Karibuni sana.”
“Asante,” waliitikia pamoja.
“Karibu mzee,” mzee Mukti alimkaribisha Thabit aliyeonekana kapendeza kwa fedha.
“Asante mzee wangu.”
“Jamani mna tatizo gani?” mzee Mukti alijifanya kama ndiyo siku ya kwanza kuonana na watu wale.
“Mzee wangu tuna tatizo, kuna vitu vimetutokea leo asubuhi ambavyo vinaonekana si vya kawaida,” Subira alianza kutoa maelezo.
sasa endelea...
“Eti mzee kuna nini?” mzee Mukti alimgeukia Thabit hakutaka Subira azungumze.
“Mzee wangu leo nimetokewa na jambo la ajabu baada ya moto wa ajabu kuteketeza duka langu lenye thamani ya mamilio ya fedha. Kwa kweli mpaka sasa nimechanganyikiwa sana sijui tatizo lile linatokana na nini.”
Mzee Mukti alijifanya akipiga ramli ya uongo kwa vile kila kitu alijua kisha alisema:
“Hapa panaonesha kuna kijicho kwa watu wasiopenda maendeleo yako ambao ndiyo wamefanya mchezo huu.”
Ilibidi atengeneze uongo kuogopa kumwambia ukweli kuwa aliyefanya vile ni jini anayetaka kumtia umaskini baada ya kuchukuliwa mumewe. Aliamini angemwambia vile lazima angekumbuka ahadi aliyomuahidi mkewe jini Nargis kwamba hatamsaliti akiwa mbali naye.
“Nani aliyefanya hivyo?” Thabit alitaka kujua.
“Kwa kweli hapa kuna giza hawaonekani vizuri, lakini najitahidi kuliondoa giza ili tuwajue.
“Kwa hiyo shida yao nini?”
“Kutaka kukurudisha katika umaskini.”
“Kwa hiyo mzee utatusaidiaje?”
“Kwa vile tatizo nimeshaliona nitazindika mali zako zote pamoja na nyumba yako kuhakikisha hupotezi tena mali zako. Na zoezi lifanyike usiku wa leo pia nitakupeni dawa za kuwalinda wote na watu hao wabaya.”
“Na mali zilizopotea zitapatikana?”
“Ile haitapatikana ila iliyopo haitapotea tena.”
“Mmh! Nitashukuru.”
“Kwa hiyo kuna dawa nitawapa mnywe na kuoga pamoja, kisha nitawapa zindiko.”
“Hakuna tatizo.”
Baada ya kusema vile mganga aliandaa tiba ili baadaye waende kwenye kazi ya kuzindika maduka kwa kulashia kwa vile kazi alikwisha imaliza toka jana yake usiku.
Mzee Mukti aliwaandalia dawa ambayo ilikuwa ya aina mbili moja ya kumlinda Thabit na majini na nyingine kumsukumia kwa Subira ili ndoa iwahi mapema.
Baada ya zoezi lile waliondoka mpaka kwenye maduka na mzee Mukti alijifanya yupo bize kumbe uongo alikuwa akipaka maji tu. Baada ya zoezi ambalo halikuchukua muda mrefu walirudi nyumbani. Mzee Mukti siku hiyo alilala nyumbani kwa Thabit na kuongeza nguvu kwenye zindiko lake la awali usiku uleule.
Baada ya zoezi lake alipewa chumba kizuri akalala, katikati ya usingizi alishtuliwa na ndoto iliyomtisha, aliota bahari yote ikiwaka moto. Alijiuliza ndoto ile ina maana gani, kwani kila alipoangalia kwenye rada zake hakuona kitu kingine zaidi ya moto mkubwa umetanda baharini.
Baada ya kushindwa kutambua ndoto ile aliachana nayo na kuendelea kulala akisiburi taarifa yoyote kutokana na njozi yake.
Usiku mkubwa jini Hailat dada wa Nargis pamoja na uchovu alitoka chini ya bahari na kwenda kwenye meli iliyokuwa imebeba Makontena ya bidhaa mbalimbali yakiwemo ya Thabit. Alipofika aliyachagua ya Thabit na kuyawasha moto wa kijini na kurudi chini ya bahati kumpelekea taarifa mama yake. Alipofika alimueleza mama yake kazi aliyomtuma aliifanya.
“Vipi hukukutana na vikwazo?” mama yao Malkia Zabeda aliuliza.
“Walaa, kazi ilikuwa nyepesi kuliko ya madukani.”
“Basi kapumzike mwanangu na jambo hili libakie siri yetu.”
“Hakuna tatizo.”
“Ila bado kuna kazi nyingine nitakupa.”
“Juu ya Thabit?”
“Ndiyo, nina imani hiyo ukiifanya japo utakutana na upinzani mkubwa lakini utaifanikisha. Mdogo wako Nargis kwa sasa hawezi kutuelewa lakini baadaye atatushukuru.”
“Na kuhusu yule mganga?”
“Achana naye, huyo atuhusu alichofanya ni kazi.”
“Nilitaka kula naye sahani moja hawezi kunitia makovu ya ukubwani.”
“Achana naye inaweza kumbumbulua Nargis.”
“Sawa mama nimekuelewa.”
Kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana waliagana kila mmoja aliingia chumbani kwake kulala.
Kama kawaida meli ilitia nanga katika bandari ya Dar es Salaam, baada ya taratibu zote mizigo ilianza kupakuliwa na kuwekwa sehemu kwa ajili ya kuchukuliwa na wenyewe. Vijana wa Thabit nao walikuwepo na magari makubwa ya kubebea mizigo ili kuisambaza.
Magari yalibeba mizigo kama kawaida na kuisambaza kwenye maduka yote ikiwemo kutenga makontena mawili kwa ajili ya duka la Posta lililounguzwa vitu vyake na moto wa ajabu. Baada ya kufikishwa zoezi la kufungua makontena lilianza mara moja. Msimamizi alishtuka kuona majivu ndani ya kontena bila bidhaa zilizoagizwa.
Itaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment