Katika pingamizi hilo, Ntimbwa aliwasilisha sababu tano za kupinga kesi hiyo ya katiba akidai kesi haiko mahakamani kkwa mujibu wa sheria kwa vile iko kinyume cha Katiba na Sheria ya Madaraka, Kinga na haki za Bunge.
Sababu nyingine ni kwamba kesi inapingana na kanuni za mwenendo wa makosa ya madai, kesi haieleweki inaleta usumbufu.
“Walalamikaji na wale waliounga mkono hawana haki ya kufungua kesi hii, wanaingilia shughuli za Bunge, amri zinazoombwa kutolewa haziwezi kutolewa kwa kuwa zinaenda kinyume na sheria za msingi,” ilisema sehemu ya sababu za kuwasilisha pingamizi hilo la awali.
Baada ya kuwasilisha pingamizi hilo upande wa walalamikaji ukiongozwa na Wakili Fulgence Massawe ulidai pingamizi walilipata Septemba 11 mwaka huu hivyo waliomba siku 21 wawasilishe majibu.
Wakili Ntimbwa aliomba upande wa walalamikaji upewe siku 14, maombi ambayo yalikubaliwa na jopo la majaji. Walalamikaji watajibu kabla ya Septemba 30 mwaka huu na mapingamizi yatasikilizwa Oktoba 18 mwaka huu.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika kilifungua kesi ya katiba wakipinga kauli ya Waziri Mkuu aliyotoa bungeni Mei mwaka huu akiruhusu Jeshi la Polisi kuwapiga raia wanaokaidi amri halali ya jeshi hilo.
Wadaiwa katika kesi hiyo namba 24 ya 2013 ni Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Chanzo Mtanzania.
No comments:
Post a Comment