Social Icons

Wednesday, 11 September 2013

MWAKYEMBE, MAGUFULI KUKWEPA RUNGU LA PAC...



WAZIRI wa Uchukuzi na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe pamoja na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli ambaye pia ni Mbunge wa Chato, wanasifika kwa utendaji kazi na kulinda maadili ya taifa. Katika nyakati tofauti, wamekuwa wakizungumzwa na Watanzania kuwa wanafaa kuchukua uongozi wa juu kabisa ikiwemo urais, ingawaje wenyewe hawakuwahi kutangaza nia hiyo.

Magufuli na Mwakyembe kwa namna nyingine si kitu rahisi kuwahusisha na ukosefu wa maadili, ikiwemo ulaji rushwa, ubadhirifu au matumizi mabaya ya madaraka yao.

Lakini hali imekuwa tofauti, baada ya Ripoti ya Kamati ya PAC chini ya Uenyekiti wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe. 

Mwenyekiti wa PAC, Zitto anasema kuwa mawaziri hao wanatakiwa kujibu tuhuma zao wanazokabiliwa nazo, kutokana na Kamati yake kubaini udanganyifu kwenye Bajeti ya mwaka wa fedha uliopita, wakati wakiwa wote kwenye wizara ya Ujenzi, hivyo huenda ikaisumbua Serikali kwa ujumla wake.

“Kimsingi Serikali ilidanganya Bunge, ili Bunge lipitishe bajeti ya Wizara ya Ujenzi ya mwaka 2011/12. Mawaziri John Magufuli na aliyekuwa Naibu wake, Harrison Mwakyembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Sera na Uratibu, William Lukuvi kwa nyakati tofauti walidanganya Bunge ili kupitisha jumla ya shilingi bilioni 252,” anasema Zitto Kabwe.

Anaongeza kuwa, “PAC imeamua mawaziri hawa waende Kamati ya Maadili ya Bunge ili kujieleza na kuadhibiwa kwa uwongo wao.” 

Aidha, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alinukuu utetezi wa mawaziri hao, akisema kuwa mwaka 2011, Waziri Magufuli, alisema: “Tunaomba fedha Tsh bilioni 252 kwa ajili ya kuanza kazi za ujenzi wa barabara.”

Mwaka huo huo, naye aliyekuwa Naibu Waziri, Dk. Mwakyembe alisema: “Fedha hizi zitachangia miradi ya wafadhili.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Sera na Uratibu, William Lukuvi, anadaiwa kusema: “Hizi ni fedha kwa ajili ya ‘counterpart fund.” 

Hata hivyo Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), mwaka huu (2013), inayoongozwa na Mkaguzi mkuu, Ludovic Utoh imesema: “Hizi fedha ni za miradi na kasma kivuli.” 

Aidha, Waziri Magufuli ananukuliwa kutoa utetezi kuwa fedha hizo zilitumika kulipa madeni, huku Katibu mkuu wa wizara hiyo naye akisema walilipa madeni. 

Kwa mujibu wa Zitto Kabwe ni kwamba, Kamati ya PAC, inahoji ni kwanini Waziri Magufuli, Mwakyembe na Lukuvi walilidaganya Bunge? 

Kwanini waliomba fedha za kuanza miradi maalumu, badala ya kuomba fedha za kulipa madeni? Kwanini waliunda kasma kivuli na kuifuta mara baada ya pesa kulipwa? 

Kutokana na hoja hizo, Kamati ya PAC imechukua uamuzi wake kwa kumwagiza CAG akague fedha zote za kasma kivuli na kuripoti fedha zimekwenda kwa wakandarasi gani na kutoa taarifa kwenye Kamati ya PAC ifikapo mwezi Oktoba. 

Pia, Mawaziri wote waliodanganya Bungeni watashtakiwa Kamati ya Maadili kwa kudanganya bunge kwa lengo la kupitisha bajeti ya Tshs bilioni 252 kufadhili miradi hewa. 

Katika hali hiyo, maelezo ya kamati ya PAC inatokana na namna Bajeti nzima ilivyotamka na kushindwa kufanyia kazi kile kilichotakiwa kufanyika. 

Kwa mantiki hiyo, hali hii inazua sintofahamu juu ya hatima ya Waziri Mwakyembe na Waziri Magufuli pamoja na mwelekeo wa kisiasa. 

Kwa upande wa Waziri Magufuli, aliwahi kulaumiwa wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa, kutokana na uamuzi wa Serikali kuuza nyumba zake. 

Hata hivyo, hilo haliwezi kuondoa uwezo na ufanisi wa Waziri Magufuli na pia kwa Mwakyembe. Lakini tatizo kubwa linalojitokeza ni namna ambavyo walivyosimama bungeni na kusoma hotuba hiyo kisha kuelezea jinsi wanavyopanga kutekeleza miradi ambayo haikufanyika na badala yake wamelipia madeni. 

Nani atasimama kati ya wanasiasa, tuliona na kukiri kwamba yeye anapaswa kuaminiwa ikiwa mawaziri hao walioaminiwa wameshindwa kuonyesha uaminifu wao ingawa uamuzi wao wa kulipa madeni ni mzuri, lakini ilipaswa Wizara ya Ujenzi iombe fedha za kulipa madeni na kueleza yametokana na nini. 

Katika utumishi wa umma, hatua hii imechora picha hasi kwa mawaziri Mwakyembe na Magufuli, kiasi ambacho kinaweza kupoteza haiba yao kiuongozi na kisiasa. 

Kwa kawaida kama wizara ya ujenzi ilitaka kulipa madeni, ilipaswa kulieleza Bunge ili yote yafanyike kwa taratibu zinazoeleweka. 

Kwa muktadha huo, bado sintofahamu inazidi kuongezeka, huku alama za kuuliza zikisema, ‘Mwakyembe, Magufuli kunusurika rungu la PAC?” Je, nini hatima ya mawaziri hao mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge?

Chanzo :- Mtanzania.

No comments:

 
 
Blogger Templates