Social Icons

Saturday, 17 August 2013

NDUGU ZETU WAALIMU

NENO LA LEO; ENYI WALIMU ' WATAKATIFU'...

 Ndugu zangu,
 Umezinduliwa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ( MMMS) kwenye Sekta ya Elimu.  Kwa kimombo unaitwa ‘ Big Results Now’ ( BRN).
Kwa lugha nyingine ni mpango wa ‘ Mavuno Makubwa Sasa’. Na mkulima anayetarajia mavuno makubwa ya mahindi  ni lazima awe amefanya makubwa matatu; kulima shamba lenyewe, kupanda mbegu bora na kulipalilia vema shamba lake.

Na jana nilipokuwa nikifuatilia ‘ live’ TBC1 uzinduzi ule wa ‘ Mavuno’ makubwa sasa nilijiuliza; Je, maofisa wale wa elimu wa mikoa wenye kula kiapo hadharani kuhakikisha ‘ mavuno’ makubwa yanapatikana SASA walielewa hasa  changamoto ya jukumu walilotwishwa la kuhakikisha tunapata ‘mavuno’ makubwa sasa.

 Maana, kiapo kile kingeweza pia kuwa ‘ ungamo’ la dhambi tuzitendazo zenye kupelekea kila mwaka tupate ‘ mavuno’ hapa na wakati mwingine kuambulia debe mbili tatu tu kwenye ‘ mavuno’ yetu ya elimu. Niaonavyo, sambamba na mpango huu ulioandaliwa kwa dhamira njema kabisa, bado kunahitajika Mjadala Mkubwa wa Kitaifa kujadili namna ya kuinasua elimu yetu kutoka hapa tulipo.

Maana, inabaki, kuwa dhumuni kubwa la maisha ya mwanadamu ni kufanya juhudi za kutafuta namna ya kuyaelewa mazingira yake na hivyo kupiga hatua za maendeleo. Na juhudi hizo za mwanadamu  ndicho chenye kujulikana kama ‘ Elimu’. Naam, mwanadamu anapaswa aitafute elimu, hivyo basi, maarifa.

Na shule  yaweza kutafsiriwa kuwa ni ‘ Maabara’ ambamo hutengenezwa ‘ chanjo’ ya maradhi ya kimaisha kwa mwanadamu. Wale wenye maarifa na busara  za kuandaa ‘ chanjo’ hiyo  ndio wanaoitwa walimu.

Maana, shule ni mahali pa kujifunzia, ambapo yote yenye kuhusiana na maisha  ya sasa na hata yajayo hufundishwa. Ni mahali ambapo hupatikana tafsiri za vitu na matukio katika jamii. Ni mahali ambapo, mbali ya mambo mengine,  mwanafunzi anapaswa kusaidiwa kuweza kupata maarifa ya kujitambua na kuyatambua mazingira anamoishi.
Twaweza kabisa kusema, kuwa shule ni mahali pa ‘ ibada’. Na ‘ viongozi watakatifu’ wenye kupaswa kuongoza ‘ ibada’ hizo ni  WALIMU.

Hivyo, enyi walimu ‘ watakatifu’ , mnapaswa kuianza sasa kazi ya kuitambua nafasi yenu katika jamii. Vile vile, kulitambua jukumu lenu, vinginevyo, Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa yumkini yaweza kuwa sawa na mkulima anayesubiria ‘ mavuno’ makubwa sasa ilihali  shamba alilolima ni dogo. Amepanda mbegu dhaifu  na ameshindwa hata kupalilia shamba lake.

                                                Ni Neno La Leo.
                                                       Maggid,
                                                   0754 678 252
                                            http://mjengwablog.com

No comments:

 
 
Blogger Templates