Social Icons

Sunday, 21 August 2016

HISTORIA YA TUKUYU STAR YA MBEYA MABINGWA WA SOKA TANZANIA BARA MWAKA 1986. SEHEMU YA 2.

MAFANIKIO YA TIMU YA TUKUYU STAR

Mara tu baada ya kuanzishwa na kusajiliwa rasmi uongozi wa timu ya Tukuyu Star chini ya Mlezi na mfadhili mkuu wa timu Ramnik Pater Kaka, walianza jitihada za kuhakikisha timu yao inachukuwa ubingwa wa wilaya mwaka huo huo 1982.
  
                Godwin Aswile (Scania)

Jitihada ya kwanza ilikuwa ni kusajili wachezaji wazuri kutoka timu zote zilizokuwepo wilayani Rungwe, Miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa na Tukuyu Star mwaka 1982 walikuwa, Lawlance Pyukula, Mwangupi, Jeriko Lwaga, Saimon Mwasakyeni, Agostino Mumbe, John Alex na Bashiru Madodi. Kocha wa timu alikuwa John Ameni.
              Seleman Mwankenja

Mwaka huo huo 1982, mafanikio ya Tukuyu Star yalianza kujitokeza kwa timu kuchukua ubingwa wa daraja la tatu wilayani Rungwe na kuwa bingwa wa wilaya ya Rungwe. Timu ilizochuana nazo zilikuwa Kurugenzi, Tanesco, Chai, Rungwe Sekondari, na Kapologwe.
                           Abdalla Madodi

Baada ya kuchukua ubingwa wa wilaya mwaka 1982, Mwaka 1983 Tukuyu Star ilishiriki ligi daraja la pili, wakati huo ikiitwa ligi ya mkoa, na ikaweza kuchukua ubingwa wa daraja la pili na kuwa bingwa wa mkoa wa mbeya.

Mchezo unaokumbukwa na wapenzi wa mpira katika ligi ya mkoa wa Mbeya, ulikuwa ni kati ya timu mbili za Tukuyu, yaani Kurungenzi na Tukuyu Star, mchezo huo ulichezwa Chimala wilayani Mbarali. Mji wote wa Tukuyu ulihamia Chimala, magari yote ya wafanyabiashara wa Tukuyu yalibeba mashabiki wa Tukuyu Star kuwapeleka Chimala mbarali.
                       Seleman Methew

Na magari yote ya Serikali yalibeba mashabiki wa Kurugenzi, ikumbukwe kuwa timu ya Kurugenzi ilikuwa inamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, katika mchezo huo timu ya Tukuyu Star ilishinda 1-0, goli ambalo mpaka leo hakuna anaejua liliingiaje golini.

Kwani wakati mpira unaelekea golini mwa Kurugenzi Golikipa wa Kurugenzi alipandwa na siafu mwilini ambao hawakujulikana wametokea wapi, wakati anahangaika na siafu ndipo mpira ulipompita kirahisi na kuwa goli pekee katika mchezo huo. Timu nyingine zilizokuwepo kwenye ligi hiyo zilikuwa N.M.C, R.T.C. Red Angels.

Baada ya kuchukua ubingwa wa mkoa wa Mbeya Tukuyu Star ilishiriki ligi ya kanda za nyanda za juu kusini mwaka 1984 na kuongoza kundi lao na kwenda kupambana na mabingwa wa kanda zingine, ndipo mwaka 1985 Tukuyu Star ikapanda daraja la kwanza na kushiriki ligi kuu ya Tanzania bara mwaka 1986.
                           Peter Mwakibibi

Wachezaji wa timu ya Tukuyu Star walioipandisha daraja mwaka 1985 walikuwa ni hawa wafuatao, Selemani Mwankenja, Fadhiri Hembe, Taisi Mwalyoga, Daniel Chundu, Richard Lumumba, Danford Ngesi, Kervin Haule, Wilfred Sangula, Godwin Aswile, John Alex, Abdalla Shaibu, Mohamed Salehe, Ally Kimwaga, Hussein Zitto.
 
                    Hussein Zitto

Wengine, Haji Shomari, Aston Pardon, Augostino Mumbe, Abdalla Madodi, Michael Kidilu, Jastin Mtekele, Lawlance Pyukula, Asanga Aswile na Benson Kasambo. Meneja wa timu alikuwa Lucas Monyo, na kocha wa timu alikuwa Athmani Juma.

Baada ya kupanda daraja na kuwa ligi kuu Tukuyu Star iliwaacha wachezaji wafuatao ili kusajili wachezaji wenye uwezo wa kupambana na mikiki mikiki ya ligi kuu ya Tanzania Bara. Wachezaji walioachwa walikuwa, Lawlance Pyukula, Benson Kasambo, Chogo na Twaha.

Ili kuimalisha kikosi Tukuyu Star ilisajili wachezaji wafuatao, 
1: Peter Mwakibibi   Toka Kurugenzi Dodoma.
2: Mbwana Makatta toka  Waziri Mkuu Dodoma.
3: Karabi Mrisho  toka  Kurugenzi Dodoma.
4: Dickson Ntole toka Lipuli Iringa
5: Selemani Methew  toka Mwatex Mwanza
6: Yusuph Kamba  toka Bora Iringa.
                       Kalabi Mrisho

Baada ya kupanda daraja na kushiriki ligi kuu Tanzania Bara mwaka 1986, Timu ya Tukuyu Star iliishangaza dunia kwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, na kuziacha hoi timu kongwe za Simba na Yanga za Dar.

Ukiwauliza viongozi wa Tukuyu Star wa wakati ule, mchezo gani wanaukumbuka katika kumbukumbu zao, watakwambia ni mchezo kati ya Tukuyu Star na Pamba ya Mwanza uliochezwa Mbeya na Pamba kushinda goli 1-0, Pamba ikiwa na wachezaji hatari kama, Rajabu Risasi, Nteze John, George Masatu, Halfan Ngasa na John Makelele.

Makocha waliowahi kufundisha Tukuyu Star ni hawa wafuatao, John Ameni, Abdulrahaman Juma, Selemani Mbwembwe, Athmani Juma, Artha Mwambeta na Paul West Gwivaha

NAFASI YA USHIRIKINA KATIKA MCHEZO WA MPIRA WA MIGUU

Tukuyu Star kama timu nyingine zinazoshiriki ligi kuu ilikuwa na wataalamu wake, wao wakiita kamati ya ufundi watalamu wao waliwatoa Tanga, Tukio la kishirikina wanalolikumbuka viongozi wa Tukuyu Star, ni lile la kupasuka mpira wakati unaenda kuingia kwenye goli la Tukuyu Star walipokuwa wanacheza na Nyota Nyekundu ya Dar.

Inakumbukwa siku hiyo mpira ulipigwa na mshambuliaji wa Nyota Nyekundu, mpira huo ulimpita golikipa wa Tukuyu Star Mbwana Makata, wakati mpira unaelekea kuingia golini kabla haujavuka mstari ukapasuka na kubaki pale pale kwenye mstari..

Itaendelea 3

Mwandishi Bashiru Madodi



No comments:

 
 
Blogger Templates