Social Icons

Friday, 12 September 2014

HADITHI: Nilioa jini nikamsaliti -13


“Majini wana hasira baada ya kushindwa kumrudisha Thabit kwao wameamua kuharibu mali zake ili arudi katika umaskini.”

“Kwa hiyo na yale maduka nayo yatateketea?”
“Yale yatakuwa salama hawataweza kufanya chochote kwa vile tumewahi tungechelewa ingekuwa kilio cha kusaga meno.”
SASA ENDELEA...

Wakati wakizungumza walishangaa moto kuzimika ghafla na kujikuta wote wakishangaa.
“Mmh! Mbona moto umezimika ghafla?” aliuliza subira na kumfanya mzee Mukti naye kushangaa.
“Hii ajabu!”

Waliteremka kwenye gari na kuelekea kwenye duka lililokuwa sehemu ya chini, kama kawaida alianza kufanya dawa zake kwa nje ya duka kisha aliingia ndani. Walipoingia ndani walishtuka kukuta vitu vyote vimeteketea kwa moto. Ajabu ilikuwa vilivyoungua ni vitu vyote vya dukani tu lakini ndani hakukuwa na dalili za moto kuwaka.

“Mungu wangu mbona maajabu haya,” Subira alisema huku akishika mikono kichwani.
“Ule moto ni wa kijini ambao huaribu kilichokusudiwa tu.”
“Jamaniiii!” Subira alisema kwa sauti ya kukata tamaa.
“Huku tumechelewa, hatuna jinsi turudini nyumbani.”

Kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana waliingia kwenye gari na kurudi nyumbani. 
                                                             ***
Subira ilibidi akae kimya kuhusiana na tukio zito la usiku ule huku akiwa haamini kama kweli moja ya duka la Thabit lilikuwa limeunguzwa na moto wa kichawi.  Walilala mpaka asubuhi ili asikie nini kimetokea au ilikuwa ndoto na wala hakuna kilichotokea.

Asubuhi wakiwa bado wapo kitandani simu iliingia, Thabit aliichukua na kuweka sikioni na kupokea.
“Haloo Juma,” alikuwa msimamizi wa duka la Posta.
“Za asubuhi bosi.”
“Nzuri, kwema.”

“Si kwema bosi.”
“Kuna nini?”
“Duka limeungua lakini moto wake wa ajabu.”
“Mungu wangu! Jengo zima limeungua?” Thabit alitaharuki.
“Siyo jengo lote ni duka letu tu.”

“Hakuna hata kimoja kimepona.”
“Kumebakia majivu tu.”
“Na maduka ya mjini?”
“Huko sijui.”
”Subiri.”

Alikata simu na kupiga mjini, baada ya kuita kwa muda ilipokelewa.
“Haloo bosi.”
“Sadiki upo wapi?”
“Kazini.”
“Kwema?”

“Kwema, tena bosi lile kontena nasikia linatua kesho usiku, nina imani tutatumia mwezi mzima na kazi ya kupakua na kupanga vitu madukani.”

Kutokana na nguvu za kijini zilizowekwa na jini Nargis kwa mumewe kila kukicha utajiri wa Thabit ulikuwa ukikua kutokana na kuwa karibu kiutendaji na majini waliosimamia mali zake chini ya usimamizi wa mkewe.

Zaidi ya maduka yale matatu, alikuwa amepanga kufungua maduka makubwa ya vyakula kila wilaya pia duka kubwa sana maeneo ya kituo cha daladala cha Mwenge, lingine kubwa kuliko yote City Center. Alikuwa ameagiza kontena kumi za bidhaa mbalimbali. Kati ya maduka hayo matatu la City center matano, la Mwenge matatu na mengine mjini.

Ndoto ya Nargis kuhakikisha Thabit anakuwa tajiri mkubwa dunia hiyo alipanga atakaporudi duniani na kuishi na mumewe kama mwanadamu wa kawaida basi wawe na maisha mazuri. Kila kukicha alihakikisha utajiri wa Thabit unazidi kuongezeka na si kupungua.

“Hakuna tatizo lolote.”
“Hakuna tupo shwari.”
“Sawa.” 
Alikata simu na kupiga duka lingine na kukuta nako hali shwari, alirudia kupiga tena Posta na kupokelewa.
“Naam bosi.”

“Kuna mabadiliko yoyote?”
“Hakuna.”
“Nakuja.”
“Sawa.”
Alikata simu na kuteremka kitandani kitu kilichofanya Subira aulize.
Mpenzi mbona umeamka haraka hivyo?” Subira alijifanya hajui kitu.
“Kuna tatizo.”
“Tatizo gani?”

“Sijajua ila nimeambiwa niende duka la Posta.”
“Twende wote,” Subira alisema huku akinyanyuka kitandani na kumfuata Thabit, walikwenda bafuni kuoga na kutoka pamoja hata kifungua kinywa hawakunywa siku hiyo.

Waliingia kwenye gari na kuelekea Posta, walikwenda hadi eneo la tukio na kukuta nje ya jengo kazi zikiendelea kama kawaida hakukuwa na mshtuko wowote kama kuna tukio kwani jengo lilikuwa katika hali ya kawaida hakukuwa na dalili zozote za moto kutokea. Aliwakuta wafanyakazi wake zaidi ya arobaini wakiwa ndani ya jengo wakiwa wameshika tama na wengine kutoka machozi.

Walishangaa kukuta ndani ya duka kumejaa jivu vitu vyote vya mamilioni ya fedha vikiwa vimeteketea. Ilikuwa ni hasara kubwa kwani ilikuwa ni wiki tu aliingiza dukani mali ya zaidi ya milioni mia sita na nusu. Alijisikia miguu kumwisha nguvu lakini alijikaza na kujiuliza kile ni kitu gani, kwani kuta na sakafu za duka zilikuwa hazioneshi dalili zozote za kuungua na moto ulioteketeza mali ya mamilioni.

Wote walikuwa wapo kwenye usiku wa giza kasoro Subira alikuwa akijua kila kitu na sababu ya kuwa vile. Alimshukuru kimoyomoyo mzee Mukti kwani kama angechelewa maduka yote yangeteketea na kuwa kilio cha kusaga meno. Kutokana na dawa alizolishwa Thabit na Subira alijikuta akisahau kabisa chanzo cha mali ile ni mkewe jini Nargis.

“Hii si bure lazima kuna mkono wa mtu,” alisema mmoja wa wafanyakazi.
“Wameona sisi ndiyo tunafanya vizuri hivyo lazima wametuendea mbali, moto gani usiounguza sehemu yoyote zaidi ya bidhaa za dukani wanataka tukale wapi?” msichana mmoja alisema huku akili.

Itaendelea 

Chanzo globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates