Aisha aliinamia chini. Aliwaza ajibu nini, ni kweli au si kweli?
“Nakuuliza wewe Aisha. Na kama ukisema si kweli nampigia simu mumeo naye aje hapa ili nimsikie yeye anasemaje,” alikuja juu baba huyo.
“Ni kweli baba, lakini naomba samahani sana kwa hilo.”
“Ni kweli kwamba?” mama mtu alidakia sasa…
“Namnyimaga unyumba mume wangu.”
“Kabisa kabisa… na unadiriki kusema ni kweli bila aibu Aisha?” alizidi kushangaa mama mtu.
“Enhe, endelea wewe,” sasa hapo baba mtu alielekeza kwa dada mtu aendelee kusema…
“Kutokana na hali hiyo wazazi wangu hasa ikizingatiwa kwamba na mimi nilikuwepo pale bila mwanaume, ubinadamu ukanipata. Kwangu nilihisi kumwonea huruma shemeji yangu kwani ni kijana bado…”
“Uliwahi kumwonya mdogo wako kuhusu tabia hiyo na madhara yake?” aliuliza baba.
“Niliwahi ndiyo. Nilimsema akasema nimwachie na maisha yake.”
“Eti ni kweli Aisha aliwahi kukuonya?”
“Ni kweli.”
“Ni kweli ulimjibu akuachie na maisha yako?”
“Ndiyo.”
“Haa! Kwanza hiyo tabia nani kakufundisha mwanangu Aisha. Mumeo unamnyima unyumba na wewe ndiyo mke, unataka iweje? Aisha unataka sisi wazazi tuseme siri zetu kwenu nyie watoto siyo?” Baba mtu alifoka.
Mama naye akadakia kwa hasira hasa alipokumbuka kwamba aliumwa ghafla…
“Mimi sijawahi hata siku moja kumwambia baba yenu sitaki, hata siku moja. Wewe Aisha umepatia wapi hiyo nguvu mwanangu?”
Dada mtu alimfuata mama yake kwa magoti na kumshika miguu akimwomba asiendelee kusema maneno hayo kwao kama watoto…
“Mama chondechonde, hayo maneno ni laana kwetu mama, usiyaseme.”
“Si ndiyo mnataka!”
Baba mtu alisimama akaingia ndani, chumbani…
“Haya, baba yenu kama hivi ameondoka. Haya yote shauri yenu. Sijui mkoje?” alipomaliza kusema hayo naye akasimama na kuondoka kumfuata mume wake.
Nje walibaki Aisha na dada yake. Walikuwa kimya, hakuna aliyejua nini kifuatie. Ikawa haijajulikani nani anazibeba lawama zote sasa.
Aisha alimwangalia dada yake, akasimama na kuingia ndani. Dada mtu alibaki kwa muda hapo akiwaza, akaenda mbali kidogo na nyumba akapiga simu kwa Beka. Simu hiyo ilipokelewa haraka sana na Beka…
“Haloo…”
“Haloo, mambo shemeji?”
“Poa, vipi huko?”
“Huku poa tu. Mwenzangu nikwambie kitu…”
“Niambie shemeji.”
“Si nimembwaga mkeo huku, kalowa kama katembea kwenye mvua, we acha tu.”
“Ilikuwaje?”
“Kwenye kikao, nikasema yote kisa cha yeye kukunyima unyumba, wazazi wakashtuka sana tena sana. Wakamuuliza alifundishwa na nani kumwambia mume sitaki?”
“Acha bwana…”
“Eee, baba amekasirika hadi akatoka kikaoni, mama naye akaondoka. Hivi hapa nipo nje naongea na wewe.”
“Da! Safi sana shemeji, sikujua kama ungeweza kutumia engo hiyo ya kuninyima unyumba.”
“Wee, unanijua unanisikia! Na mimi nikasema nitumie engo hiyohiyo.”
“Safi sana, nitakutafutia zawadi mama.”
“Nitaipataje?”
“Kwani hurudi?”
“Mh! sidhani, we unaamini naweza kuruhusiwa kuja Dar kwa Aisha? Labda nije kivyangu.”
“Basi siku ukija kivyako nitakuwekea zawadi yako,” alisema Beka.
“Baadaye shemeji, naona mlango unafunguliwa, sijui nani anatoka, nitakupigia,” alisema dada mtu na kukata simu.
Aliyetoka ni mama mtu…
“We huingii ndani kulala?” aliuliza mama.
“Naingia mama.”
Mama akatoka nje kabisa akamwambia kwa sauti ya chini…
“Baba yako amesema ulichofanya si kizuri, lakini alichofanya mdogo wako kwa mumewe ni kibaya sana. Amekasirishwa sana na mdogo wako. Amesema anaweza kusababisha ndoa kuvunjika na yeye hataki kusikia hivyo.”
Kwa mbali dada mtu huyo akaanza kuwaza kuhusu ndoa yake maana tangu amepigwa chini na mumewe hakuwaambia wazazi wake…
“Mimi mama sijafanya kwa nia mbaya.”
“Hapana, ulipoona shemejiyo kakwambia hivyo na umemshauri mdogo wako hataki, ungetuletea habari sisi.”
“Nisamehe mimi mama.”
Mara mlango ukafunguliwa, Aisha akatoka huku akimwaga machozi
Inaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment