Magari yalibeba mizigo kama kawaida na kuisambaza kwenye maduka yote ikiwemo kutenga makontena mawili kwa ajili ya duka la Posta lililounguzwa vitu vyake na moto wa ajabu. Baada ya kufikishwa zoezi la kufungua makontena lilianza mara moja. Msimamizi alishtuka kuona majivu ndani ya kontena bila bidhaa zilizoagizwa.
Hakuamini macho yake, alifungua lingine hali ilikuwa ileile, ilibidi apigiwe simu Thabit kuelezwa kilichoonekana kwenye kontena badala ya bidhaa walikutana na majivu kama yale yaliyokutwa dukani kwake.
Taarifa ile ilimfanya Thabit kwenda haraka kujionea, alipofika alioneshwa mali iliyoteketea kwa moto wa ajabu. Lilikuwa pigo jingine, hakuamini alikwenda kwenye makontena yote hali ilikuwa ileile. Ilikuwa mali ya fedha nyingi sana aliamini kabisa wamemmaliza.
Kutokana na mshtuko alianguka chini na kupoteza fahamu, ilibidi akimbizwe hospitali. Alipimwa vipimo vyote lakini ugonjwa haukuonekana. Upande mmoja wa mwili wake ulipooza ghafla. Lilikuwa pigo mujarabu lililomchanganya sana, Subira naye alichanganyikiwa na kumpigia simu mzee Mukti na kumueleza kilichotokea.
“Mzee wangu mbona kila siku matatizo yanazidi?”
“Kilichotokea kilikuwa nje ya uwezo wangu, ndoto ya kuungua vitu ndani ya maji niliiona lakini sikujua ilikuwa ina maana gani.”
“Kwa nini hukuzuia?”
“Ilikuwa vigumu kama ningeingia kwenye ufalme wao wa maji kwa ajili ya vita nisingerudi salama, wangenipoteza kwa njia yoyote.”
“Sasa tutafanyeje maana hali na mpenzi wangu ni mbaya sana?”
“Atapona ni mshtuko tu.”
“Nini hatima yetu?”
“Ulichelewa kunijulisha tungeweza kuanza mchakato mapema ili kuokoa mali zenu.”
“Mmh! Nitaolewa kweli?”
“Utaolewa, kuna dawa utaletewa na kuitumia kumpa itamsaidia.”
“Sawa, na mali iliyobakia itasalimika kweli?”
“Ile ipo salama wala usihofu.”
“Sawa basi nasubiri.”
Mzee Mukti ilibidi aangalie ugonjwa wa Thabit tatizo nini, jibu lilimtisha kuonesha bila kazi ya ziada Thabit atakuwa mlemavu milele. Aliamini dawa zake zote zisingeweza kumtibu ilikuwa lazima asafiri kwa siku mbili ili afuate dawa ambayo nayo ilikuwa bahati nasibu japo ilionesha kila dalili za kulemaa kwa Thabit.
Ugonjwa wa Thabit ulifanya iwe furaha kwa Hailat na mama yake.
“Mama Thabit kwisha.”
“Kwa nini?”
“Kazi uliyonituma imeleta matokeo mazuri.”
“Imekuwaje?”
“Amepooza upande mmoja si wa kupona leo kesho.”
“Sasa tuone kama yule mwanamke ataendelea kuwa naye.”
“Halafu yule mganga anajitia kiherehere kumtibu, tumshughulikie nini?”
“Mwache amtibu, lakini atachukua muda kupona na muda wote huo lazima yule mwanamke atamkimbia.”
“Kama hivyo sawa.”
Nargis akashangaa kuona mama na dada yake wakinyamaza ghafla baada ya kumuona. Ilimshtua sana na kuamini kuna kitu juu yake walikuwa wakimteta. Aliwapita bila kuwasemesha lakini moyoni alijawa na wasiwasi juu ya kikao kile cha faragha cha mama yake na dada yake. Alizunguka na kujificha nyuma ya mlango.
Alichokisikia roho ilimuuma sana na kuona jinsi gani familia yake imeamua kwenda kinyume na makubaliano juu ya mumewe Thabit kumuacha kama alivyo. Hakutaka kusema chochote alijipanga kurudisha kila kitu kilichopotea kwa mpenzi wake bila kujua kama akirudi duniani atakubaliwa na mumewe au atatoswa.
Alijipanga kuondoka usiku kwenda kurudisha kila kitu cha mumewe kilichopotea kuanzia dukani mpaka kwenye makontena. Naye aliamua kufanya kwa siri ili familia yake wasijue kinachoendelea. Usiku baada ya kuwaweka vizuri wanawe alitoka chini ya bahari na kwenda moja kwa moja nyumbani kwake.
Alipokaribia kwenye nyumba ya Thabit aliona bahari, japo moyo ulimuuma nyumbani kwake kuwa kwenye hali ile.
Alijaribu kuingia katika umbile la kijini joto la maji ya moto lilimzuia, akalazimika kurudi katika umbile la kibinadamu na kuteremka kwa mbali kidogo. Aliweza kuiona nyumba yake.
Alitembea taratibu kuelekea kwenye nyumba ile, alipokaribia moto mkubwa ulionekana ukiizunguka nyumba yake. Alijua nyumba imezindikwa ili yeye na majini wote wasiingie katika nyumba ile. Kwa vile shida yake ilikuwa kurudisha mali iliyopotea aliondoka hadi dukani.
Kama kawaida alijirudisha katika umbile la kijini na kuruka kwenda sehemu ya maduka. Alipokaribia alijirudisha katika umbile la kibinadamu na kuweza kusogea kwenye duka. Aliusogelea ukuta wa duka na kuushika, akafumba macho na kuvivuta vitu vilivyopotea.
Baada ya muda aliviona vitu vyote vilivyokuwemo kabla, alivivuta taratibu mpaka kila kitu kilirudi kama zamani. Alitabasamu kuona mali ya mpenzi wake imerudi na duka lilijaa kama mwanzo.
Baada ya kumaliza zoezi lile alijirudisha katika umbile la kijini na kuruka hadi kwenye makontena yote na kuyashika kila moja na kurudisha kila kitu. Baada ya hapo alikwenda hospitali alipokuwa amelazwa mumewe.
Kwa vile hakukuwa na zindiko aliingia katika umbile la kijini na kuwapita watu bila kumuona.
Baada ya kuingia kwenye wodi aliyokuwa amelezwa mumewe, wakati huo hakukuwa na mtu mwingine chumbani.
Alimuangalia kwa huzuni na kuona ubaya wa viumbe kutaka kumuua mumewe bila sababu.
Akiwa amelala kitandani alipotaka kumshika alipigwa na shoti kama umeme na kumrusha upande wa pili. Alijua tayari na mumewe amezindikwa ili asiwe naye karibu. Hakuondoka alisimama pembeni ya Thabit aliyekuwa amelala hajitambui.
Kutokana na uchungu moyoni alijikuta akilia na machozi kumtoka, kwa vile alikuwa ameinama machozi yake yalitua kwenye paji la uso wa mumewe. Alishangaa kumwona akibadilika rangi mchanganyiko huku mwili ukitikisika kisha alirudi katika hali ya kawaida na mwili ulitulia.
Itaendelea wiki ijayo.
Alimuona Thabit akifumbua macho na kupepesa kasha alijinyoosha kuonesha yupo sawa. Nargis alitaka kumsemesha lakini hakutakiwa kufanya vile kwa vile sicho kilichompeleka na muda ule.
Aliamini kila alichokipanga kimekwenda kama alivyotaka aligeuka na kuondoka na kumuacha mumewe akiwa hajambo na kuamini taarifa atakayoisikia juu ya mali zake kurudi atamuongezea furaha.
Kwa vile alikuwa ametoka usiku sana aliwahi kurudi chini ya bahari kabla familia yake haijagundua kitu.
Inaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment