Hakimu mmoja wa mahakama maalumu ya kusimamia kesi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 ameulaumu uongozi wa kanisa katoliki kwa kuwalinda washukiwa waliohusika ambao ni viongozi wa dini.
Katika mahojiano aliyoyafanya na gazeti la "Badisches Tagblatt" la Ujerumani, jaji Wolfgang Schomburg amewanyooshea viongozi wengi kidole: Schomburg aliyekuwa sehemu ya jopo la majaji lililosimamia kesi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 amewataka mapadri wa kikatoliki waliohusika katika mauaji hayo ya kinyama wafikishe mahakamani. Schomburg ameukosoa uongozi wa kanisa katoliki, Vatikan, kwa kuwalinda mapadri hao ambao wanapaswa kufikishwa mbele ya sheria.
Ni kweli kwamba vipo visa ambapo uongozi wa kanisa katoliki uliamua kuwapatia hifadhi viongozi wa kiroho ambao walihusika moja kwa moja kwenye mauaji ya kikatili.
Mmoja wao ni padri Wenceslas Munyeshyaka. Yeye mwaka 1994 alibeba bunduki kama mwanajeshi na kupanga njama na waasi wa Kihutu. Waasi hao waliwaua mamia ya watu waliokuwa wametafuta hifadhi ndani ya kanisa la padri Munyeshyaka. Padri huyo baadaye alihamia Ufaransa. Mahakama moja ya nchini Rwanda ilimhukumu adhabu ya kifungo cha maisha lakini kanisa katoliki nchini Ufaransa lilimtetea na kusema kuhukumiwa kwa Munyeshyaka kwa mauaji ya kimbari si sababu ya kumfanya asiendelee na kazi yake ya upadri.
Mapadri wafichwa Ulaya
Padri Munyeshyaka hayupo pekee yake. Mapadri na masista waliofahamika kuhusika katika mauaji ya Rwanda walipelekwa Ulaya na kupatiwa hifadhi huko. Miongoni mwao alikuwa Padri Athanase Seromba aliyeruhusu kanisa lake libomolewe likiwa na Watutsi 2,000 ndani. Wale walioponea walifyatuliwa risasi na kuuliwa. Kanisa Katoliki lilimsaidia kukimbilia Italia na hata kuhakikisha kwamba anapwea jina jipya na pasipoti mpya.
Mbali na viongozi hao wa dini, bado wapo wanasiasa na wanajeshi waliohusika ambao kamwe hawakuwahi kufikishwa mahakamani au kufunguliwa mashtaka. Jaji Schomburg amekumbusha kuwa bila kuwepo kwa mahakama maalumu ya Umoja wa Mataifa, watu wengi waliosababisha maafa ya Wanyarwanda wapatao 800,000 wangeweza kuukwepa mkono wa sheria.
Rwanda imepiga hatua
Pamoja na hayo, jaji huyo wa zamani amekosoa pia namna ambavyo jumuiya ya kimataifa ilichelewa kuingila kati mgogoro wa Rwanda hadi pale ambapo mamia kwa maelfu ya raia, wengi wao Watutsi, walipokuwa tayari wameuliwa. "Hata mahakama ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia mauaji ya kimbari ya Rwanda ilianzishwa kwa kuchelewa," anakosoa Schomburg. "Mahakama hiyo ilipaswa iundwe mwishoni mwa mwaka 1993 au mwanzoni mwa 1994."
Lakini jaji huyo, ambaye alifanya kazi kwenye mahakama hiyo kuanzia mwaka 2001 hadi 2008, hakuishia hapo. Ameelezea kushangazwa kwake na ukweli kwamba hakuna Mfaransa hata mmoja aliyefunguliwa mashtaka, licha ya kwamba baadhi ya Wafaransa walituhumiwa kuuza silaha nchini Rwanda katika miaka ya 1990 na kwamba wakati mwingine hata walizigawa silaha hizo kwa Wahutu. Wakati fulani serikali ya Rwanda ilijaribu kuwafungulia mashtaka wahusika, lakini bila mafanikio. Schomburg anasema Ufaransa haina nia ya kweli kufanya uchunguzi wa kipindi hicho kilichogubikwa na giza.
Lakini Schomburg ameisifu mahakama ya Umoja wa Mataifa ya kushughulikia mauaji ya kimbari ya Rwanda kwa kupiga hatua za haraka kuwawajibisha wahusika na kuwapatia haki wale walioonewa na hii imekwenda haraka hata kuliko vile ambavyo Ujerumani ilivyoendesha kesi za waliohusika katika mauaji ya Wayahudi chini ya utawala wa Wanazi.
Chanzo: Dw.de
No comments:
Post a Comment