeye hakuna mwanachama huko na hata alipokwenda kundi la Wayahudi alikaa kimya kwani hakuwa Myahudi.
“Ilipomfikia zamu yake hapakuwa na mtu wa kusema kwa ajili yake na alijikuta akienda kufungwa kwenye makambi kwa miaka saba.
“Ndiyo maana tunawataka Watanzania kujiunga na umoja huu kwani kama wameshafikiwa kwenye makundi yao, basi waje ili kuzuia wengine wasiumie bila kufuatwa kwa taratibu za kisheria.
“Kama hawajafikiwa wajiunge na Ukuta ili wakifikiwa awepo mtu wa kusema kwa ajili yao pindi akifikiwa.
“Ukuta ni operesheni tofauti na hizi nyingine kwani hii hailengi kuimarisha Chadema. Hii ni kwa ajili ya Watanzania wote na lengo kuu ni kupigania utawala unaoheshimu Katiba na Sheria za nchi.
“Ni operesheni ya kitaifa zaidi kuliko itikadi za vyama . Ndio maana inaitwa "Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania.
“Kuna kila sababu ya Watanzania kujiunga na Umoja huu kwa ajili ya kulinda utawala wa sheria. Wasikae kimya kwa sababu hawajafikiwa wasimame sasa. ..tayari makundi mengi ya kijamii wameshafikiwa wasisubiri mpaka wafikiwe ndipo waanze kupigania demokrasia. .
Mmoja wa wachambuzi mashuhuri wa masuala ya kisiasa nchini, M.M Mwanakijiji, amekosoa operesheni hiyo akisema haina uhalisia kutokana na hali ya sasa iliyopo nchini.
Akiandika katika mtandao wa kijamii wa Jamii Forums hivi karibuni, Mwanakijiji alisema tofauti na operesheni za nyuma za chama hicho, Ukuta itakosa mwitikio wa maana kutoka kwa wananchi.
“Tangu walipoanza na Operesheni Sangara, Operesheni Mzizima, M4C, wengi tuliona hatari ya kampeni hizi zenye majina mbalimbali ambayo labda matokeo yake yanaweza kubishaniwa.
“Kwa wanaojua, mimi sikuwahi kuwa shabiki wa lile dubwasha la UKAWA ambalo naamini lilichangia sana kuvuruga upinzani na mwelekeo wa upinzani kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
“Lakini kama vile ndugu zetu hawataki kujifunza au wamegoma kujifunza baada ya kikao chao kingine wameamua kuja na kampeni nyingine au operesheni nyingine ambayo sasa wameamua kuiita “Ukuta” ukiwa ni Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania.
“Nina uhakika wa kutosha kati ya operesheni zitakazoshindwa vibaya ni hii. Kwa sababu wakati zile nyingine kwa kiasi ziliakisi hisia za Watanzania wengi na zilibeba kwa kiasi maudhui ya matamanio yao hii ya sasa ni operesheni ya wasomi wachache (the few elite) ambao wanaamini kinadharia na kwa sababu zao za kisomi kuwa (Rais) Magufuli ni dikteta.
“Wanaamini hivi na wanataka watu wa kawaida ambao hawaoni huo udikteta wa Magufuli waunge mkono. Operesheni hii itafeli kwa sababu, mamilioni ya Watanzania waliokuwa wanalalamikia watoto wao kukosa madawati leo wanaona madawati yanatengenezwa na kupatikana kwa wingi.
“Waliokuwa wanalalamikia watu kutokuwajibika au kuwajibishwa wanaona watu vigogo wanawajibishwa kila kona, na wale ambao walikuwa wanataka kuona serikali inasimamia vizuri watendaji wake wanaona hilo linatokea tena bila kupepeseana macho.
“Wale ambao kwa muda mrefu walikuwa wanataka mafisadi washughulikiwe bila huruma leo hii wanaanza kupinga serikali ambayo imeanzisha na kutenga fedha tayari kwa ajili ya mahakama maalumu ya kushughulikia wahujumu uchumi na mafisadi.
“Ndio maana hofu yangu ni kuwa tusipoangalia baada ya harakati hizi kushindwa; ndugu zetu wapendwa hawa wanaweza wakaja na operesheni “UKUTI UKUTI”.
“Binafsi ningependa kuona Chadema kinarudi na kuwa chama cha siasa na kufanya mambo yake kama Chadema, na kupitia taasisi zake. Hizi operesheni zake mbalimbali si tu zinapoteza muda mrefu lakini pia zinatishia zaidi uhai wake kama chama cha siasa na kwa vile viongozi wake bado hawajawajibishwa kwa madudu yao ya mwaka jana, basi wanaweza kabisa kwenda kuipoteza Chadema kuelekea 2020,” ameandika.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu aliyepita wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, anasema Ukuta ni muafaka kwa sasa kwa sababu Rais Magufuli ametaka iwe hivyo.
Anasema yatakuwa ni makosa makubwa endapo vyama vya upinzani na wafuasi wao watakaa kimya katika wakati ambao inaonekana serikali haitaki kuwapo kwa uwanja sawia wa ushindani wa kisiasa.
“ Juzi hapa kuna wanachama wa upinzani wamekamatwa wakiwa katika mechi ya mchezo wa mpira wa miguu jijini Dar es Salaam kwa sababu zisizo na kichwa wala miguu.
“ Sasa huku tunakokwenda, tunaenda wapi? Kama Rais Magufuli angekuwa haonyeshi kuvibana hivi vyama, hakuna ambaye angekuwa anazungumzia Ukuta hivi sasa lakini mazingira yaliyopo yamesababisha hili,” alisema.
Hata hivyo, Mtatiro ambaye sasa ni mchambuzi huru wa masuala ya kisiasa na kijamii anasema tatizo lake na Ukuta ni kwamba imeanzishwa kama kampeni ya chama kimoja.
“ Karibu vyama vyote vya kisiasa vinaunga mkono Ukuta. Ingekuwa vizuri sana kama vingeunganishwa vyote na kujadili kuhusu uamuzi huu wa Operesheni Ukuta. Kwa hali ilivyo sasa inaonekana kama ni chama kimoja jambo ambalo si zuri,” alisema.
Chanzo. Raia mwema
No comments:
Post a Comment