Social Icons

Monday, 26 August 2013

MLINZI WA KAGAME AKAMATWA UGANDA

Aliyewahi kuwa mlinzi wa Rais Paul Kagame wa Rwanda, Luteni Joel Mutabazi amekamatwa na Polisi nchini Uganda akidaiwa kuingia nchini humo kinyume cha sheria.

Gazeti la Daily Monitor la Uganda lilieleza jana kwamba Luteni Mutabazi alikamatwa Jumanne wiki hii kisha kukabidhiwa kwa Idara ya Wakimbizi iliyopi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Uganda.

Luteni Mutabazi ambaye alikuwa mlinzi wa Kagame sasa anahesabiwa kuwa miongoni mwa wakimbizi wa kijeshi wa Rwanda na alihifadhiwa kwa usiku mmoja kwenye kituo cha polisi cha Jinja wakitaka arejeshwa Kigali, hatua ambayo Kamishna wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa aliipinga akisema ni ya hatari.

Waziri wa Maafa wa Uganda, Preparedness Musa Ecweru alisema jana kwamba Luteni Mutabazi yuko ‘huru na salama’ ambapo upo uwezekano wa kumtafutia nchi ya tatu kwa ajili ya kupata hifadhi kwa usalama wake.

Luteni Mutabazi alikimbia Rwanda baada ya kutuhumiwa kushirikiana na aliyekuwa mkuu wa jeshi la nchi hiyo ambaye alitofautiana na Kagame na kukimbilia Afrika Kusini, Jenerali Kayumba Nyamwasa lakini taarifa iliyotolewa na Polisi nchini Uganda ilieleza kwamba anatafutwa na Serikali ya Rwanda kwa kosa la Ujambazi wa kutumia silaha.

Yeye ni miongoni mwa watu waliokimbia jeshini mwaka juzi baada ya kubainika kumuunga mkono Jenerali Nyamwasa na kuwepo kwa taarifa kwamba huenda akawa miongoni mwa wanaotafutwa ili wauawe.

Polisi ilieleza kwamba taarifa rasmi ya kutaka akamatwe na kurejeshwa Kigali ilitumwa na polisi wa kimataifa, Interpol mjini Kigali.

Msemaji msaidizi wa Polisi, Patrick Onyango alisema Polisi wa Uganda walipata taarifa za kuwepo kwa mtuhumiwa huyo mkimbizi kwenye hoteli moja nje kidogo ya Kampala ambapo walimkamata.

Serikali ya Rwanda imekuwa katika mvutano wa muda mrefu sasa na baadhi ya maofisa wake wa juu wa kijeshi ambao wameonesha kuwa na mtazamo tofauti na Rais Kagame, na kulazimika kukimbia nchi ili kuepuka kukamatwa.


Chanzo:- Gazeti la mwananchi


No comments:

 
 
Blogger Templates