Aliyahamisha macho yake toka kwenye tumbo lake na kumuangalia mumewe Thabit aliyekuwa katikati ya usingizi. Aliinama na kumbusu shavuni na kurudi kukaa kitako. Alijikuta akibubujikwa na machozi bila kizuizi.
Siku ile ilikuwa ngumu maishani kwake kutengana na mumewe waliyezoeana na kuishi kama mke na mume kwa muda mrefu. Pamoja na kuwa jini lakini alimpenda sana mwanaume yule kuliko kitu chochote chini ya jua na maji.
Alikumbuka mpaka kufika pale, alimpigania Thabit kwa hali na mali kwa muda mrefu kwa vita kali na nzito toka kwa wanadamu na majini wenzake waliyoyatamani maisha ya mpenzi wake.
Ili kuhakikisha anamlinda mpenzi wake iliyagharimu maisha ya wanadamu na majini kwa kuwaua.
Aliweza kuishi na mumewe maisha ya raha mustarehe baada ya kutokwa na jasho na machozi ya damu. Matunda ya kwanza yalikuwa kupata ujauzito alioutamani usiku na mchana kwa kuamini ile ndiyo sababu ya kuishi naye milele.
Baada ya kupata ujauzito wazazi wake walimweleza arudi haraka ujinini akailee mimba yake ili wanadamu wasiichezee. Lakini aliwaomba sana abakie duniani mpaka ikibakia wiki mbili kujifungua ndipo aende.
Wazazi wake walipinga, lakini aliwapa masharti yaliyokuwa magumu kwao kuwa aende na mumewe ambaye hakutakiwa kwa kipindi kile. Baada ya kushindwa masharti ya mtoto wao walikubaliana naye akae mpaka akibakiza wiki mbili kujifungua ndipo aende.
Sharti lingine lililomuumiza akilini Nargis ni kukaa miaka kumi chini ya bahari baada ya kujifungua ndipo atoke kurudi duniani na kuishi na familia yake japokuwa wazazi walitaka watoto waendelee kuishi ujinini mpaka watakapokuwa wakubwa.
Kwa mapenzi aliyokuwa akimpenda Thabit hakutaka kumuacha, alitaka aende naye akaishi naye kipindi chote cha kujifungua na kulea watoto wao. Lakini familia yake ilimruhusu kitu kimoja kuolewa na mwanadamu tu na si kumpeleka mwanadamu kuishi ujijini kipindi kirefu. Alijikuta akilia kwa zaidi ya saa nzima kutokana na maumivu ya moyo kwa kutengana na kipenzi chake.
Akiwa amezama kwenye lindi la mawazo, muda nao ulikuwa ukikaribia alikuwa na saa moja tu kuwepo duniani. Huko baharini majini waliokwenda kumpokea walikuwa wamejaa juu ya bahari huku wakiimba nyimbo tamu za kumkaribisha malaika wa majini Nargis. Alijizuia kulia na kumtikisa Thabit ili amuage kwa kumwita jina.
“Thabit…Thabit.”
“Mmh!” Thabit aliitika bila kufumbua macho na kujigeuza upande wa pili.
“Thabit mume wangu hebu amka basi,” alisema huku akimtikisa.
“Naam.”
“Hebu amka mwenzio nachelewa.”
“Ha! Kwani sasa ni saa ngapi?” Thabit alikurupuka usingizini.
“Nina nusu saa tu ya kuendelea kuwa hapa.”
“Mungu wangu! Mbona umechelewa kuniamsha?”
“Nisamehe mpenzi wangu.”
“Mbona macho yamevimba?”
“Acha tu, Thabit sikupenda kuwa mbali na wewe kwa kipindi kirefu, kitendo walichonifanyia wazazi wangu kimeniumiza sana. Kama walikubali uwe mume wangu kwa nini hawataki tukae wote kipindi cha kujifungua na kulea watoto wetu?” Nargis alianza kulia tena.
“Hatuna budi kukubaliana nao, hata mimi najua nitateseka sana, miaka kumi ni mingi sana Nargis, nitakuwa mpweke sana. Pamoja na kukupenda lakini ulikuwa mtu muhimu sana katika maisha yangu, nilikuzoea sana, nitacheka na nani na nitacheza na nani?” Thabit alijikuta akizungumza sauti ya kilio kutokana na kutengana na mpenzi wake Nargis.
“Hilo hata mimi linaniumiza, lakini naomba uniombee nijifungue salama.”
“Nitakuombea siku zote.”
“Thabit naondoka nikiwa nimekuachia utajiri mkubwa ambao hutaumaliza mpaka unakufa, unajua kiasi gani nilivyopigana na majini wenzangu na wanadamu kukulinda.
“Nina dhambi ya kuua majini na wanadamu kwa ajili yako. Nimewatia wanadamu na majini vilema ambavyo watakufa navyo kwa ajili yako.
“Thabit naondoka nakuacha peke yako, kwa utajiri ulio nao una mtihani mzito kwa wanadamu, kila mwanamke atakutaka, wapo watakaokuendea kwa waganga ili wakupate. Kipindi changu cha kujifungua sitaweza kutoka mpaka miaka kumi hivyo sitakuwa karibu na wewe tena.
“Mpenzi naomba usinisaliti nimechoka kubeba dhambi za wanadamu na majini kwa ajili yako.
Nakuomba baada ya kuondoka kaa mbali na wanadamu, mafuta niliyokuachia siku ukinikumbuka sana jipake usiku wakati wa kulala utaniota usingizini lakini hatutaonana mpaka miaka kumi ipite,” Nargis alisema kwa hisia kali.
“Nakuahidi kuwa muaminifu kwako, sitakusaliti nakupenda sana Nargis, nilitamani niwapokee wanangu wakati wa kuzaliwa lakini sina jinsi. “Nenda mpenzi wangu ukijua nakupenda kuliko kiumbe chochote kilichoumbwa na Mungu. Nakuahidi kukusubiri hata kwa miaka mia moja,” Thabit alimuahidi Nargis.
“Kweli Thabit?” Nargis alimuuliza Thabit huku akimkazia macho yake makubwa lakini yenye urembo wa aina yake.
“Kweli kabisa.”
“Hutanisaliti?” alimuuliza tena.
“Siwezi.”
“Na hii nyumba ya baharini kuanzia leo utaihama na kwenda kuishi kwenye nyumba tuliyojenga. Naogopa kukuacha hapo unaweza kufanya kosa nyumba ikayeyuka na wewe kufa maji. Sitaki kukupoteza mpenzi wangu nakupenda sana.”
“Nitajilinda kulilinda penzi letu.”
“Basi amka tukaoge ili niwahi, wenzangu wamefika zaidi ya saa nne kunisubiri.”
Walikwenda kuoga kisha alibadili nguo na kuvaa mavazi ya kijini na kumkumbatia Thabit wote waliruka hadi pembeni ya bahari ambako walikuta bahari ikimeremeta kwa mishumaa iliyokuwa imebebwa na majini.
Walitembea wameshikana mkono kama siku ya harusi yao mpaka walipokaribika kwenye kina kirefu, waliagana kila mmoja alilia kutengana na mwenzie.
Nargis kabla ya kuondoka alisema neno moja la mwisho.
“Thabit nakupenda sana usinisaliti, kwa heri.”
Ghafla juu ya bahari kiza kizito kilitokea, Thabit alijiona kama akizamishwa ndani ya bahari.
Itaendelea kesho
No comments:
Post a Comment