Sasa Beka alianza kuwa mkorofi f’lani hivi kwa mkewe baada ya kuwaza yake…
“Yaani mi nakuita unasema nini?”
“Ulitaka niitikiaje?”
“Kwani siku zote unaitikiaje?”
“Hebu niambie ulichoniitia…”
JIACHIE NAYO SASA…“
Oke, ni kwa nini umenisaliti kwa dada yangu?”
“Hilo swali jijibu mwenyewe.”
“Kwa nini?”
“Kwa sababu unajua ni kwa nini?”
“Mimi sijui ndiyo maana nimekuuliza wewe.”
“Na mimi najua wewe unajua ndiyo maana nimesema ujijibu mwenyewe,” alisisitiza Beka kwa sauti isiyotaka utani.
“Mimi sijui, ila kusema ukweli nimeshtuka sana.”
“Hata mimi nilikuwa nashtuka sana.”
Aisha aliamua kukaa kimya huku akiwaza mengi kichwani. Hakumwambia mumewe kwamba kesho yake anakwenda kijijini ameitwa na wazazi.
***
Asubuhi na mapema, Aisha alitoka kitandani, akaenda kuoga. Aliporudi alijiandaa, akatungua mkoba wake na kuweka baadhi ya nguo. Beka alishuhudia tukio hilo lakini hakumuuliza.
Aisha alipomaliza, alibeba begi na kuliweka begani ndipo akasema…
“Mimi nasafiri, nakwenda nyumbani wazazi wameniita.”
“Oke,” alijibu kwa mkato Beka. Hakuuliza kuna nini wala mbona unaniambia kwa kunishtukiza!
Aisha alipotoka alikuta mlango uko wazi, akajua dada yake naye ameshatoka kitambo. Kila hatua tano mbele alitupa macho kama atamwona dada yake, lakini haikuwa hivyo.
***
Mabasi stendi kuu ya kwenda kijijini kwao yalikuwa mengi lakini Aisha alichoomba asipande basi moja na dada yake hivyo kabla ya kukata tiketi alichungulia ndani kwanza. Alipata basi ambalo aliamini dada yake hakupanda.
***
Beka aliamka saa moja juu ya alama, akatoka na kuangaza huku na kule. Alibaini shemeji yake naye alitimua zake baada ya kwenda chumbani kwake na kumkosa. Hata begi lake halikuwepo!
“Liwalo na liwe. Atakaloamua Aisha ndilo hilohilo.
Yeye ni mke wangu ni kwa nini alikuwa ananikatalia kunipa tendo la ndoa, anadhani ningeishije. Naamini hilo ndilo limechangia mimi kufanya vile,” alisema moyoni Beka huku akirudi chumbani kulala kidogo.
Ni ukweli usiopingika kwamba, Beka amekuwa na wakati mbaya kwa mkewe kuhusu unyumba, mara nyingi amekuwa akimkatalia hata kwa miezi mitatu bila sababu za msingi. Pamoja na kufanyiwa yote hayo, Beka hakuwahi kumsaliti mkewe.
Kuwepo kwa dada yake ndani ya nyumba na tabia yake ya kushobokea ndiko kulisababisha Beka ajikute akitumbukia kwa mtego wa mapenzi kwa shemeji yake huyo.
***
Aisha ndiye aliyetangulia kufika nyumbani kwao kijijini na kumkuta mama yake amelazwa kwenye zahanati ya kijiji hicho kwa matatizo ya presha.
Baada ya kupata taarifa za tukio la usaliti alilolifanya binti yake mkubwa kwa mume wa mdogo wake alipata msongo mkubwa wa mawazo na kusababisha presha ya kushuka.
Aisha alishangaa kukuta dada yake hajafika. Alimwambia baba yake kwamba yeye dada mtu ndiye aliyeanza kutoka nyumbani asubuhi. Wakiwa wanajadili, dada mtu aliingia…
“Shikamoo baba.”
“Marahaba,” aliitika mzee huyo bila hata kumuuliza za safari kama alivyofanya kwa Aisha.
Dada mtu huyo alipitiliza hadi ndani akatua begi lake. Aliwauliza wadogo zake wengine aliko mama yake…
“Mama amelazwa hospitali.”
“Anaumwa nini?”
“Presha.”
Dada mtu huyo alikwenda kwenye zahanati hiyo ambayo anaijua na kumkuta mama yake kidogo ana nafuu. Pia alimkuta Aisha, maana wakati yeye anafika nyumbani Aisha alikuwa anatoka.
“Shikamoo mama,” alimsalimia lakini mama mtu huyo alimtumbulia macho tu kama anayemsuta kwa tabia yake chafu aliyoifanya…
“Pole mama,” alisema.
Lakini bado mama mtu huyo hakuitikia zaidi ya kutoa macho.
Ilimbidi dada mtu huyo ageuke kurudi nyumbani huku akiwa anamwaga machozi mwenyewe. Alianza kuhisi hali ni mbaya sana nyumbani hapo.
***
Jioni ya saa moja kulikuwa na kikao nyumbani na ni baada ya mama yao kutoka zahanati akiwa anajisikia nafuu sana.
Baba yao ndiye aliyeanza kuongoza kikao hicho huku akionekana kutetemeka midomo kwa hasira…
“Ime,” alianza kusema baba mtu huyo kwa kumtaja jina dada wa Aisha. Wakati huo watoto wote walitakiwa kuingia ndani vyumbani mwao…
“Abee baba.”
“Ni nini umekifanya kwa mdogo wako Dar es Salaam?”
Dada mtu huyo akikaa kwa muda wa kama dakika moja nzima kabla ya kusema chochote halafu ndipo akaamua kusema…
“Wazazi wangu, mimi nakiri kutenda kosa. Nimetembea na shemeji yangu Beka. Ni kweli mdogo wangu alitufumania.”
Ukimya wa sekunde kadhaa ulimfanya baba mtu huyo kuendelea…
“Ni kwa nini uliamua kufanya kosa kubwa kama hilo?”
Dada mtu huyo akatulia tena kidogo kisha akafunguka…
“Wazazi wangu, kusema ule ukweli nilijikuta nikiangukia kwenye dhambi ile baada ya shemeji mwenyewe siku moja kunishitakia. Aliniambia shemeji afadhali umekuja, mdogo wako amekuwa akinitesa sana kwenye ndoa.
“Mimi ni mume wake lakini anadiriki kunikatalia kunipa unyumba. Inaweza kupita hata miezi miwili mpaka mitatu hajanipa unyumba. Nilishtuka sana kusikia hivyo.”Baba mtu na mama mtu walionekana kushtushwa na kipengele hicho, wakamgeukia Aisha…
Itaendelea
Chanzo Globalpublishers
No comments:
Post a Comment