Social Icons

Saturday, 28 March 2015

Hadithi: Familia tata - 44

Maria akatoka, akaangaza macho huku na kule, Stone akajificha kwenye mojawapo ya nguo zilizokuwa zimetundikwa nje ya duka moja la nguo. Kisha msichana huyo akaanza kuondoka taratibu akiufuata mtaa wa Msimbazi.
Sasa endelea...

STONE alitoka na kuanza kumfuatilia taratibu kwa nyuma. Maria, akiwa hana hili wala lile, alitoa simu yake ya mkononi kutoka katika mkoba aliokuwa ameubeba, akabonyeza namba kadhaa na kuanza kuzungumza na shoga yake.

Akaendelea kupiga stori huku akisonga mbele, akaufikia mtaa wa Msimbazi, akaelekea kushoto, akaenda huku akisimama mara kwa mara kuangalia vitu vilivyokuwa vikiuzwa na wamachinga waliokuwa wamevipanga kando ya barabara.

Akaupita mzunguko na kwenda mbele ambako aliingia katika moja kati ya Bajaj zilizokuwa zimesimama sehemu moja hivi. Baada ya sekunde chache za kuzungumza na dereva, ikaondoka sehemu hiyo huku Stone akiharakisha mwendo naye akisogelea kituo kile.

Akiwa anaifuata Bajaj, nyingine ikawa inapita, akaisimamisha na kumuuliza dereva.
“Una mafuta ya kutosha?”
“Full tank kaka, hata Mwanza tunafika non stop,” alijibiwa na kijana aliyekuwa anaendesha. Akaingia na kumwambia;

“Unaiona ile Bajaj?” alimuonyesha Bajaj aliyokuwa amepanda Maria na kumweleza kuwa alitaka aifuate kwa nyuma hadi atakaposhuka abiria aliyepanda. “Vipi, kuna tatizo lolote kaka,” kijana huyo aliuliza huku akiongeza mafuta kuiondoa Bajaj hiyo. Stone akamwambia kuwa msichana aliyepanda ni mpenzi wake na anahisi ana mchepuko kwa hiyo anataka kumfumania. Kijana akacheka na kuendelea na hamsini zake.

Kijana aliyempakia Stone akajikuta akimtilia mashaka, hata hivyo hakumuonyesha. Bajaj aliyokuwa anaifuatilia ilikuwa inaendeshwa na rafiki yake, hivyo wakiwa wamesimama kwenye foleni alimtumia ujumbe mfupi kwenye simu yake ya mkononi.

“Oyaa, kuna jamaa nimempakia anaifuatilia Bajaj yako, una abiria gani humo?”
“Kuna demu mmoja mkali kweli mwanangu, huyo jamaa anamfuatilia huyu au mimi,” mtu wa upande wa pili naye alijibu baada ya muda mfupi. Waliendelea kuwasiliana na kila mmoja alionyesha mashaka yake.

“Hebu mpige picha afu unitumie nimuone huyo jamaa,” ujumbe uliingia katika simu ya kijana aliyekuwa na Stone, ambaye akili yake yote ilikuwa katika Bajaj iliyokuwa mbele yao. Aliamini wakati huu wakiwa wanaishi mbalimbali, ulikuwa ndiyo muafaka zaidi kumaliza kazi aliyopania kuifanya.

Kumpiga picha Stone ilikuwa ni kazi ambayo asingeweza, kwanza kwa kuwa alikuwa amekaa nyuma ya Bajaj na hivyo kugeuka na kumfotoa ingekuwa ishu kubwa, lakini kikubwa zaidi ni kwamba umbo lake lilimtisha, akamtumia jamaa yake ujumbe na kumfahamisha kuhusu suala hilo.

Wakakubaliana kusubiri ili kuona kitakachoendelea. Bajaj iliyombeba Maria ilikata kona kuifuata barabara ya Nyerere, baadaye ikapinda kushoto na kuelekea Keko. Ilipofika katika maghorofa ya NHC, Bajaj hiyo ilisimama na Maria akateremka.

“Paki pembeni babu, itakuwa bei gani hadi hapa” Stone alimwambia dereva wake, ambaye aliisogeza pembeni na kusimama. Akalipa kiasi cha fedha alizotakiwa na akaanza kuondoka, kijana huyo alitumia muda huo kumpiga picha bila mwenyewe kujua.

Maria akiwa hana hili wala lile, alivuka upande wa pili wa barabara, akaingia katika uchochoro mmoja uliokuwa na watu wengi, akatokezea upande wa pili mtaani. Hakumuona Stone aliyekuwa nyuma yake, alimfuatilia hadi alipoingia katika nyumba moja nzuri.

Stone akaipita nyumba hiyo na kwenda mbele kidogo, katika duka moja, akasimama nje na kuagiza soda. Hakutaka kuamini mara moja kama hapo ndipo alikuwa anaishi. Alikaa saa nzima bila kumuona Maria wala ndugu yake yeyote akitoka wala kuingia.

**
Jumba alifika katika nyumba ya kulala wageni aliyoelekezwa na Mzee Linus, akiwa mapokezi alimkuta mhudumu ambaye alipomuuliza kuhusu mgeni wake, alimwelekeza chumba alichokuwa amefikia.
Mama yake Asfat alishangaa sana kumuona Jumba nje ya mlango baada ya kumgongea. Walisalimiana na ndipo alipomueleza chanzo cha yeye kufika pale alipokuwa. Ndipo mama huyo aliposhtuka na kubaini kwamba simu yake haikuwa hewani tokea alipoizima muda mrefu uliopita.

“Jamani pole sana, simu niliizima muda mrefu, sikutaka usumbufu, basi asante ntampigia baba nimsikie,” alisema na Jumba akatikisa kichwa huku akiondoka sehemu hiyo.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua inayoelekea ukingoni katika toleo lijalo.

Chanzo: globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates