Social Icons

Friday, 20 February 2015

Marekani inavyochochea vita Ukraine


Mapigano nchini Ukraine yanaelekea kusitishwa baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya amani yaliyokuwa yakifanyika nchini Belarus na makubaliano kutiwa saini Februari 12, 2015 na wakuu wa Urusi, Ukraine, Ufaransa na Ujerumani. Wakuu hao walikaa katika kikao kilichochukua saa 17 

Wapiganaji wa Ukraine mashariki nao waliwakilishwa. Mwishowe wakakubaliana kuwa mapigano yasitishwe ifikapo saa sita usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili. Walikubaliana pia kuwa silaha nzito zirudi nyuma ili kuachia ukanda wa amani wa kilomita takriban 75.

Kwa sasa inaonekana makubaliano yanaheshimiwa, ingawa hakuna aliye na hakika. Mwaka jana Septemba makubaliano kama haya yalifikiwa lakini baada ya muda vita ikaanza tena.

Safari hii wakati jitihada za amani zilikuwa zinaendelea pande zote mbili ziliendelea kujiimarisha. Wapiganaji wa mashariki wanaojiita jamhuri ya Donetsk (People’s Republic of Donetsk) walitangaza kuwa wanakusudia kuwaandikisha wapiganaji wapya 100,000. Rais Poroshenko wa Ukraine naye alitangaza kuwaajiri askari wapya 75,000. Hali hii inaashiria kutoaminiana licha ya mazungumzo ya amani.

Hali ya Ukraine iliharibika kuanzia Februari 2014 wakati nchi za Magharibi zilipochochea kuangushwa kwa Rais Viktor Yanukovych wa Ukraine ambaye alikataa kufungamana na upande wowote, kati ya Marekani na Urusi. Ndipo zikafanywa mbinu za kuchochea maandamano na machafuko mpaka Yanukovych akalazimika kuacha madaraka na serikali mpya ikapachikwa. Marekani ilitumia dola bilioni tano kuchochea machafuko haya.

Ni vizuri tukaelewa jinsi serikali ya vibaraka ilivyopachikwa. Ilichofanya Marekani ni kuwajaza vibaraka wake katika serikali mpya ya Ukraine baada ya kuipindua serikali iliyochaguliwa. Haya yalibainika katika mazungumzo ya simu baina ya naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Bi Victoria Nuland na balozi wa Marekani huko Ukraine, Geoffrey Pyatt.

Hii ni simu ya siri iliyovujishwa. Numan alimwambia Pyatt afanye mipango ya kuwaingiza ‘marafiki zetu’ katika serikali mpya. Pyatt akasema ni vizuri kwanza kuwashauri ‘wenzetu’ katika Umoja wa Ulaya (EU) kabla ya kuwateuwa watu hao. Numan akajibu kwa jeuri, akisema “Fuck the EU” yaani kwa tafsiri nyepesi “potelea mbali EU”.

Baada ya hapo Numan akasema waziri mkuu mpya wa Ukraine anapaswa kuwa Arseniy Yatseniuk aliyekuwa akifanya kazi katika benki. Na cheo cha urais akapewa Petro Poroshenko ambaye amekuwa jasusi wa Marekani tangu 2006. Kwa mujibu wa ripoti zake za siri kutoka Marekani huyu alikuwa ameandamwa na kashfa za rushwa, lakini ripoti inasema yeye ni “mtu wetu wa ndani”.

Kisha wakamteua Natalia A. Jaresko kuwa waziri wa fedha. Huyu alifanya kazi wizara ya mambo ya nje ya Marekani. Akapelekwa Ukraine baada ya mapinduzi, na siku hiyo hiyo akapewa uraia feki wa Ukraine na akafanywa waziri. Huko Marekani kazi yake ilikuwa ni kusimamia hizo dola bilioni 5 zilizokuwa zikitumwa na CIA kwenda kuchochea upinzani na machafuko nchini Ukraine na kutengeneza “mapinduzi” ya Februari 2014.

Mtoto wa makamo rais wa Marekani, Hunter Biden na rafiki wa waziri wa mambo ya nje Kerry, Devon Archer wakateuliwa kujiunga na bodi ya kampuni kubwa ya gesi nchini Ukraine (Busima Holding). Archer ndiye aliyekuwa mpambe wa Kerry alipokuwa akigombea urais mwaka 2004.

Hali hii haikukubaliwa na wananchi wa Ukraine, hasa katika maeneo ya mashariki ambako kuna majimbo mawili ya Donetsk and Lugansk. Wananchi wake wana asili ya Kirusi. Hawa walikataa kuitambua serikali mpya iliyoongozwa na makundi ya kifashisti yaliyosaidiwa na nchi za NATO. Wakafanya maandamano wakidai kujitoa kutoka Ukraine na kujiunga na Urusi. Majeshi ya Ukraine yakapelekwa Donesk na Lugansk ambako yaliwashambulia wananchi kwa makombora.

Kuanzia Aprili 2014 majimbo hayo yamekuwa yakishambuliwa kwa mizinga na majeshi ya Ukraine ili kukandamiza upinzani. Mnamo Mei 2014 wakaendesha kura maoni na takriban wananchi wote wakachagua kujiunga na Shirikisho la Urusi. Makombora ya Ukraine yakaendelea kuporomoshwa. Wapiganaji wa mashariki nao wakaunda jeshi lao na kujibu mapigo.

Tangu wakati huo zaidi ya watu 5,500 wamekufa na 12,200 wamejeruhiwa. Raia milioni 1.5 wamekuwa wakimbizi.
Wakati jitihada za kuleta amani zilikuwa zinaendelea, Marekani ilitangaza kuwa itapeleka majeshi ya ziada huko Ulaya ya mashariki karibu na mipaka ya Urusi. Kamanda wa majeshi ya Marekani huko Ulaya, Luteni Jenerali Ben Hodges alitangaza kuwa askari wa miavuli 600 watahamishwa kutoka Italy kwenda Ukraine ili kuyafunza majeshi ya huko.

Na kikosi cha anga cha Marekani kimetangaza kuwa kitatuma ndege za kivita 12 aina ya A-10 pamoja na wanaanga 300 kwenda Ujerumani, tayari kutumika mpakani. Rais Obama ametangaza kuwa yuko tayari kutoa misaada ya kijeshi kwa utawla wa Ukraine.

Na bunge la Marekani kwa pamoja limejitayarisha kupitisha bajeti ya dola bilioni moja kwa kazi hii. Obama alipowasilisha bajeti ya bima ya matibabu kwa raia wote bunge lilimpinga. Alipotaka kuwatoza kodi matajiri bunge lilimpinga. Lakini akitaka fedha za silaha kwa ajili ya Ukraine wabunge wanaitika “Ndiooo” bila kujali vyama vyao.

Baadhi ya maofisa wa NATO wamedokeza kuwa vitendo hivi vya Marekani vinatishia vita baina ya Urusi na nchi za NATO.

Maofisa hao wa NATO wameona kuwa wakati mazungumzo ya amani yanaendelea mjini Minsk, Marekani ina uchu wa kuongeza silaha na majeshi huko Ukraine. Hii inahatarisha makubaliano yaliyofikiwa. Ni sawa na makubaliano yaliyofikiwa Septemba mwaka jana ambayo yalihujumiwa na kuvunjika wiki chache baada ya kusainiwa. Kuna wasiwasi kuwa na mara hii huenda makubaliano ya kusitisha mapigano yakahujumiwa tena.

Msomi na mwandishi mashuhuri nchini Marekani, Profesa Noam Chomsky amesema kinachofanyika Ukraine ni tishio kwa amani ya dunia. Alipoulizwa vipi Urusi imeikalia Crimea, Chomsky alisema ni lazima ikumbukwe kuwa kihistoria Crimea daima ilikuwa sehemu ya Urusi, ni sehemu muhimu kimkakati. Akaongeza:

“Marekani imesaliti makubaliano yake na aliyekuwa rais wa USSR, Gorbachev kuwa NATO haitapanua majeshi yake jirani na Urusi. Tukaweka majeshi na silaha zetu kwenye mipaka ya Urusi. Halafu tukataka kuingia Ukraine ambayo siku zote imekuwa na uhusiano wa karibu na Urusi”.

Alipoulizwa iwapo hali ya usalama katika maeneo hayo ni tete, alijibu kuwa si tete tu bali ni hatari, kwani kuna “uwezekano wa kuzuka kwa vita kuu ya tatu, na hata utumiaji wa silaha za nyuklia”.
Haya pia yamesemwa na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani tangu enzi za Rais Nixon, Henry Kissinger, ambaye alisema kwa Urusi jimbo la Crimea limekuwa na umuhimu maalum. Akaongeza:

“Ingawa hatuwezi kuunga mkono uvamizi wa nchi yoyote, lakini ni kosa kumfananisha Putin na Hitler aliyevamia Czechoslovakia. Putin hakuwa anapanua himaya yake kwa kuvamia nchi za jirani. Hali ya Ukraine ni ya hatari mno, kwa vile Vita Baridi imeibuka tena kama ilivyokuwa zamani. Si vizuri kudharau hali hii”.

Akaongeza: “Kama tunataka Ukraine iwe na demokrasia endelevu ni vizuri isifungamane na upande wowote, isiwe koloni letu. Badala yake ni vizuri iwe daraja inayounganisha Mashariki na Magharibi”.
Mkutano wa baraza la NATO ulihudhuriwa na mawaziri 28 wa mambo ya nje. Wakaamua kuimarisha majeshi yake Ulaya Mashariki pamoja na nchi za Kiarabu na Afrika Kaskazini. Wakaamua kupanua kikosi cha dharura (NATO Response Force) kutoka wanajeshi 13,000 hadi 30,000, hasa katika nchi za Ulaya Mashariki.

Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg alisema huu ni mpango mkubwa wa kujiimarisha kijeshi tangu kumalizika kwa Vita Baridi. Alisema:

“Tumeamua kuanzisha kikosi kikubwa katika Ulaya mashariki, kikiwa na vituo sita katika Bulgaria, Estonia, Latvia, Lithuania, Poland na Romania.”

Marekani inatumia mkakati ambao ulibuniwa zamani na Zbigniew Brzezinski, aliyekuwa mshauri wa mambo ya usalama tangu wakati wa Rais Jimmy Carter. Ni yeye aliyeshauri kuwa Marekani iwasaidie kwa hali na mali wapiganaji wa Taliban huko Afghanistan ili kupigana na Umoja wa Kisovieti (USSR). Sasa anashauri kuwa Ukraine ipewe silaha ili kupigana na Urusi.

Mkakati huu wa Brzezinski unatumiwa na Marekani katika Bara la Asia, Amerika Kusini, Uarabuni, Afrika na Ulaya Mashariki. Waliutumia mnamo Septemba 2013 wakati walipotaka kuivamia Syria baada ya kubuni uwongo kuwa Rais Assad anatumia silaha za kemikali. Na mwaka jana wakabuni uwongo kuwa Urusi ilihusika na kuanguka kwa ndege ya Malaysia (MH 17) nchini Ukraine
Magharibi huwa inaishutumu Urusi kuwa imeivamia Crimea. Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy alisema hatuwezi kuwalaumu wananchi wa Crimea kwa kuamua kujitoa kutoka Ukraine na kujiunga na Urusi.

Mnamo Machi 2014 kura ya maoni iliendeshwa katika jimbo la Crimea na zaidi ya asilimia 96 walichagua kujiunga na Urusi. Hii ni baada ya serikali halali ya Ukraine kuangushwa kijeshi. Hatua ya kwanza iliyochukua serikali iliyopachikwa na Marekani ni kuwapokonya haki za kimsingi raia wa Ukraine wenye asili ya Kirusi.

Raia wa Crimea walikuwa na haki ya kujiamulia kwa kupiga kura ya maoni. Ni tofauti na Kosovo ambako NATO iliwashawishi wajitoe kutoka Serbia na kuunda taifa lao, bila ya kura ya maoni.
Ndiyo maana alipotembelea Misri hivi karibuni, Rais Putin alisema anakanusha lawama anazotupiwa na nchi za Magharibi. Alisema:

“Mgogoro wa Ukraine haukuanzishwa na Urusi. Umetokana na msimamo wa Marekani na wenzake wa NATO kujiona kuwa wao ni washindi wa Vita Baridi na kwa hivyo watafanya watakalo duniani”.
Huko Misri Rais Putin alisaini mkataba wa biashara na Rais Sisi. Chini ya mkataba huu nchi zao zitapanua biashara kati yao bila ya kutumia dola ya Marekani. Badala yake watatumia sarafu zao. Putin amesaini pia mkataba kama huu na China. Akiwa Misri, Putin alimzawadia Rais Sisi bunduki ya Kirusi aina ya Kalashnikov.

Hivyo ndivyo Putin anavyokabiliana na vikwazo alivyowekewa na nchi za NATO.

Chanzo: Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates