Social Icons

Monday, 13 October 2014

HADITHI: Nilioa jini nikamsaliti - 35


Aliendesha gari na kwenda moja kwa moja ofisini kwa Thabit na kuingia ndani. Thabit alipomuona alishtuka na kumuuliza:
“Subira ulikuwa wapi?”
“Thabit naomba unisamehe.”
“Nimekusamehe, kaendelee na kazi.”
“Hapana kuna kitu nataka kuzungumza na wewe.”
“Kitu gani?”
SASA ENDELEA...“

Kuhusu mimi na wewe.” 
“Kitu gani hicho?”
“Eti mimi na wewe tupo vipi?”
“Subira swali gani hilo?” Thabit alishangaa.

“Thabit naomba kuanzia leo uendelee na mkeo Nargis, mimi si mkeo.”
“Kwani wewe ndiye unayeongoza maisha yangu kwanza nani kakupa jeuri ya kusema hivyo?”
“Na kazi ndiyo mwisho.”

“Mbona sikuelewi, kama umeamua mwenyewe sawa.”
Subira alishangaa na kuamini kila chenye mwanzo kina mwisho, kwa hali ile ilionesha Thabiti alirudi katika hali yake ya kawaida. Hakuongeza neno alinyanyuka na kutoka nje ya ofisi. Kabla ya kuvuka mlango wa kutoka nje alifumba macho na kutoka, ghafla alijikuta kwenye nyumba nzuri. Hakuamini alibakia amesimama kama mgeni, mara alisikia hodi.

Hakujibu haraka, aliusogelea mlango na kuufungua, alishtuka kumuona Nargis akiwa amesimama.
“Ka...ka...ribu,” aliingia wasiwasi.
“Asante,” Nargis alisema huku akiingia ndani.

“Ka...karibu,” Subira alimkaribisha huku akitetemeka. 
“Acha woga, hukuogopa ulipotaka kuniua uniogope nikiwa hivi.”
“Sa...sa...mahani dada Na...na...”
“Nargis,” Nargis alimalizia jina lake.
“Karibu dada.”

“Asante,” Nargis alijibu huku akikaa.
“Dada mimi ndo’ nafika hata sijui nyumba ikoje,” Subira alizungumza kwa unyenyekevu.
“Utajua kwa vile ni kwako, mi si mkaaji nimekuja kukumbusha tena achana kabisa na mume wangu ukijitia kiburi cha nazi kushindana na jiwe sitakuua nitakugeuza nzi wa chooni  maisha yako yote yatakuwa kwenye kinyesi.”

“Dada nakuapia kuanzia leo sitamfuata mumeo, nashukuru kwa kunisamehe kwa ubaya wote niliokufanyia.”“Hilo si la muhimu kwangu zaidi ya kukukanya kwa mara ya mwisho.”
“Nakuahidi sitamsogelea tena, hivi nimetoka kumweleza pia kuacha kazi.”
“Nashukuru kama umenielewa.”

Baada ya kuachana na Subira, Nargis alirudi moja kwa moja ofisini kwa Thabit ili kuhakikisha kama kweli dawa za Subira alizopewa na mganga zimefanya kazi. Baada ya kufika eneo la ofisi za Thabit alitembea taratibu. Alijishangaa alivyokuwa mwepesi kila alivyotembea tofauti na siku za nyuma.

Alimsalimia mlinzi ambaye alimpokea na kujikuta akimuuliza.
“Shemeji ni wewe?”
“Ni mimi John.”
“Karibu.”

“Asante, mheshimiwa yupo?”
“Ndiyo.”
Wakati huo Nargis alikuwa ameishamweka jini sehemu ya mapokezi mwenye sura ya Subira ili asiwachanganye watu. Alipomuona alimkaribisha.
“Karibu binti wa mfalme.”

“Asante,” Nargis alijibu huku akiingia ofisini  kwa Thabit.
Wakati huo Thabit alikuwa ameinama akiishangaa picha yake na Subira ambayo ilimshangaza sana kila alivyojiuliza alikosa jibu. Alijiangalia mkononi na kutandaza vidole kuangalia pete aliyoachiwa na mpenzi wake haikuwepo. Alijuliza kipi kimepita kwani alishindwa kuelewa nini kinaendelea.

Moyo wake ulijaa wasiwasi na kujiuliza kama mkewe Nargis angetokea siku ile na kukuta hali ile lazima angeonekana msaliti.  Alipata wazo la kuziondoa picha zote alizokuwa amepiga na Subira wakionekana wapenzi kitu ambacho yeye kwa akili zake alikuwa hakumbuki kabisa kama aliwahi kuwa na uhusiano na mwanamke yeyote zaidi ya Subira.

Akiwa bado katika dimbwi la mawazo aliisikia sauti ya Nargis siku alipokuwa akiondoka kwenda kwao ujinini kujifungua: “Thabit naondoka nikiwa nimekuachia utajiri mkubwa ambao hutaumaliza mpaka unakufa, unajua kiasi gani nilivyopigana na majini wenzangu na wanadamu kukulinda. 

Nina dhambi ya kuua majini na wanadamu kwa ajili yako. Nimewatia wanadamu na majini vilema ambavyo watakufa navyo kwa ajili yako. Thabit naondoka nakuacha peke yako, kwa utajiri ulionao una mtihani mzito kwa wanadamu kila mwanamke atakutaka wapo watakaokuendea kwa waganga ili wakupate. Kipindi changu cha kujifungua sitaweza kutoka mpaka miaka kumi hivyo sitakuwa karibu na wewe tena.

“Mpenzi naomba usinisaliti nimechoka kubeba dhambi za wanadamu na majini kwa ajili yako. Nakuomba baada ya kuondoka kaa mbali na wanadamu, mafuta niliyokuachia siku ukinikumbuka sana jipake usiku wakati wa kulala utaniota usingizini lakini hatutaonana mpaka miaka kumi ipite,” Nargis alisema kwa hisia kali.

“Nakuahidi kuwa muaminifu kwako, sitakusaliti nakupenda sana Nargis, nilitamani niwapokee wanangu wakati wa kuzaliwa lakini sina jinsi. Nenda mpenzi wangu ukijua nakupenda kuliko kiumbe chochote kilichoumbwa na Mungu. Nakuahidi kukusubiri hata kwa miaka mia moja,” Thabit alimuahidi Nargis.
“Kweli Thabit?” Nargis alimuuliza Thabit huku akimkazia macho yake makubwa lakini yenye urembo wa ajabu.

“Kweli kabisa.”
“Hutanisaliti?” alimuuliza tena.
“Siwezi.”

Baada ya kuyakumbuka maneno ya zaidi ya miaka kumi iliyopita alijikuta mapigo ya moyo yakimwenda mbio na kujiuliza Nargis akitokea na kuona zile picha alizopiga na Subira atamuona mnafiki na muongo. Wazo lilikuwa kuzitoa picha zote na kuzichoma moto.

Akiwa katika mawazo mazito alisikia mtu akibisha hodi, alitulia bila kujibu huku macho yake yakitua kwenye picha kubwa ya Subira akiwa katika tabasamu pana iliyokuwa mbele yake ambayo siku ile lilikuwa tabasamu baya kama amemuona mtoa roho mbele yake.

itaendelea

No comments:

 
 
Blogger Templates