Social Icons

Friday, 20 February 2015

Mazito yafichuka ugaidi Tanga


MAGAIDI walioua askari kwenye mapango ya Amboni huko Tanga mwishoni mwa wiki iliyopita, yalikuwa na mawasiliano na wenzao kutoka nchi jirani ya Kenya na vikosi vya Tanzania vimenasa mawasiliano hayo, Raia Mwema limeambiwa.


Mawasiliano hayo yamevifanya vikosi vya Tanzania kuimarisha ulinzi katika mpaka wa Tanzania na Kenya unaotumia barabara ya Horohoro, kwa vile mojawapo ya meseji hizo ilieleza bayana kwamba kuna uwezekano wa wale walio nchini kuongezewa nguvu na wenzao.


Taarifa kutoka kwa askari walioshiriki katika operesheni maalumu ya kupambana na magaidi hao zimedai kwamba mojawapo ya vitu vilivyokamatwa ni simu ya mkononi ambayo ilionyesha namba zilizopigwa na zilizotumiwa meseji.


“Kuna meseji moja iliyokuwa na namba iliyoanzia na + 254 (nambari ya Kenya) ambayo ilikuwa inauliza kama wale magaidi waliokuwa mapangoni wanahitaji msaada ili wasaidiwe.


“Ile ilitupa taarifa kuwa kuna uwezekano kwamba kuna wengine wanaweza kuja. Ndiyo maana sasa utaona ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo ya mipakani haswahaswa ile njia ya kutoka Kenya,” kilisema chanzo cha habari cha gazeti hili kilichozungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kwa vile si msemaji wa Polisi wala Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).


Zaidi ya simu hiyo, gazeti hili limeelezwa kwamba askari pia walifanikiwa kukuta pikipiki, baiskeli na silaha ndogondogo za jadi kama visu na mapanga, ingawa katika mashambulizi baina yao na askari wa Tanzania, magaidi hao wanadaiwa kutumia silaha za moto.


Hadi wakati gazeti hili linakwenda mitamboni juzi usiku, kulikuwa hakuna taarifa yoyote ya kukamatwa kwa magaidi hao ambao walimuua mwanajeshi mmoja wa JWTZ aliyezikwa juzi kwenye kijiji cha Kwashemshi, Korogwe Tanga na kujeruhi askari wengine wanne.


Tukio lilivyokuwa
Kwa vile JWTZ na Polisi walikuwa hawajatoa taarifa rasmi kuhusu tukio la Amboni hadi wakati tunakwenda mitamboni, Raia Mwema limetumia vyanzo vyake ndani ya vyombo hivyo vya dola kupata taarifa hizi.


Mojawapo ya vyanzo hivyo, vimeeleza kwamba mmoja wa magaidi hao alitambuliwa na kukamatwa na Polisi ambao hatimaye walimtaka awapeleke mahali ambapo zilifichwa silaha zilizotekwa katika tukio la Januari 27 mjini humo ambapo bunduki aina ya SMG ilitekwa.


Gazeti hili limeambiwa kwamba gaidi huyo alisindikizwa na askari wanne, wa kiume watatu na mwanamke mmoja, hadi katika eneo ambalo aliwambia wenzake wamejificha pamoja na silaha zilizoibwa.


“Alipofika kwenye eneo la tukio, ghafla akaanguka na kujifanya amezimia. Sasa ikabidi wale askari waingie wenyewe ndani kwenye mapango. Walipoonekana ndipo wale magaidi wakaanza kuwarushia risasi na mabomu.


“Kosa la kwanza la Polisi lilianzia hapo. Nafikiri kiongozi wa wale askari alitaka sifa kwamba yeye ndiye kafanikisha upatikanaji wa silaha zile na kukamatwa kwa magaidi. Hakufikiri kwamba kutakuwa na upinzani mkali. Nimeambiwa pia walikwenda na bunduki moja tu”, kilisema chanzo cha Raia Mwema kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani.


Taarifa hizo zilieleza kwamba mara baada ya mapambano kokolea, gaidi yule aliyejifany kuzimia aliinuka na kukimbia na hivyo kufanikiwa kutoroka kutoka kwenye eneo la tukio.


“Baada ya kuona mashambulizi ni makali na silaha ni nzito, askari wale walikimbia umbali wa kama mita 300 hivi kutoka katika eneo la tukio na ndipo wakaamua kuomba msaada kutoka kwa JWTZ ambao angalau walipofika ndiyo wakaweza kupambana hadi magaidi wale walipotoroka,” kilisema chanzo hicho.


Kuna dhana mbili kuhusu wapi walikokimbilia magaidi hao. Kuna wanaoamini kuwa wametumia njia za ndani kwa ndani kwenye mapango hayo na kutorokea katika nchi jirani, ingawa wengine wanadai kwamba bado wamejificha ndani.


Mmoja wa vijana ambao hufanya kazi ya kuchimba mawe katika eneo jirani na mapango hayo, alisema eneo hilo lina mapango zaidi ya 13 ndani kwa ndani na hivyo mtu anaweza kujificha humohumo na asionekane na pia kuna giza.


Vita ya Mapangoni
Wakati Polisi na JWTZ sasa wakiwa wanapambana kwa pamoja kumaliza ugaidi huo, Raia Mwema limeelezwa kuhusu tofauti za kimtazamo zilizopo kuhusu namna gani ya kuendesha operesheni hiyo kwenye mapango.


Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam juzi, mmoja wa majenerali wastaafu wa JWTZ aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema njia rahisi kuliko zote ya kupambana na magaidi hao wa mapangoni ni kuziba njia zote za kutoka.


“Sina hakika sana lakini nimesikia kuwa magaidi hao walikuwa wakitoka kwenda kula nje ya hayo mapango. Hii maana yake ni kuwa hawana akiba ya chakula kule ndani. Ningekuwa naongoza operesheni ningefanya kitu kwa lugha ya kitaalamu kinaitwa containment.


“Yaani ningelizunguka tu lile eneo na kuhakikisha njia zote za kutoka zinalindwa. Nisingewafuata ndani. Kwa sababu wana shida ya chakula, watatoka tu au wataamua kufia ndani. Wakitoka watakamatwa na wakifia ndani itakuwa faida pia. Nadhani hiyo ndiyo njia bora,” alisema mstaafu huyo.


Jumatatu, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Said Mgalula na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo pamoja na viongozi wa operesheni hiyo walikutana ofisini kwa mkuu huyo kwa ajili ya kupanga mikakati ya kushughulika na tukio hilo ambalo limetikisa Taifa.


Gazeti hili limearifiwa kwamba vikosi vya JWTZ na Polisi vimewekwa katika hali ya tahadhari na vinaweza ‘kuingia kazini’ wakati wowote kama kutatokea maelekezo kutoka ngazi za juu.


“Sisi bwana tuko standby. Tangu Jumapili hatujatoka makambini. Unajua hakuna gaidi aliyekamatwa na maana yake ni kwamba mapambano haya hayajaisha. Tukiambiwa tu nendeni, tunaondoka muda huo,” alisema askari huyo aliyesema kwamba ingawa aliyeuawa ni mwanajeshi, wote wanataka kulipa kisasi kwa ajili ya mwenzao huyo.


Kikwete afanye uteuzi haraka
Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete ametakiwa kufanya haraka uteuzi wa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) na ule wa Mkurugenzi wa Intelijensia ya Jinai; nafasi ambazo ziko wazi hivi sasa.
Aliyekuwa DCI, Isaya Mngulu alistaafu mwishoni mwa mwaka jana baada ya kufikisha umri wa lazima wa kustaafu wa miaka 60 na nafasi yake imekuwa ikikaimiwa na Diwani Athumani.


Nafasi ya Mkurugenzi wa Intelijensia ilikuwa ikishikiliwa na Ernest Mangu kabla hajapandishwa cheo na kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) mwaka 2013. Tangu kuondoka kwa Mangu, nafasi hiyo haijajazwa.
“Sasa hizi ni nafasi muhimu sana ndani ya Jeshi lolote. Ukiangalia tukio la Tanga na mengine katika maeneo mbalimbali hapa nchini, utaona kuna upungufu kwenye intelijensia. Bila kuwa na mtu wa uchunguzi mtafanyaje kazi zenu?


“Tungependa kumuomba sana Amiri Jeshi Mkuu Kikwete kufanya uteuzi huu haraka. Na uteuzi wenyewe usiwe wa kujaza nafasi lakini watafutwe watu wenye uwezo na wanaoweza kukabili changamoto hizi zilizojitokeza,”kilisema chanzo hicho kutoka Mambo ya Ndani.


Ingawa hadi sasa hakuna ushahidi wa waziwazi wa kuhusisha tukio hilo na makundi ya ugaidi kama Al Shabaab la Somalia, baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa vimelihusisha na makundi hayo.


Chanzo: Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates