Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema hana uhakika iwapo juhudi mpya anazofanya kwa kushirikiana na Rais Francois Hollande wa Ufaransa kuutatuwa mzozo wa Ukraine zitafanikiwa.
Akizungumza katika Mkutano wa Usalama wa Munich Jumamosi (07.02.2015) uliohudhuriwa na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Marekani,Ulaya,Ukraine na Urusi ,Merkel amesema mpango huo wa amani wa Ujerumani na Ufaransa uliowasilishwa kwa serikali ya Ukraine na Urusi wiki hii unastahili kujaribiwa lakini "hakuna uhakika iwapo utafaulu."
Kiongozi huyo wa Ujerumani amesisitiza shutuma zake kwamba Urusi imevunja sheria ya kimataifa kwa hatua inazochukuwa huko Ukraine lakini hata hivyo amefuta uwezekano wa kutumiwa silaha kwa serikali ya Ukaraine kupambana na waasi wanaoegemea upande wa Urusi mashariki mwa Ukraine.
Merkel baadae alikutana na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Lavrov,Rais Poroshenko wa Ukraine na Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden.
Ni fursa ya mwisho
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani (kushoto)Rais Vladimir Putin wa Urusi (katikati) na Rais Francois Hollande wa Ufaransa.(kulia) mjini Moscow.(07.02.2015),
Rais Hollande wa Ufaransa amesema hiyo ni mojawapo ya fursa za mwisho kuepusha vita nchini Ukraine.Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba iwapo watashindwa kupata makubaliano ya mwisho ya amani na sio tu muafaka wanajuwa fika hali itakavyokuwa ambayo ina jina moja na jina hilo ni vita.
Merkel na Hollande walikuwa wakizungumza masaa machache baada ya kurudi kutoka Moscow ambapo wameweza kuafikiana na Rais Vladimir wa Putin baada ya mazungumzo yao ya masaa matano juu ya namna ya kutekeleza usitishaji wa mapipano mashariki mwa Ukraine.
Hakuna ufafanuzi wa kina uliotolewa juu ya mazungumzo yao hayo lakini viongozi hao wamekubali kuandaa mpango mpya wa utekelezaji wa suluhu kati ya vikosi vya serikali na waasi wanaoungwa mkono na Urusi walioko mashariki mwa Ukraine.
Mpango huo unabidi ukubaliwe na Rais Petro Poroshenko wa Ukraine wakati wa mkutano kwa njia simu hapo Jumapili.
Urusi yashutumu mataifa ya magharibi
Akizungumza baada ya hotuba ya Merkel,waziri wa mambo ya nje wa Urusi Segei Lavrov amesema anaamini kwamba kuna fursa zote za kufikiwa kwa makubaliano kuhusiana na mapendekezo yaliyotolewa.
Amesema mzozo huo hauwezi kutatuliwa katika medani ya vita na kuongeza kusema kwamba Urusi iko tayari kuyadhamini makubaliano hayo mara tu yatakapokuwa yamesainiwa na waasi mashariki ya Ukraine.
Lavrov amerudia shutuma zake kwa mataifa ya magharibi kwa kuikosowa Marekani na washirika wake kwa kuukongowa mpango wa usalama wa Ulaya kutokana na kutanuka kwa Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuelekea nchi za mashariki mwa Ulaya na kuweka mipaka mipya.
Pia ameishutumu Marekani na Umoja wa Ulaya kwa kuiyumbisha Ukraine katika kila hatua ya mzozo huo.
Amesema zimeunga mkono kupinduliwa kwa serikali nchini Ukraine kwa kuunga mkono maandamano dhidi ya serikali.
Waziri huyo wa Urusi pia alisababsiha washiriki wa mkutano huo wa Munich waanguwe kicheko wakati alipodai kwamba Crimea ilijiunga kwa hiari na Urusi kwa kuzingatia Katiba ya Umoja wa Mataifa.
Mjadala waiibua tafauti
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden (kulia) na Rais Petro Poroshenko wa Ukraine katika picha ya pampja kwenye Mkutano wa Usalama wa Munich.
Mataifa ya magharibi yanaishutumu Urusi kwa kuinyakuwa rasi hiyo ilioko Bahari ya Nyeusi baada ya kutuma vikosi vyake na kuandaa uchaguzi wa hadaa.
Mjadala katika mkutano huo mashuhuri wa usalama mjini Munich umeibuwa tofauti kati ya Marekani na Ulaya juu ya namna ya kumkabili Putin wakati waasi waoegemea upande wa Urusi wakizidi kujinyakulia maeneo nchini Ukraine.Rais Barack Obama yuko kwenye shinikizo kutoka kwa baadhi ya wabunge la Marekani kuipatia silaha serikali ya Ukraine.
Mzozo huo wa Ukraine umeuwa zaidi ya watu 5,000 na kuja kudhoofisha sana uhusiano kati ya Urusi na mataifa ya magharibi katika kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa kabla.
Chanzo: Dw.de
No comments:
Post a Comment