Social Icons

Thursday, 19 May 2016

Mmojawapo wa wasichana wa Chibok apatikana

Msichana wa kwanza kati ya wasichana 219 wa shule ya Chibok nchini Nigeria waliotekwa nyara na waasi wa Boko Haram miaka miwili iliyopita amepatikana.

Msichana huyo amepatikana jana katika msitu wa Sambisa ulioko katika jimbo la Borno na kundi la raia wanaoshika doria wakisaidiwa na wanajeshi wa Nigeria. Jeshi la Nigeria limethibitisha kupatikana kwa msichana huyo katika kijiji cha Baale karibu na mji wa Damboa kilomita chache kutoka alipotekwa nyara na wenzake.

Msemaji wa jeshi Kanali Sani Usman amesema Falmata Mbalala ni miongoni mwa watu waliowaokolewa katika operesheni iliyofanywa katika msitu wa Sambisa ambako kuna kambi za waasi wa Boko Haram.

Kuna matumaini ya kupatikana wengine

Kuna taarifa za kukinzana kuhusu jina halisi la msichana huyo. Baadhi ya vyombo vya habari vimemtambua kwa jina Amina Ali huku vingine vikisema anaitwa Falmata Mbalala. Taarifa nyingine za kuhitilafiana ni kuwa aidha amejifungua na alipatikana akiwa amebeba mtoto huku taarifa nyingine zikiarifu ni mja mzito.

Wanaharakati wa kampeini ya Bring Back our Girls wakiandamana

Wanaharakati wa kampeini ya Bring Back our Girls wakiandamana

Kiongozi mmoja wa kijiji Ayuba Alamson amesema msichana huyo alikutana na wazazi wake waliomtambua kabla ya kupelekwa katika kambi ya kijeshi iliyoko Damboa.

Yakubu Nkeki ambaye ni kiongozi wa kundi la wazazi wa wasichana hao waliotekwa nyara wa Chibok amesema jina la msichana huyo ni Amina Ali na alikuwa na umri wa miaka 17 alipotekwa nyara.

Boko Haram iliwateka nyara wasichana 276 kutoka shule ya umma ya upili ya wasichana tarehe 14 mwezi April mwaka 2014. Wasichana 57 walifanikiwa kutoroka punde tu baada ya shambulizi hilo.

Na tangu wakati huo, hatma ya wasichana 219 haikujulikana licha ya juhudi kabambe za kuwatafuta. Inaripotiwa kuwa huenda wasichana zaidi wameokolewa na jeshi baada ya operesheni ya kuwaokoa iliyofanyika jana usiku katika msitu huo wa Sambisa.

Wasichana wa Chibok walitekwa nyara 2014

Amina anaripotiwa kuwa salama ila mwenye msongo wa mawazo. Kiongozi wa kundi la Boko Haram Abubakar Shekau aliapa kuwafanya wake za wapiganaji wake na kuwauza wasichana hao katika nchi jirani kama watumwa wa ngono.

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau

Gavana wa jimbo la Borno Kashim Shettima amewaambia wanahabari kuwa msichana huyo anapelekwa katika mji mkuu wa jimbo hilo wa Maiduguri.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari alipoingia madarakani mwaka mmoja uliopita aliahidi kuwatafuta na kuwaokoa wasichana hao na kuliangamiza kundi la Boko Haram.

Kulingana na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International takriban wasichana na wavulan 2,000 wametekwa nyara na Boko Haram tangu 2014 na kutumika kama watumwa wa ngono, wapishi, wapiganaji na washambuliaji wa kujitoa muhanga.

Boko Haram imewaua takriban watu 20,000, kupelekea kiasi ya wengine milioni 2.6 kuyatoroka makaazi yao na kusababisha janga la kibinadamu kaskazini mwa Nigeria na katika nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad.

Chanzo. Dw.de


No comments:

 
 
Blogger Templates