Social Icons

Thursday, 8 September 2016

Mfumuko wa bei wapungua mwezi Agost

Mfumuko wa bei kwa mwezi Agosti mwaka huu umepungua hadi kufikia asilimia 4.9 kutoka asilimia 5.1 kwa mwezi Julai, kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu Nchini (NBS).

Kupungua kwa mfumuko wa bei ni matokeo ya kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za huduma na bidhaa kwa mwezi Agosti ikilinganishwa na kasi ya mwezi Julai.

Baadhi ya bidhaa zilizosababisha kupungua kwa mfumuko wa bei ni nafaka ambazo bei yake imeshuka kwa asilimia 0.6 na bei ya unga wa mhogo imeshuka kwa asilimia 2.1.

Katika kipindi hicho cha mwezi jana, bei ya dagaa, ambazo ziko kwenye kundi la bidhaa chakula ilishuka kwa asilimia 3  wakati bei ya mbogamboga ilipungua kwa asilimia 2.6.

Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, farihisi za bei zimeongezeka hadi kufikia 103.28 mwezi Agost kutoka asilimia 98.49 za mwezi Agost mwaka jana.

Mfumuko wa bei ya vyakula na vinywaji visivyo na kilevi umepungua na kufikia asilimia 7.0 mwezi jana ikilinganishwa na asilimia 7.6 za mwezi Julai mwaka huu.

Ripoti hiyo imeonyesha kwamba, katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, kiashiria cha bidhaa zisizo za chakula kimeshuka hadi kufikia asilimia 3 mwezi Agosti mwaka huu kutoka asilimia 3.2 mwezi Julai.

Hata hivyo, kiashiria cha bidhaa nyingine ukiondoa chakula na nishati kwa mwezi Agosti hakikubadilika katika kipindi hicho na kubakia palepale kwenye asilimia 2.6.

Chanzo. Raia mwema.

No comments:

 
 
Blogger Templates