Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, dunia itashuhudia tukio hilo la Septemba 16, mwaka huu la kupatwa kwa mwezi kivuli, ikiwa ni muendelezo wa tukio hilo la kupatwa kwa jua la Septemba Mosi.
Anasema katika tukio la Septemba 16, mwezi utakuwa upande wa pili wa dunia na kwamba nusu ya dunia inatarajiwa kuona tukio hilo la kupatwa kwa mwezi kivuli na kwa hapa nchini litaonekana sehemu zote.
Ilivyokuwa kupatwa Jua
“I have seen one eclipse before, but this one is special as it occurs in Rujewa,” Hii ni kauli ya mtalii kutoka nchini Sweden, Birgitta Palm Andersson, ambaye hiyo ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza kukanyaga Bara la Afrika, mahususi kuja kushuhudia kupatwa kwa jua.
Pamoja na ugeni wake, bado mtalii huyo alitumia muda wake mfupi aliokuwepo Mbeya, hususani eneo la Mpunga mjini Rujewa katika Wilaya ya Mbarali kujifunza maisha ya Watanzania.
“People here are very very friendly and the food taste so good,” alisema Birgitta akielezea maisha yake katika siku chache alizoishi Tanzania, ambapo tafsiri isiyo rasmi alikuwa na maana kwamba “Watu ni wakarimu sana na chakula hapa kina ladha nzuri.”
Birgitta ni miongoni mwa watalii waliofika mkoani Mbeya na Njombe mahsusi kushuhudia kupatwa kwa jua. Pamoja na Sweden, watalii wengine walitoka Ujerumani, Marekani na Canada.
Walikuwepo pia watalii kutoka nchini China, Australia na kwa nchi za Afrika walikuwepo kutoka nchini Malawi, Zambia, Uganda na Kenya.
Watalii wengine waliokuwepo kwenye tukio hilo ni pamoja wanafunzi kutoka shule mbali mbali za msingi na sekondari zilizo jirani na maeneo ya Mpunga mjini Rujewa na katika kijiji cha Kitunda, Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe.
Kivutio kingine katika tukio la kupatwa kwa jua siku hiyo ilikuwa ni uwepo wa Mwanasayansi wa masuala ya anga kutoka Ujerumani, Dk. Eckahard Schmidf ambaye alifuatilia tukio hilo kutokea kijiji cha Litundu, wilayani Wanging’ombe, takribani kilometa 45 kutoka Rujewa.
Dk. Schmidf anasema hilo ni tukio lake la 19 kushuhudia ambapo anatarajia mwakani kushuhudia tukio la 20 kama hilo linalotarajiwa kutokea nchini Marekani.
Wanafunzi kutoka Shule ya Wasichana Sega mkoani Morogoro walivutia zaidi halaiki iliyohudhuria tukio hilo, kikubwa ni hatua yao ya kusafiri zaidi ya kilometa 600 kuja kujionea wenyewe kupatwa kwa jua.
Mtaalamu kutoka Kitivo cha Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Mazingira, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk. Noorali Jiwaji anasema ni mara ya kwanza, katika historia ya nchi kuhusu masuala ya kupatwa kwa jua watu kujitokeza kwa wingi kiasi kile.
“Nimependa jinsi watu walivyojitokeza kwenye tukio la kisayansi,” alisema Dk. Jiwaji.
Matarajio ya mtaalamu huyo, kutokana na uzoefu wa huko nyuma ilikuwa watu 500, lakini kwa mshangao walijitokeza zaidi ya watu 5,000 katika eneo la Mpunga mjini Rujewa pekee. Wengine wengi waliendelea kufuatilia katika maeneo mbali mbali ya nchi.
Sega Girls wamewezaje
Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Sega ni maalumu kwa ajili ya watoto wa kike wanaoishi kwenye mazingira magumu ikifadhiliwa na Shirika la Marekeni liitwalo “Nurturing Minds in Africa,” hawa walikuwepo Rujewa pamoja na walimu wao wa kujitolea kutoka Marekani.
“Leo tunashuhudia kwa macho yetu kupatwa kwa jua, tulijifunza kwa nadharia, tulisimuliwa na walimu lakini leo tunajifunza kwa kuona wenyewe,” anasimulia mwanafunzi wa kidato cha tatu kutoka Shule ya Sekondari Sega, Sophia Kalagusi.
Uhusiano wa shule hiyo na Marekani ndiyo uliowawezesha kulifuatilia tukio hilo la kupatwa kwa jua kwa karibu zaidi tofauti na shule zingine hapa nchini. Shule hiyo kutoka Morogoro ilifika Rujewa lakini shule za jijini Mbeya na hata za wilayani Mbarali zilishindwa kupeleka wanafunzi wao.
Mwalimu Ng’habi Mbogo wa Shule hiyo ya Sekondari Sega, anasema kuwa uhusiano uliopo kati yao na taasisi hiyo ya Nurturing Minds in Africa ya Marekani, huwawezesha kupata taarifa zote muhimu duniani kwa ajili ya wanafunzi wao.
“Tulijulishwa mwishoni mwa mwaka jana tumeleta darasa moja kushuhudia, tumetengeneza vifaa vya kutazamia, 500 tumekuja navyo hapa na 500 tumempatia Mkuu wa Mkoa,” alisema Mwalimu Mbogo akiwa eneo la Mpunga mjini Rujewa.
Maandalizi na ushiriki wa shule hiyo unatoa fundisho juu ya kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza, kupatwa kwa jua ikiwa mojawapo.
Ilikuwa fursa muhimu kwa wanafunzi kujifunza, wafanyabiashara kuwekeza kwa ajili ya tukio hilo na sekta ya utalii kulitumia kutangaza utalii na kuingiza fedha nchini. Kuamkia siku ya tukio, nyumba zote za kulala wageni katika miji ya Rujewa, Igawa, Igurusi, Chimala, Kitunda na Makambako zilijaa wageni, wengine wakilazimika kulala jijini Mbeya.
Sayansi yagongana na imani
Baadhi ya wenyeji katika mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Njombe wanaamini kuwa tukio hilo la kupatwa kwa jua lililotokea juma lililopita katika ukanda huo, linahusika moja kwa moja na hali ya baridi inayoendelea hadi sasa katika mikoa hiyo.
“Hii baridi na upepo wa mwaka huu ni shauri la hii kupatwa kwa jua,” alisikika kijana mmoja jirani na Shule ya Msingi Isisi mjini Rujewa akichangia katika mazungumzo yao kuhusu tukio hilo.
Katibu wa Mila, Wilaya ya Mbarali, Mwanasimtwa Andrew Mwagongo (65) anasema jamii yao iliamini tukio hilo kuwa baya lililowaletea magonjwa na majanga.
“Lilihesabiwa kuwa tukio baya, watoto walizuiwa kutoka nje,” alisema Mwagongo katika mahojiano yake na Raia Mwema nyumbani kwake.
Dk. Noorali Jiwaji wa OUT naye ni miongoni mwa wataalamu wenye kufuatilia matukio ya kupatwa kwa jua na mwezi ambapo anakubali siku hiyo ya tukio kuwepo kwa baridi kali katika dakika zile tatu.
Hata hivyo, anabainisha kuwa hali ya hewa ya baridi inayoendelea hivi sasa katika mikoa hiyo na sehemu mbalimbali nchini ni kutokana na mabadiliko ya tabianchi na haina uhusiano na kupatwa kwa jua.
“Kiwango cha joto kilishuka kwa nyuzi mbili, baridi ilikuwa kali sana katika dakika zile tatu, lakini hii inayoendelea ni suala la mabadiliko ya tabianchi, haihusiani na kupatwa kwa jua,” alisema Dk. Jiwaji ambaye hilo lilikuwa tukio lake la tano kushuhudia.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria tukio hilo wanabainisha kuwa ni fursa ambayo haikutumiwa vizuri kutangaza na kuvutia watalii wa ndani na nje. Watalii kutoka nje ya nchi wengi wamekuja kutokana na uelewa wao kuhusu suala hilo na wengine waliletwa na Kampuni ya UPL Safaris ya jijini Mbeya na uhamasishaji ukifanywa na Waandishi Habari za Mazingira (TAJATI), vyombo vya habari na TANAPA.
Chanzo. Raia mwema
No comments:
Post a Comment