Social Icons

Friday, 16 September 2016

Mazungumzo mapya ya amani nchini Msumbiji

Wasuluhishi wa kimataifa wameshafika nchini Msumbiji ili kuongoza mazungumzo ya amani lakini wakati huo huo maeneo mengine yanakabiliawa na machafuko.

Wananchi wa Msumbiji katika mkutano wa kisiasa

Wakati mazungumzo hayo ya kusaka amani yakiwa karibuni kuanza, wachambuzi wanasema serikali ya Msumbiji inataka kuendesha mazungumzo hayo ikiwa ndiyo yenye ushawishi na nguvu kubwa. Vyombo vya usalama vimekuwa vikiendelea kuyatwaa maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na wapiganaji wa Renamo, na haviachi kujisifia kwa mafanikio hayo.

Kwa mujibu wa msemaji wa polisi, Jacinto Felix, ni hivi majuzi tu walipoutwaa mji wa Morrumbala uliopo katika jimbo la kati la Zambezia, makao makuu ya Renamo lakini msemaji huyo wa polisi hakuzungumzia kuhusu watu waliouwawa kwenye uvamizi huo uliofanywa na vikosi vya serikali ya Frelimo katika makao makuu ya Renamo.

Wakati huo huo, duru rasmi zimesema kuwa watu tisa wameuwawa. Kwa mujibu wa taarifa ya ripota wa Deutsche Welle aliyeko mjini Maputo, inaaminika kwamba waasi na raia wengi wameuwawa.

Waasi wa Renamo waliposhambuliwa

Tokea Msumbiji ipate uhuru wake mwaka wa 1975, Frelimo imekuwa inalinda utawala wake hasa katika ngazi ya kidiplomasia, na sasa matumaini juu ya kufanikiwa mazungumzo haya si mazuri kwa sababu pande zote mbili zimezidi kuwa na misimamo mikali.

Kiongozi wa Renamo, Afonso Dhlaklama, ametangaza kuwa atawaamuru wapiganaji wake kuweka silaha chini iwapo tu serikali itahakikisha kwamba wapiganaji wake wataingizwa kwenye jeshi la serikali.

Je serikali inakabiliwa na changamoto zipi?

Mmoja wa wajumbe katika mazungumzo hayo, Egidio Vaz, amethibitisha juu ya shinikizo la Renamo kwa serikali kwamba linazidi kuwa kubwa. "Amani itapatikana ikiwa serikali itayakubali matakwa ya Renamo yakiwa ni pamoja na kuwaingiza katika jeshi la serikali maafisa wa chama hicho na vile vile serikali ihakikishe mageuzi ya katiba na kiutawala katika majimbo yote". Anasema mpatanishi huyo.

Wajumbe huru wanatarajia mazungumzo kati ya serikali chini ya chama cha Frelimo na chama cha waasi wa Renamo kuwa magumu. Raia wa Msumbiji walikuwa na matumaini makubwa ya kufikiwa mapatano katika mazungumzo yaliyofanyika katikati ya mwezi Agosti lakini walivunjika moyo baada ya mapatano kukosa kupatikana.

Mwandishi: Antonio Cascais/DW Maputo

Chanzo. Dw.de


No comments:

 
 
Blogger Templates