RAIS Jakaya Kikwete, katika kikao cha mwaka cha Umoja wa Afrika (AU), kilichofanyika mwanzoni mwa Juni, mwaka huu, mjini Addis Ababa, Ethiopia, alitoa ushauri kwenye Kamisheni ya Ulinzi na Usalama ya umoja huo, kwamba ili kutafuta suluhisho la kudumu la hali ya kiusalama katika nchi za Maziwa Makuu, upo umuhimu kwa marais Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda na Joseph Kabila wa DRC kuzungumza na makundi ya waasi wanayopambana nayo katika nchi zao.
Makundi hayo ya waasi ni pamoja na Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), kundi ambalo Rais Kagame amekuwa akisisitiza linaundwa na Wanyarwanda waliokimbilia DRC mwaka 1994, baada ya kutekeleza mauaji ya kimbari, wanaojulikana kwa jina la Interahamwe. Mengine ni Allied Democratic Froce (ADF) kwa upande wa Uganda na M23 kwa Rais Kabila wa DRC.
Marais hao hawatakuwa viongozi wa kwanza au wa mwisho kupewa ushauri na Rais Kikwete. Itakumbukwa Rais Kikwete alikuwa mmoja wa viongozi walioshiriki kumshauri Rais Mwai Kibaki wa Kenya akubali kuzungumza na mpinzani wake, Raila Odinga baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007 uliomalizika kwa vurugu na uvunjifu wa amani.
Kibaki alikubaliana na ushauri wa Rais Kikwete, na Kenya ikaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoongozwa kwa mafanikio hadi kufikia ukomo wake baada ya Uchaguzi Mkuu mwingine wa Aprili, mwaka huu.
Marais Marc Ravalomanana na Andry Nirina Rajoelina wa Madagascar walikuja wenyewe Dar es Salaam kuomba ushauri wa namna watakavyomaliza mgogoro wao. Rais Kikwete aliwashauri kwamba ni vyema ikiwa wote wataacha kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao. Walikubali, na ni mategemeo ya wengi kuwa Madagascar patakuwa na amani.
Ushauri wa Rais Kikwete kwa Rais Kagame, haikuwa amri kama ilivyokuwa kwa Kanali Bakar aliyevamia na kuupindua utawala wa Comoro. Ushauri wa Rais Kikwete, ulitegemewa ukubaliwe au ukataliwe, na nina uhakika kwamba Rais Kikwete asingelalamika kama Rais mwenziye angesema wazi kwamba hakubaliani na ushauri ule katika kikao kile.
Kinyume chake, Rais Kagame aliukataa ushauri huo kwa kutoa matusi kwa Rais Kikwete, akidai ushauri huo ni upuuzi mtupu uliotolewa kwa ujinga na mtu asiyefahamu chochote. Hili lilisemwa na Rais Kagame wakati akifunga mafunzo ya maofisa wake wa kijeshi wa ngazi ya juu wa Jeshi la Rwanda, ambapo pamoja na hilo, aliwaeleza maofisa wake hao kufanya kazi zao bila wasiwasi wowote, kabla ya habari hiyo kukaririwa na gazeti la Raia Mwema (gazeti hili) katika magazeti yote ya hapa nchini.
Hata hivyo, kwa wafuatiliaji wa mambo watakumbuka kwamba Rais Kikwete si mkuu wa kwanza wa nchi kutukanwa na Rais Kagame. Mara tu baada ya kuwa Rais wa nchi hiyo, Rais Kagame alitembelewa na aliyekuwa Rais wa Afrika kusini, Thabo Mbeki. Pamoja na mambo mengine, katika mazungumzo yao, Rais Mbeki alishauri kwa Rais Kagame umuhimu wa Rwanda kutengeneza Katiba itakayotoa nafasi kwa wengi kutawala na wachache kulindwa. Baada ya ushauri huo, Rais Kagame alionyesha hasira za ajabu na kutoa matusi kwa Rais Mbeki. Nachelea kuandika hapa matusi hayo kwani nami nitaonekana natukana.
Kwa bahati mbaya sana, ni watu wachache mno, ndani na nje ya Rwanda wanaofahamu vyema historia ya Rais Kagame. Binafsi, naifahamu historia yake walau kidogo. Alizaliwa Rwanda mwaka 1957, na alihamia Uganda kama mkimbizi mtoto akiwa na umri wa miaka miwili tu mwaka 1959.
Ninafahamu pia kwamba Rais Kagame aliishia kidato cha tatu wakati akisoma elimu yake ya sekondari nchini Uganda, katika shule ya Bado, ambayo ilikuwa maalum kwa ajili ya watoto wa viongozi wa juu tangu enzi za ukoloni. Nafahamu kuwa Kagame alijiunga na jeshi la Uganda, chini ya Museveni, na alipanda vyeo hadi kufikia ngazi ya Afisa Mkuu wa Utambuzi katika jeshi hilo.
Hata hivyo, pamoja na elimu yake ndogo hiyo, sikutegemea kamwe ashindwe kutumia kiasi kidogo cha elimu ya uhusiano wa kimataifa, na badala yake akatoka hadharani na kuanza kutoa matusi yanayofanana na yale ya Rais wa zamani wa Uganda, Nduli Iddi Amin Dada, Rais wa Tanzania wa wakati wake, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Kwa kadri ya utafiti wangu wa muda mrefu juu ya Rais Paulo Rutagamba Kagame, kauli yake hii ya kwamba “ushauri wa Rais Kikwete ni upuuzi mtupu uliotolewa kwa ujinga na mtu asiyejua historia ya Rwanda,” hakuitoa kwa bahati mbaya. Rais Kagame alidhamiria.
Alifanya hivyo kwa sababu nyingi, lakini kubwa ni kwamba hata kama asingekuwepo Rais Kikwete kwa sasa, Tanzania kama Taifa na nchi huru, inafahamu ni kiasi gani cha mifupa kwa idadi, ambacho Rais Kageme amehifadhi kwenye makabati yake.
Maneno ya Kagame yamenikumbusha kile kilichokutwa na majeshi yetu kwenye Makao Mkuu ya Idara ya Usalama ya Uganda (State Reserch Bureau) mara baada ya Nduli Iddi Amini kukimbia nchi yake. Nasema, ikitokea leo Kagame akaondoka madarakani kwa namna yoyote ile, tutashuhudia mengi kwenye lile jumba maalum lililoko pale mjini Kigali, alilolipa jina la Pentagon.
Rais Kagame anatambua kwamba hata ombi lake la kutoka kujiunga kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, lilitiliwa shaka na viongozi wengi wa Jumuiya hiyo, lakini ni Rais Kikwete aliyesema mwacheni aje, tutaelewana naye tu. Taarifa za Rais Kagame kutoa maneno ya matusi kwa Rais Kikwete, ziliandikwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Serikali ya Rwanda linaloitwa Times. Hili ndilo gazeti ambalo mara nyingi linatumika kuandika taarifa zinazotayarishwa na Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi hiyo, na hapo ndipo ninapoamini kwamba taarifa hizo ni za kweli tupu na zililenga kusomwa na watu wengi zaidi kwa sababu gazeti hilo liliwekwa kwenye mitandao ya kijamii inayosomwa sana hapa nchini, ambayo ni pamoja na Jamiiforums, facebook, Youtube na twitter.
Wanaomuunga mkono Rais Kagame, wamedai kwamba Rais Kikwete anajivunia nchi kubwa isiyo na maendeleo ya uhakika. Wamedai kuwa Rais Kikwete anamuonea gere Rais Kagame kutokana na kuifanya nchi yake iendelee haraka. Kwamba Rais Kikwete sasa anadai nchi za Rwanda na Burundi zilikuwa sehemu ya Tanganyika. Kuna madai mengi, ambayo naamini, badala ya kumkera Rais Kikwete, yalimshangaza tu. Kwanza kwa mtu mwenye akili ya kawaida, hawezi kukaa akaanza kuifananisha Tanzania na nchi za Rwanda na au Burundi. Nchi hizi zinatofautiana sana. Rwanda ni nchi ndogo kuliko hata mkoa wa Kilimanjaro, ambao ndiyo mkoa mdogo kuliko yote hapa nchini.
Inawezekana Rwanda imeendelea kuliko Tanzania, lakini kwangu, hili ni suala la mtizamo tu. Rwanda inapata misaada mingi kutoka nchi za Magharibi ambayo sina uhakika kama yote inatumika kwa shughuli za maendeleo. Hilo ni kwa upande mmoja, lakini kwa upande mwingine, maendeleo ya Rwanda yamechangiwa kwa kiwango kikubwa na uporaji wa maliasili nyingi za DRC.
Maelezo ya kwamba Rwanda na Burundi zilikuwa sehemu ya Tanganyika yanatumika kama kikolezo tu, kwa sababu ukweli utaendelea kubaki pale pale kwamba nchi hizo zilikuwa ni sehemu ya utawala wa Kidachi katika eneo la mashariki mwa Afrika. Ni suala la kihistoria ambalo tutabaki nalo sote; Tanzania, Rwanda na Burundi.
Ikumbukwe pia kwamba katika shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu vya Rwanda, wanafunzi wanafundishwa kwamba maeneo yote ya mashariki mwa nchi hiyo na DRC, kwa maana ya eneo lote la Kigoma, Karagwe na Ngara kwa upande wa Tanzania, na eneo wanakoishi watu wa jamii ya Wakiga wa Uganda, yalikuwa chini ya miliki za Rwanda.
Historia hiyo inafundishwa kuwa maeneo hayo yaliporwa na nchi zinazopakana na Rwanda kwa upande huo, Tanzania ikiwemo, na kwamba ipo siku maeneo hayo yatarejeshwa kwa nguvu, madai ambayo yanashabihiana na madai ya Nduli Iddi Amin Dada, ambaye wakati wa utawala wake alidai kuwa eneo lote la mkoa wa Kagera, ni sehemu ya Uganda.
Wasomaji wangu, inatupasa tushukuru kwamba Rais Kikwete si mtu wa kulipuka, na hatakuwa na muda wa kujibu hoja hizo za Rais Kagame, ambazo binafsi naziita za ujanja wa mbuni kuficha kichwa kwenye mchanga wakati mwili mzima ukiwa nje.
Pamoja na hayo yote, naomba nimkumbushe mambo machache Rais Kagame, ambayo pengine ameyasahau au hataki kuyakumbuka kwa sababu yanamtia wasiwasi na hofu. Kagame alipoingia madarakani mwaka ule wa 2000, alikuwa na hamu kubwa ya kutaka kuifahamu Tanzania, kama si kutaka kuichafua kupitia kwa waandishi wa habari wetu. Alivialika vyombo vya habari takriban vyote vya nchi hii kwenda kujifunza kile alichoazimia kufanya baada ya kumwondoa madarakani, Rais Pasteur Bizimungu.
Alihakikisha waandishi wa habari kutoka Tanzania wanapewa ‘Guided tour’ ili kuhakikisha kwamba hawadodosi mambo yasiyompendeza Rais Kagame, hata kama yalikuwa yakitendeka kila siku. Waandishi hao, baada ya kutembelea maeneo mbalimbali yalikohifadhiwa mabaki ya mauaji ya kimbari, na hasa yale yaliyopo eneo la Gisozi, mjini Kigali, walimuuliza maswali mengi, yaliyomkera Rais Kagame.
Miongoni mwa maswali yaliyomkera, ni pamoja na yaliyohoji mtu alikuwa na uhakika gani kama mabaki yote yale yalikuwa kweli ni ya Watutsi tu? Je; kulikuwa na ushahidi gani kama Wahutu hawakuuawa? Je; Serikali ilikuwa inajitetea vipi na tuhuma kwamba chama cha Kagame, cha Rwanda Partriotic Front (RPF), kilihusika na mauaji ya kimbari? Na je; ni kwanini Rais Kagame alikuwa mtu anayependa sana kuua?
Nakumbuka maswali hayo yaliulizwa na mwandishi mmoja wa habari ambaye sitaki kumtaja jina wala chombo anachofanyia kazi, lakini lililo wazi ni kwamba kuanzia hapo, mbali na Rais Kagame kutotaka tena kuwa na waandishi wa habari kutoka Tanzania, alianza kuamini kwamba Tanzania inaelewa kile kinachoendelea nchini mwake chini ya utawala wa Rais huyo, ambaye mtumiaji mmoja wa mitandao kutoka Rwanda kwenyewe, amemfananisha na ‘jini subiani’ linalonyonya damu za Wanyarwanda.
Hoja za Kagame kwamba Rais Kikwete haijui historia ya Rwanda, nazo hizi ni za kupuuzwa. Rais Kagame amesahau kwamba hata vikao vilivyoifanya Serikali ya Juvenal Habyarimana ikubali kuzungumza na RPF, na hatimaye chama hicho kukubaliana kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Rwanda, vilifanyika Arusha, Tanzania.
Wakati vikao hivyo vikifanyika, kila Mtanzania, akiwamo Kikwete mwenyewe, alijua kilichokuwa kinaendelea. Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo iliridhiwa na Rais Habyarimana na RPF, haikuwahi kuundwa kwa sababu Habyarimana aliuawa baada ya ndege yake kutunguliwa na maofisa wa RPF, wakiongozwa na kamanda wao, Rose Kabuye, wakitekeleza amri ya Kagame, ingawa hadi leo hataki kukiri hili.
Rais Kagame anajulikana kuendesha nchi yake kama kampuni ya familia yake. Mbali na Rais huyo kuwa na chuki ya muda mrefu dhidi ya Tanzania, hakufurahishwa hata kidogo na hatua ya Tanzania kushirikiana na nchi za Afrika kusini, Malawi na Msumbiji, kupeleka majeshi ya kulinda amani nchini DRC.
Kibaya zaidi, eneo la kioperesheni litakaloangaliwa na majeshi yetu hayo, ndilo ambalo Rais Kagame aliligeuza kuwa ‘shamba la bibi,’ akipora madini, ndilo ambalo amekuwa akiwatuma askari wake kupora kwa kisingizio cha kuwasaka FDLR, na hivyo kupunguza uwezekano wa kupinduliwa na jeshi lake kubwa ambalo halina kazi za kufanya muda wote.
Wale wanaoitwa wabaya wake, na viongozi wa taasisi kadhaa waliotoroka kutoka kwenye Serikali yake, na ambao amewafutia hati zao za kusafiria, na kwa sasa hawana utaifa wowote, wanaendelea kuishi uhamishoni kwa wasiwasi ya kuuawa na mawakala wa Rais Kagame. Kayumba Nyawasa, aliyekimbilia Afrika kusini, ni mfano mmoja wapo. Mara nyingi ameponea chupuchupu kuuawa.
Rais Kagame anafahamu kwamba nchi yake inaongoza kwa kuwa na viongozi wengi wanaotoroka na kwenda kuishi uhamishoni. Hajiulizi ni kwanini, pamoja na majigambo ya maendeleo nchini mwake, wale waliokuwa wanaitwa Wasaja au Wanyarwanda wa kabila la Kitutsi aliotoka nao Uganda, wamekimbia na kumwacha yeye na James Kaberebe, ambaye naye kwa udikteta huu wa Kagame, anangoja siku yake. Je; wako wapi marafiki zake wa karibu, kina Rudasingwa, Wilson Rutaisire, Sendashonga na Kalegaya, ambaye alikuwa mshiriki wa Kagame katika kampuni yake ya Tri-Star, iliyokuwa ikiuza madini ya Coltan kutoka DRC?
Nihitimishe makala haya kwa kumwambia Rais Kagame kwamba hakuwa na sababu ya kutoa maneno yale ya kejeli kwa Rais mwenziye. Angeweza kupuuzia ushauri ule na kila kitu kikaishia hapo. Nimkumbushe pia kwamba asije akachukulia ule usemi wa Kihindi wa kwamba simba mwenda pole, iko gonjwa. Binafsi, na kwa masikio yangu, nimewahi kuwasikia mara kadhaa baadhi ya wanajeshi wa Rwanda wakisema wanaweza kujipima ubavu na Jeshi la Tanzania. Kwa kuwa nimemfananisha Rais Kagame na Nduli Iddi Amin, hofu yangu ni kwamba anaweza akajenga kweli wazo la kutaka kujaribu kutikisa kiberiti, kwa kujaribu kuivamia Tanzania ili aone nguvu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Kwa hakika kabisa, uamuzi kama huo ataujutia.
Nasema pamoja na Rais Kagame kujiona ndiye Rais mwenye mawazo mazuri ya kuijenga Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini namuomba asiupuuze ushauri wa wengine hata kama anauona ni wa kipuuzi, kwa sababu hakuna upuuzi ulio upuuzi mtupu. Ipo siku ataomba msaada na ushauri kwa huyo aliyemtukana. Uchumi wake anaojisifu kuujenga, haujashuka kutoka mbinguni, bali umetokana na ushirikiano na nchi jirani zake Tanzania ikiwamo. Ndiyo maana nalazimika kuuliza; hivi huyu Rais Kagame ni nani hadi amtusi Rais wetu?
Chanzo:- Raia Mwema
Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Jumuia ya Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment