Social Icons

Saturday, 21 March 2015

Hadithi: Familia Tata - 38

Beka akakohoa, kuonyesha kujiandaa kwa ajili ya kutoa maelezo. Yule mzee alimpa kitu kama simu, akimwambia wakati anazungumza akiweke mdomoni mwake, ambacho dhahiri kilikuwa ni kipaza sauti. Macho ya vijana wote wawili yalionyesha woga, kitu kilichowapa nguvu wale watu waliowazunguka…
Sasa endelea...

Mzee Komba na mkewe walikuwa wamekaa sebuleni kwao, wakijadiliana hili na lile kuhusu maisha yao baada ya matukio yale ya kushangaza. Jirani na rafiki yao wa muda mrefu aligeuka adui mkubwa na wakati wowote maafa zaidi yangeweza kutokea.

Waliwaita watoto wao na kuwaeleza jinsi ambavyo familia yao ilivyokuwa vitani na majirani, na kuwataka kuwa makini kwani lolote baya linaweza kuwatokea endapo hawatakuwa waangalifu.

***
Dayani alikuwa amekaa katika moja ya vibanda vilivyomo ndani ya baa yake ya Zanzi wakati simu yake ya mkononi ilipoita na mara moja mapigo ya moyo wake yakapiga. Akaipokea kwa hamasa na baada ya sekunde chache za kusikiliza, akaiondoa sikioni na kuikata.

Baada ya sekunde chache, naye akaichukua tena simu yake na kubonyeza namba kadhaa, kisha akaipeleka sikioni kwake. Ikaita kwa muda mrefu bila kupokelewa. Akakata na kusubiri, baada ya dakika mbili akaichukua na kuirudia tena ile namba ambayo sasa ilipokelewa.
“Chuga” upande wa pili wa simu uliita.
“Uko wapi?” 
“Hotelini”

“Nakuja”
Dayani aliliendea gari lake, akaingia na kuwasha, kisha akaelekea kwanza nyumbani kwake, akakaa muda wa dakika kama ishirini akizungumza na mkewe, kisha akatoka akiwa na begi dogo mkononi mwake.
Akaingia tena kwenye gari lake na kuliwasha. Dakika ishirini baadaye alikuwa nje ya hoteli aliyofikia rafiki yake mzee Linus. Akaegesha na kuingia ndani moja kwa moja hadi chumbani kwake.

“Chuga..nina wasiwasi mambo yameharibika, nimeongea na Beka kwa simu, ananiambia niende sehemu akanipe mzigo, sauti yake haikuwa huru, ninamjua yule dogo, kwa uzoefu wangu, wamekamatwa,” Dayani alisema huku akionyesha sura ya mashaka, maneno yaliyomshtua sana Linus na mkewe.
“Dah, kwani walikuwa wameenda wapi,” aliuliza.

“Hakuna muda wa maswali, wale watakuwa wamebanwa na wamesema kila kitu, wameniita ili wakanikamate, cha kufanya hapa ni mimi na wewe kutoweka haraka sana kabla hatujakamatwa,” alisema huku akisimama, ishara kwamba waondoke.

“Mke wangu naye tunaenda naye?” aliuliza huku akijifuta jasho.
“Hapana, yeye anaweza kwenda kukaa sehemu yoyote, hata akikamatwa ni rahisi kwake kukataa kuwa hajui lolote,” akatoka nje akiwaacha ndani mzee Linus akijadiliana na mke wake.
“Sasa mume wangu itakuwaje, maana naona hasara juu ya hasara,” alisema mama Tony.
“Hata sielewi, nimechanganyikiwa kabisa, hebu ngoja kwanza nitoke eneo hili nisikilizie. Halafu mimi sitaki wewe uondoke, kaa hapahapa, ili ujue kinachoendelea upate kunifahamisha,”

“Kwani nyie mnaenda wapi?” aliuliza mkewe
“Sijui, nitakufahamisha,” alisema huku naye akitoka, baada ya kuwa amempa fedha kidogo. Benki walikuwa na akiba ya kutosha ambayo angeweza kuitumia wakati huu wa matatizo.
Akatoka nje akiwa hana hata mfuko wa Rambo, kwa sababu nguo zake zote ziliteketea na hakuwa amenunua tena. Akaungana na Dayani garini, likawashwa na likaelekezwa njia ya Bagamoyo.

***
Beka na Shosi walikuwa ndani ya gari jeusi lililochokachoka kidogo, nje ya baa ya Jilipue, mitaa ya ndanindani Mwananyamala jijini Dar es Salaam. Wakati wanazungumza na Dayani, askari mmoja alikuwa pembeni yao akiwasikiliza. Walipomaliza wakanyang’anywa simu na kuelekezwa kutulia ndani ya gari.
Zaidi ya askari kanzu kumi walikuwa wamezunguka eneo hilo wakimsubiri Dayani.

Kwa jinsi walivyokuwa wamejipanga, walikuwa na uhakika hataweza kuponyoka hata akiwa mahiri vipi. Baadhi yao walikuwa kaunta, wengine kazi yao ilikuwa ni kuangalia nyendo za wale vijana garini.
Saa moja ilipita bila Dayani kutokea, askari mmoja akawaendea mle garini na kuwauliza mbona bosi wao hajatokea hadi muda ule, nao wakamwambia hawaelewi. Yule askari akawapa ishara wenzake na watatu kati yao wakalisogelea lile gari.

“Jamaa hajatokea, tufanyaje?” aliwauliza wenzake.
“Hebu wamcheki tena kumuuliza amefika wapi,” mwingine alishauri. Wakakubaliana, wakatoa simu ya Beka na kumpa ili apige tena simu kwa Dayani.

Chanzo: globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates