Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Kwa ufupi
Alisema mizigo ikishaondoka mikononi mwa abiria hukaguliwa tena kwa kutumia mbwa wa Idara ya Usalama wa Taifa, lakini siku ya tukio hilo mbwa hao walichelewa na walitumika baada ya mizigo kuingizwa kwenye masanduku ya chuma.
Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe jana ameanika majina ya watu saba waliohusika kupitisha mabegi tisa yaliyokuwa na kilo 180 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh8 bilioni, Julai 5 mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wakiwamo maofisa usalama wanne wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na polisi mmoja.
Alisema mizigo ikishaondoka mikononi mwa abiria hukaguliwa tena kwa kutumia mbwa wa Idara ya Usalama wa Taifa, lakini siku ya tukio hilo mbwa hao walichelewa na walitumika baada ya mizigo kuingizwa kwenye masanduku ya chuma.
“Kwa abiria watatu kuwa na mabegi makubwa tisa yanayofanana si kitu cha kawaida kukwepa jicho la maofisa wa ushuru wa forodha na vyombo vya usalama, sijui walikuwa wapi siku hiyo?” alihoji Mwakyembe.
Juzi waziri huyo aliahidi kuyaweka hadharani majina ya watu wanaosafirisha dawa za kulevya nchini, na alitekeleza ahadi hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, kusema kuwa watu hao wamenaswa baada ya mfumo wa kamera (CCTV) za uwanja huo kudaka matukio kadhaa yaliyotokea siku ya tukio hilo, kuanzia saa 9:25 hadi saa 10:30 alfajiri.
Ameagiza wafanyakazi hao wanne pamoja na askari polisi mwenye cheo cha koplo, mbeba mizigo na mfanyabiashara aliyekuwa na wasichana wawili waliokamatwa Afrika Kusini, (ambao hatuwezi kuwataja kutokana na kushindwa kuwapata kujieleza) kuchukuliwa hatua za kinidhamu, kukamatwa na kuunganishwa na watuhumiwa waliokwenda na mzigo huo Afrika Kusini.
Mabegi hayo yaliyokuwa na dawa za kulevya aina ya ‘Crystal Methamphetamine’, yalipitishwa na wasichana wawili wasanii aliowataja kuwa ni Agnes Gerald ‘Masogange’ na Melisa Edward ambao walidakwa siku hiyohiyo katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Afrika Kusini na tayari wameshafikishwa mahakamani.
Juzi Dk Mwakyembe alifanya ziara JNIA kukagua utendaji kazi kwenye uwanja huo ikiwa ni siku tatu baada ya ahadi aliyotoa akiwa Mwanza kwamba katika kipindi cha wiki mbili, atahakikisha anawakamata vigogo wote walio katika mtandao wa usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya kupitia viwanja vyote vya ndege nchini.
Saa nane baada ya ziara hiyo, Maofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wanadaiwa kumkamata Edwin Monyo akiwa na kete 86 za dawa aina ya heroini na misokoto 34 ya bangi aliyokuwa akiisafirisha kwenda Italia kupitia Zurich.
Mpango ulivyosukwa
Alisema siku ya tukio saa 9:28 kamera hizo za usalama zilimwonyesha mbeba mizigo wa uwanja huo akiwa anazungukazunguka eneo la kuingilia abiria kama mtu ambaye ana ahadi na kukutana na mtu fulani.
“Kamera pia zilimnasa ofisa mwingine wa TAA kwa mara kadhaa akitoka na kuingia ndani ya jengo la abiria huku akizungumza na simu, kitendo ambacho hakiruhusiwi kabisa kwa wafanyakazi wa eneo la ukaguzi wa abiria,” alisema na kuongeza;
“Wakati huohuo, kamera zilikuwa zinamwonyesha askari polisi anayetuhumiwa kuhusika katika mpango huo akiwa anarandaranda eneo la uhakiki wa hati za kusafiria kama vile anasubiri kitu fulani.”
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment