Subira alimweleza kilichotokea muda mfupi, mumewe kumshangaa na kumwona si mkewe. Mzee Mukti aliamini kazi aliyotumwa na Nargis ilikuwa imekwisha, alishusha pumzi na kusema:
“Mmh! Mambo mazito, inaonekana uwezo wangu umefikia mwisho.”
“Mungu wangu sasa itakuwaje?”
ENDELEA...
“Kwani anasemaje?”
“Kama nilivyokueleza anashangaa hata picha za harusi yetu na kuuliza ile picha kama ni yake huoni kama naumbuka mwenzio?”
“Mmh! Kweli kazi ipo.”
“Mzee wangu fanya uwezavyo ili mambo yawe sawa nakuahidi kukupa chochote ukitakacho.”
“Nina ushauri mmoja.”
“Ushauri gani?”
“Nakuomba umuachie mume wake?”
“Eti nini?” Subira alishtushwa na kauli ya mzee Mukti.
“Njia rahisi ya kumaliza suala hili ni kuachana na mumewe lakini zaidi hapo nauona mwisho wake ni mbaya.”
“Sikubali nimeishapoteza fedha nyingi kwa ajili ya kulinda ndoa yangu, lazima niipiganie,” Subira hakukubali kirahisi.
“Lakini si unajua Thabit ni mume wa Nargis?”
“Hata kama, mimi ni mwanadamu na yule ni jini hivyo mwenye nafasi kubwa ni mimi kwa vile ndoa ya halali ni mwanadamu kwa mwanadamu.”
“Unajua mwenye haki ni huyo jini na sasa hivi ana nguvu mara mbili ukishindana naye utakufa unajiona.”
“Bora nife lakini sikubali lazima nipambane.”
“Nakuhakikishia kama kwangu umeshindwa hakuna sehemu yoyote utakapopata msaada.”
“Siamini, wewe si mganga wa mwisho nitahakikisha namrudisha mikononi mwangu,” Subira alisema kwa hasira.
“Sawa, lakini kwa ushauri wangu achana na mume wa Nargis yatakukuta makubwa.”
“Leo ndiyo umeyaona hayo?”
“Subira acha ubishi hata huo utajiri ni wa huyo mwanamke.”
“Hakuna ni wa Thabit si wa jini wako.”
“He! Ameisha kuwa jini wangu! Subira ninayokueleza haya ni kwa ajili ya kukupenda, lakini kama huyo jini angekuwa na roho mbaya angeweza kutuua wote.”
“Umejuaje?”
“Kuna siri nzito nilikuficha juu ya yule jini, ndiye aliyerudisha mali zilizopotea na ndiye aliyemponya Thabit kwa vile ni mume wake. Amekosa kuniua zaidi ya mara nne na kunieleza kama ninataka usalama wangu na wako basi tumrudishe mumewe mikononi mwake la sivyo atatupoteza wote.”
“Mzee Mukti, wewe si ulinieleza kuwa wewe ni kiboko ya majini?”
“Ni kweli lakini imeonekana Nargis ana nguvu za ziada tofauti na mwanzo tulivyomfanya.”
“Ndiyo maana nikasema wewe si mganga wa mwisho kama uwezo wako umeishia hapo wapo wenye kukuzidi.”
”Sawa, lakini nakuomba kwa usalama wako achana na Thabit kwa vile mwenye mali amerudi kama alikulaza kwenye kaburi anaweza kukufanya chochote anachotaka.”
“Sikubali nipo radhi kufa lakini nimrudishe mume wangu.”
“Kila la heri.”
Subira akiwa amechanganyikiwa alibeba mkoba wake bila kumuaga mumewe na kutoka nje. Alikumbuka kuna mganga mmoja anasifika sana maeneo ya Bunju, aliingia kwenye gari na kuondoka. Alipofika Bunju hakujua yupo wapi, ilibidi ampigie shoga yake ambaye alikuwa akiwafahamu waganga kila kona.
“Nenda mpaka Bunju mwisho kisha ulizia Moboja, ni maarufu sana.”
Baada ya kuelekezwa vile alisogea pembeni ya barabara kulikokuwa na vijana wenye bodaboda. Aliteremsha kikoo na kumwita mmoja aliyekuwa amesimama pembeni.
“Samahani kaka naomba nikuulize.”
Yule kijana alisogea hadi kwenye gari la Subira na kuuliza:
“Unasemaje Sister?”
“Eti unamjua mganga anayeitwa Moboja?”
“Si yule anakaa mpakani?”
“Hata najua, kuna mtu kanielekeza anakaa Bunju.”
“Mimi namjua yule wa mpakani?”
“Labda ndiye yeye si mwanamke?”
“Ndiyo.”
“Basi atakuwa yeye.”
“Basi nenda mpaka ukikaribia daraja linalotenganisha Bunju na Bagamoyo, kata kulia kuna njia ndogo lakini gari linafika fuata barabara hiyo mpaka mbele utaona nyumba ina kitambaa chekundu juu ya mti kama bendera ndipo hapo.”
“Asante kaka yangu,” Subira alisema huku akimpatia elfu mbili kisha aliwasha gari na kuondoka kuelekea kwa mganga.
Alifuata barabara mpaka alipokaribia kwenye daraja alikata kulia na kuifuata njia alipofika mbele aliona nyumba yenye bendera nyekundu. Aliamini ni pale alipoelekezwa alisimamisha gari. Aliteremka na kuelekea kwenye nyumba kwa kuingia mlango wa uani ambako alikuta kuna wagonjwa waliokuwa wakipata matibabu na wengine wakiwa kwenye foleni ya kumuona mganga.
Baada ya kuwasalimia alikaa pembeni kusubiri zamu yake, baada ya dakika arobaini aliitwa ndani kwenda kuonana na mganga. Baada ya kukaa na kusalimiana alitulia kumsikiliza.
“Karibu.”
“Asante.”
“Una tatizo gani?”
“Ndoa yangu imeingia katika matatizo baada ya jini mmoja kutaka kumchukuwa mume wangu. Naomba msaada wako ili kuhakikisha mume wangu hachukuliwi kwa gharama yoyote. Tena ukifanikisha kumbakisha mume wangu nitakupa zawadi kubwa ambayo hutaisahau maishani mwako.”
Baada ya kumweleza mganga alitulia kwa muda na kuchukuwa mtandio mwekundu na kujifunika usoni ili ampigie ramli. Aliwasha udi na kuufusha kisha aliuweka chini ya kitambaa na kuvuta moshi wake baada ya muda alisikika akiguna peke yake na kusema kwa sauti nyembamba.
“Ewe mwanadamu una shida gani?”
“Nataka kuchukuliwa mume wangu.”
“Mbona unasema uongo?”
“Kweli huu ni mwaka wa tano nipo ndani ya ndoa yangu.”
Inaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment