Marekani imekubali kusambaza misaada ya kijeshi yenye thamani ya dola bilion 38 kwa Israel,mpango ambao ni ishara ya makubaliano muhimu Kati ya Benjamin Netanyahu na Rais Barack Obama
Baadhi ya wanajeshi wa Jeshi la Israel
Makubaliano ya kutolewa kwa msaada huo yanafuatia miezi kadhaa ya majadiliano baina ya nchi hizo mbili. Marekani na Israel zilitiliana saini ya makubaliano hayo siku ya Jumatano (14 Septemba 2016) ambapo mpatanishi mkuu wa Israel na kiongozi wa baraza la usalama la nchi hiyo, Jacob Nagel, aliiwakilisha nchi yake kwenye utiaji saini katika Ikulu ya Marekani, mjini Washington.
Ndani ya takribani miezi 10 ya majadiliano ya kimya kimya, kulijitokeza msuguano wa wazi kati ya Rais Obama na Waziri Mkuu Netanyahu, ambapo kwa mwaka uliopita makubaliano ya Marekani na washirika wake na Iran juu ya mpango wa nyuklia wa Iran yalikosolewa vikali na Netanyahu. Chini ya utawala wa Obama, pamekuwa pia na tafauti kubwa kati ya Marekani na Israel kuelekea suala la Palestina.
Moja kati ya makubaliano muhimu katika mazungumzo hayo ni kuwa ili Israel iweze kupata fedha hizo, ni lazima kuwe na makubaliano ya kutokuchua fedha za ziada kutoka Congress na kuahidi kuwa hawatatumia fedha za msaada kwa ajili ya ulinzi wake yenyewe.
Lakini sasa Netanyahu, mwanasiasa mwenye siasa kali za mrengo wa kulia, ameona ni vyema kuwa na makubaliano hayo mapya na Marekani chini ya uongozi wa Rais Obama ambaye anatarajia kumaliza muhula wake mapema mwakani, badala ya kusubiri uongozi mpya, akihofia kutokujuwa yajayo na utawala mpya. Makubaliano hayo sasa yanatoa mwanya wa kutokuwepo wa mahusiano ya kusuasua na kiongozi yeyote atakayefuata kuliongoza taifa hilo kati ya Hillary Clinton kutoka Democrat na Donald Trump wa Republican.
Makubaliano yakoselewa
Makubaliano hayo sasa yanaiwezesha Marekani kuisadia Israel, licha ya kuwa baadhi ya wakosoaji wanasema mkataba huo ulihitaji heshima kwa kuwa unaonekana kuwa na masharti magumu na haujitoshelezi kukabiliana na mahitaji ya Israel.
Katika awamu ya kwanza ya makubaliano hayo, Israel itapokea dola milioni 500 kwa mwaka kwa ajili ya kununua silaha za kujihami ambazo zimetolewa na baraza la Congress, ambalo pia kwa miaka ya hivi karibuni limeipatia Israel jumla ya dola milioni 600 kwa mwaka kwa malengo kama hayo.
Maafisa wa serikali wanasema Israel imeamua kutokuendelea kulibana baraza la Congress kuendelea kutoa fedha za nyongeza kwa ajili ya silaha hizo katika kipindi chote cha utekelezaji wa makubaliano hayo, pamoja na kuwa kunaweza kutokea maombi maalumu katika hali ya dharura kama vile vita au mashambulizi dhidi yake.
Mwandishi: Celina Mwakabwale/ Reuters/DW English
Chanzo. Dw.de
No comments:
Post a Comment