Social Icons

Sunday, 5 April 2015

Hadithi: Familia tata - 50

Wale wa ndani wakapatwa na taharuki kubwa, lakini kwa mshangao wao, hawakuona dalili zozote kama kulikuwa na mtu. Kwa kutumia ufunguo m****** wakafungua geti, wenzao waliokuwa nje wakaingia ndani. Ua ulikuwa mkubwa, ndani kulikuwa kimya, wakakubaliana kuuvunja mlango. Wakitumia bastola isiyotoa sauti, wakapiga risasi tatu kwenye kitasa, kikaachia, mlango ukafunguka!
Sasa endelea...

Wakasubiri kwa muda wa dakika mbili, kukawa kimya. Kwa tahadhari kubwa, askari wa kwanza, bastola ameitanguliza mbele, akaingia sebuleni. Hakukuwa na mtu. Akaingia askari wa pili na wa tatu, wa nne akabakia nje.

Wakaitazama sebule, ilikuwa imepambwa vizuri, wazi kuwa kulikuwa na mtu aliyekuwa anashughulika nayo kila mara. Upande wa kila sebule, kushoto na kulia kulikuwa na milango, ya chumbani bila shaka. Wakashangaa kuona hakukuwa na mtu aliyeshituka, licha ya milio ya risasi.

Wakapeana ishara za kugonga milango. Wakachagua kuanza na wa kulia kwao, wakagonga zaidi ya mara nne, hakukuwa na jibu. Wakaugeukia wa kushoto, nao wakagonga kama vile mambo yakawa yaleyale. Wakakubaliana kutumia ufunguo malaya. Wakafungua mlango wa kwanza, ndani wakakuta kitanda kikubwa, cha ukubwa wa sita kwa sita, kimetandikwa vizuri!

Ukutani nako kulikuwa na kabati kubwa la nguo. Walipojaribu kulifungua, likakubali bila ubishi. Wakalipekua, ndani kulikuwa na nguo za aina mbalimbali, za kike, za kiume na watoto. Wakajiridhisha kuwa kuna familia inaishi ndani ya nyumba hiyo.

Wakahamia chumba cha pili, nako kama ilivyokuwa katika chumba cha kwanza, kulikuwa na kitanda kikubwa na kabati, vyote vikiwa nadhifu. Wenyewe walikwenda wapi? 
Wakakubaliana kutoka nje kwanza kwa ajili ya kubadilishana mawazo na wenzao. Wakatoka nje ya geti, wakasimama na kuwasiliana na wenzao kwa ajili ya majadiliano mafupi. Kwa muda wote tokea wanawake wale waingie, hakuna mtu aliyetoka, sasa wako wapi?

Swali lile liliwaumiza sana kichwa. Wakarejea tena ndani na kujaribu kuona kama kuna sehemu yoyote imevunjwa au dirisha limefunguliwa na kuwaruhusu kutoka, hawakuona. Wakiwa nje, eneo lote likiwa giza, wakagundua kuwa kulikuwa na nyumba mbili tu zinazowaka taa. Ile waliyokuwa wameizingira na nyingine iliyokuwa mita kadhaa mbele yao.

Wakafanya mawasiliano na watu wa Tanesco ili kujua kama umeme umekatwa kikamilifu katika nyumba zote, wakajibiwa kuwa eneo lote limezimwa na zile zinazowaka, huenda wana jenereta zao binafsi. 
Jibu hilo likawavutia, wakapeana ishara ya kuizingira nyumba ile nyingine inayowaka umeme pia. Askari wakaongezwa. Usiku ule wa saa nne, ilikuwa ni mapema mno kukamilisha operesheni yao waliyokusudia kuwakamata watu wanaohusika na mauaji. Mawasiliano ya simu kutoka simu za watuhumiwa, zilizokuwa zimetegwa, zote zilionekana kuzimwa!

***
Mlio wa risasi katika kitasa cha mlango wa ile nyumba ndogo, ulisikika kwa usahihi kabisa sebuleni kwa akina Dayani, kwani kulikuwa na spika kubwa iliyotegwa, ambayo ingeweza kuleta sauti ya kitu chochote kisicho cha kawaida ambacho kingetokea.

Na ni mlio ambao ni Dayani pekee miongoni mwa watu zaidi ya sita waliokuwepo sebuleni waliousikia na kutambua maana yake. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, hofu ikamtawala moyoni mwake. Hata hivyo, hakutaka kuionyesha.

Mzee Linus, mshirika wa zamani wa Dayani, pamoja na kuwa hakuwa naye karibu kwa miaka mingi, lakini bado hisia za kihalifu zilikuwa ndani ya damu yake, na alijua jinsi ya kuhisi hatari au hata kumtambua mtu aliye hatarini. Mabadiliko ya ghafla ya rafiki yake, yalimpa ishara mbaya.
“Chuga” Mzee Linus alimshtua Dayani kutoka katika mawazo ya kuchanganyikiwa yaliyokuwa moyoni mwake na kuitwa jna hilo, kulimkumbusha kuwa alikuwa katika mapambano.
“Noma,” alijibu kwa kifupi, kauli ambayo mzee Linus aliielewa vizuri sana.
“Sasa?” aliuliza.

“Wapo hatua chache kutoka tulipo, inabidi tuondoke haraka eneo hili,” alisema na kusimama, akaingia chumbani kwake, kwenye kiboksi kimoja kilichokuwa ukutani mwake, akabonyeza kitufe chenye rangi ya njano.

Kama ilivyokuwa katika makazi yake ya jijini Dar es Salaam, Dayani pia aliijenga nyumba hii kwa ajili ya ulinzi wake binafsi wakati wa matatizo yake ya kihalifu. Nyumba ndogo ambayo Devo na mama Asfat waliingia, ilikuwa na sehemu ya kuingilia, yenye ngazi zilizotokeza kwenye nyumba yake na ndimo walimopita. Kitufe cha njano alichokibonyeza, kiliziba njia hiyo kwa zege kubwa lilionyesha kama mwisho wa njia hiyo!

Chanzo: globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates