Social Icons

Saturday, 13 August 2016

WANANCHI WA NDANTO WAMPONGEZA MKUU WA MKOA MBEYA MHE. AMOSI MAKALA KWA KUWAPATANISHA

Wananchi wa Kata ya Ndanto wilayani Rungwe wamempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amosi Makala kwa kumaliza uhasama uliokuwepo katika kata hiyo kati ya wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi na wafuasi wa UKAWA uliodumu toka kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amosi Makala akiwahutubia wananchi wa Kata ya Ndanto
Wakati wa kuwapatanisha.

Wafuasi wa vyama hivyo walifikia hali ya kutokuzikana, kutokushirikiana katika sherehe mbali mbali, kuchomeana nyumba na kadhalika, lakini Mkuu wa Mkoa aliwatembelea katika kata hiyo na kuitisha mkutano wa hadhara uliohudhuliwa na viongozi wa vyama vyote vya siasa akiwemo Mbunge wa Jimbo la Rungwe Mhe. Saul H. Amon, Mkuu wa Mkoa alitoa nafasi kwa pande zote kueleza kinachowakera dhidi ya wenzao.

Mheshimiwa Amos Makala akipokea zawadi ya jogoo kutoka kwa mwananchi wa
Ndanto aliyoitoa kutokana na furaha ya kupatanishwa kwani alichoka na uhasama

Baada ya kuwasikiliza Mkuu wa Mkoa aliwataka viongozi wa vyama vyote kuwatuliza wafuasi wao, na kuwaambia wananchi wa Ndanto wasikubali kuchonganishwa na viongozi wa kisiasa kwani mwisho wa siku wanapofanya makosa ya kijinai hushitakiwa wao, na viongozi wa kisiasa hawaonekani mahakamani hata magerezani wanapo hukumiwa vifungo.

Mheshimiwa Amos Makala akipokea zawadi za viazi na mihogo kutoka kwa wananchi
wa Ndanto

Mwisho wa mkutano wananchi walifurahi sana kwa upatanisho alioufanya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amosi Makala, na kumpatia zawadi mbali mbali za vyakula vikiwemo viazi mviringo, mihogo, kuku na kadhalika.

Imeandikwa na Bashiru Madodi.

No comments:

 
 
Blogger Templates