Social Icons

Saturday, 20 August 2016

HISTORIA YA MABINGWA WA SOKA TANZANIA BARA MWAKA 1986 TUKUYU STAR YA MBEYA

Timu ya Tukuyu Star ni timu ya mpira wa miguu iliyoanzishwa mwanzoni mwa mwaka 1982 Na makao makuu yake yalikuwa katika eneo la Bagamoyo mjini Tukuyu. Timu ya Tukuyu Star mala baada ya kupanda daraja la kwanza mwaka 1985 na kushiriki ligi kuu ya Tanzania Bara mwaka 1986, mwaka huo huo 1986 iliishangaza dunia kwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.

WAZO LA KUANZISHWA TIMU.

Wazo la kuanzishwa timu ya Tukuyu Star lilitokana na Joseph Kasyupa na Abdul Lausi, Joseph Kasyupa alikuwa mwamuzi wa mpira wa miguu yaani refa na Abdul Lausi alikuwa ni katibu mkuu wa Mwenge Sports Club.
Siku hiyo walikuwa wamekaa kwenye gari la Abdul Lausi aina ya Land Rover 109 (Lunar 10), wakawa wanajiuliza kwa nini wilaya ya Rungwe hakuna maendeleo ya mpira wa miguu, tatizo waliloligundua lilikuwa pamoja na kuwa na wachezaji wenye vipaji wengi, lakini pia timu za mpira wa miguu zilikuwa nyingi sana wilayani Rungwe.

Ndipo walipopata wazo la kuziunganisha timu mbili zilizokuwa katikati ya mji wa Tukuyu, timu hizo zilikuwa Mwenge Sports Club na Jamuhuri Sports Club. Mwenge Sports Club ilikuwa ikifadhiliwa na Jeshi la Polisi Tukuyu, OCD wakati huo akiwa SP Msoffe, na timu ya Jamuhuri Sports Club ilikuwa ikifadhiliwa na wafanya biashara wa soko la Tukuyu.

Joseph Kasyupa na Abdul Lausi walikubaliana wawaone viongozi wa timu hizo mbili, na kuwauzia wazo lao la kuziunganisha timu zao na kuunda timu moja yenye nguvu na ubora. Mwenyekiti wa Mwenge alikuwa Marehemu Salumu Madodi na Katibu alikuwa Marehemu Abdul Lausi Uongozi wa Jamuhuri mwenyekiti wake alikuwa Juma Omari ( Juma wa ESSO) katibu alikuwa Marehemu Anyimike Hamuli.
           
             Marehemu Salumu Madodi

Kwanza walimfuata Mwenyekiti wa Jamuhuri Juma Omari, ambaye alikubali wazo mara moja, na baadaye walimsubili Mwenyekiti wa Mwenge Marehemu Salumu Madodi ambaye alikuwa safarini, aliporejea kutoka safari Mzee Madodi nae alikubali wazo hilo mara moja.

Walikubaliana kila kiongozi aende akawaeleze wazo hilo kwenye timu yake, baada ya muda mfupi viongozi wote wawili walirudisha majibu kuwa wanachama wao wamekubali kuziunganisha timu zao, na kuunda timu moja yenye nguvu. 

MWANZO WA TIMU MPYA

Mkutano wa kwanza wa timu hizo mbili kwa pamoja ulifanyika mwanzoni mwaka 1982, katika mkutano huo wajumbe waliamua kabla ya kuanzisha rasmi timu, kwanza waangalie watu wengine walio nje ya timu zao ambao wanaweza kuwashirikisha katika uanzishaji wa timu hiyo mpya. Ndipo wazo la kumshirikisha mfanyabiashara maarufu wa mji wa Tukuyu Ramnik Pater Kaka, lilipotolewa na kuungwa mkono.

KWA NINI KAKA ALIHUSISHWA KUANZISHA TIMU MPYA.

Ramnik Pater Kaka na Mkewe walikuwa na mazoea ya kila siku jioni kwenda kwenye uwanja wa mpira wa CCM Tukuyu kuangalia mpira, siku moja KAKA alivutiwa na uchezaji wa timu ya Utumishi iliyokuwa ikimilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, hivyo akaamua kuwazawadia Jezi na viatu vya kuchezea mpira.
        
                     Ramnik Pater Kaka

Joseph Kasyupa kwa kuwa alikuwa rafiki wa KAKA alilijua wazo lake na akaliwakilisha wazo la KAKA kutaka kutoa vifaa vya michezo kwa Utumishi kwenye mkutano huo, ndipo wajumbe walipomtaka Kasyupa amuwahi KAKA kabla hajaingia Utumishi aingie kwao ili waanzishe nae timu mpya.

Kikao kilichofuata kilipofanyika Ramnik Pater KAKA alihudhuria ndicho kilichoamua kuanzisha rasmi timu mpya, kikao hicho kilikuwa chini ya Mwenyekiti wa muda Mzee Salumu Madodi.

Baadae ulifanyika uchaguzi wa viongozi wa timu mpya, waliochaguliwa kuiongoza timu kwa kipindi cha mpito walikuwa ni.

Mwenyekiti wa timu : Hebroni Mwasambili
Katibu wa timu : Saimon Mfikwa
Mfadhiri wa timu : Ramnik Pater Kaka.

Baada ya kupata viongozi, waliamua kutafuta jina la timu katika kikao hicho wajumbe walikubaliana timu iitwe Limbe sports Club, wakiiga jina la timu maarufu nchini Malawi ya Limbe Leaf. Kikao kiliagiza itengenezwe katiba ya timu na timu kusajiliwa rasmi Baraza la Michezo la Taifa.

Jina la Limbe Sports Club lilikataliwa kusajiliwa na BMT kutokana na kuwepo timu yenye jina hilo nchini Malawi. Hivyo kutakiwa kutafuta jina jingine, kikaitishwa kikao kingine ili kutoa taarifa ya kukataliwa kwa jina la Limbe.

Baada ya majadiliano ndipo mke wa Ramnik Pater Kaka alipotoa wazo la timu kuitwa Tukuyu Star Sports Club, kwa maana ya ( Nyota ya Tukuyu) wazo lililoungwa mkono na wajumbe wote. Ndio ukawa mwanzo wa TUKUYU STAR SPOTS CLUB.
        
           Kadi ya kwanza ya Tukuyu Star

Baada ya kuanza rasmi timu ya Tukuyu Stars ilifanya uchaguzi mkuu na kupata viongozi wafuatao.

Mwenyekiti wa timu : Hebron Mwasambili
Makamu mwenyekiti : Salumu Madodi
Katibu Mkuu : Kimpokile Mwakyoma
Msaidizi : Abdul Lausi
Mtunza hazina : Mama Kaka
Msaidizi: Njovu
Mlezi wa Timu : Ramnik Pater Kaka.

Inaendelea sehemu ya 2

Mwandishi Bashiru Madodi


No comments:

 
 
Blogger Templates